Na Steven Augustino,Tunduru
WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamemuua kwa kumpiga mapanga mkulima wa kitongoji cha Mkangwala kilichopo katika kijiji cha Mbatamila Wilayani Tunduru aliyefahamika kwa jina la Bibie Mtenje (25) na kumjeruhi vibaya mume wake Kasim Shaibu (35).
Taarifa kutoka katika kijiji hicho zinaeleza kuwa baada ya watu hao kutekeleza uharamia huo walifanikiwa kupora fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni mbili pamoja na kuchoma moto nyumba ya jirani yake aliyetambulika kwa jina la Anafi Alifa aliyedaiwa kutoka na kupeleka taarifa kwa majirani wakati tukio hilo likiendelea.
Ndugu wa majeruhi Shaibu ,Bw.Sandali Shaibu na Kazembe Rajabu wanao muuguza majeruhi huyo aliyelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Tunduru akiwa hajitambui walisema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Septemba 21 mwaka huu.
Wakifafanua taarifa hiyo wanafamilia hao walidai kuwa fedha alizo porwa majeruhi na kusababisha kifo cha mkewe zilitokana na mauzo ya viroba 24 vya mpunga ambao walilima na kufanikiwa kuvuna msimu uliopita wakiwa na matumaini ya kujiletea maendeleo baada ya kuuza.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda mbali na kukiri kuwepo kwa tukio hilo alisema kuwa jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na kwamba endapo watabainika watu kuhusika na tukio hilo sheria itafuata mkondo wake.
Mganga wa hospitali ya Wilaya ya Tunduru Dkt. George Chiwangu ambaye alimpokea na kumshughulikia majeruhi Shaibu alisema kuwa, majeruhi huyo ameumizwa vibaya kichwani na sehemu za tumboni kutokana na kukatwa mara nyingi na mapanga.
Naye Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Mtenje, Dkt.Titus Tumbu alisema kuwa kifo chake kimesababishwa na kutokwa na damu nyigi zilizosababishwa na majeraha ya kukatwa na mapanga sehemu za kichwani.
Mwisho
No comments:
Post a Comment