Na Augustino Chindiye ,Tunduru
VIONGOZI,Wanachama na Wakereketwa wa Chama Cha Mapinduzi CCM Tarafa ya Nakapanya wametoa siku tatu kwa viongozi wa Chama hicho ngazi ya Wilaya kwenda kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua zikiwemo za kufukuzwa kwa kupigiwa kura za kuto kuwa na imani nao.
Tamko hilo limetolewa na wanachama hao katika kikao kilicho wahusisha viongozi wa Chama na jumuiya zake kilicho fanyika katika ukumbi wa ofisi ya Serikali ya Kata ya Namiungo kikiwa na nia ya kujadili mikakati ya kukinusuru chama hicho ili kisifanye vibaya katika chaguzi zijazo.
Sambamba na tamko hilo pia wanachama hao wametishia kutopiga kura katika uchaguzi ujao ama ikiwezekana watamuomba Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete awaruhusu wajiunge na kupiga kura katika Jimbo la Nanyumbu lililopo Mkoani Mtwara.
Wakiongea kwa jaziba wana CCM hao kutoka katika Kata za Nakapanya ambao waliongozwa na Mjumbe wa Mkutano wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Tunduru Likambale Omari, Shaib Akijo kutoka Kata ya Mindu, Yasini Kaweje kutoka Kata ya Ngapa na Mjumbe wa halmashuri Kuu ya CCM Wilaya Maimuna Bora kutoka Kata ya Muhuwesi walisema wameamua kuchukua maamuzi hayo baada ya kubaini kuwepo kwa ubabaishaji uliokithiri ndani ya Chama hicho huku kukiwa na taarifa za kubebana na kuwachagulia wananchi viongozi wanaotoa fedha kwao.
Aidha wanachama hao wakatolea mfano ubabaishaji wa taarifa za kuteuliwa kwa Diwani wa Viti Maalumu Wanawake wa Tarafa hiyo Salima Limbalambala ambaye mbali na kushiriki katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Faridu Khamisi baadae zilitolewa taarifa zenye utata za kutenguliwa kwa wadhifa huo na kuiweka Tarafa yao katika mkanganyiko ambao hadi leo Uongozi wa Chama hicho ngazi ya Wilaya haujatolea kauli yoyote ikiwa ni tofauti na walivyofanya baada ya kutenguliwa kwa udiwani wa Selemani Chisopa aliyetuhumiwa kufanyia kampeni vyama vya upinzani katika uchaguzi mdogo wa Kuziba nafasi ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tunduru Marehemu Juma Akukweti.
Nao Diwani mstaafu Hasan Futali, Dastan Amlima na Husen Ndayani ambao pamoja na mambo mengine walihoji vigezo na sababu za uhalali wa kutenguliwa kwa udiwani wa Salima Limbalambala ambaye jina lake lipo katika barua zilizo andikwa na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Taifa Rajab Kiravu na badala yake viongozi wa CCM Wilaya wakapendekeza na kumchagua Diwani wa Viti Maalumu wanaweke kutoka Tarafa ya Mjini Siwema Kalipungu ambaye hakupiga kura za Kumchagua mwenyekiti wa halmashuri huyo huku matokeo ya kuchaguliwa kwake yakiendelea kuheshimiwa.
Kwa ujumla maelezo ya viongozi hao Kero kubwa inayotembea vichwani na katika midomo yao ni Usimamizi mbovu wa Viongozi wa Chama hicho ngazi ya Wilaya ambao wamedai kuwa umeshindwa kusimamia haki kwa wanachama wake, hawafanyi mikutano ya uhamasishaji na wanasema uongozi huo kuwa umepoteza Dira na wakaendelea kutahadharisha kwamba endapo CCM Taifa itawaachilia waendelee kuiongoza Wilaya hiyo kuna hatari ya chama hicho kufanya vibaya zaidi katika chaguzi zijao ukiwewmo uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
Hata hivyo baada ya kutoa dukuduku zao hizo zenye maneno makali kwa uongozi wao ukafuata wasaa wa kutoa tamko la kuita kikao cha dhalula kilicho pangwa kufanyika Septembar 28 mwaka huu na kwamba watakao tolewa kafala katika kikaango hicho ni uongozi wa CCM Wilaya unao ongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Mustafa Bora, Katibu wa CCM Wilaya Ramadhan Amer. Katibu Mwenezi CCM Wilaya Hasan Kindamba.
Wakizungumzia mgogoro huo baadhi ya madadisi wa masuala ya siasa walisema kuwa kupotea kwa mwelekeo na utashi wa viongozi wa chama Tawala CCM kunatokana na mfumo mbovu wa ufuatiliaji na upembuzi wa viongozi wanao takiwa kuwekwa madarakani tofauti na mfumo wa wasisi wa taifa hili Baba wa taifa hayati Mwl. Julius Nyerere ambao wakati wao walikuwa makini nia viongozi wao na walikuwa wakihakikisha kuwa kiongozi anayefaa ni yule aliyepikwa na kuifa kisiasa.
No comments:
Post a Comment