About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Wednesday, September 21, 2011

MANISPAA YA SONGEA WAFANIKIWA KUDHIBITI MIMBA KWA WANAFUNZI WA SHULE ZA MSINGI

               Na Thomas Lipuka,Songea

IDARA ya Elimu  na wadau wa Elimu katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma,wamefanikiwa kuondoa tatizo la mimba kwa wanafunzi wa Shule za Msingi kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2011 ambapo hakuna mwanafunzi aliyepata mimba katika Shule zote za Msingi katika Manispaa hiyo.
Taarifa ya hali ya Elimu ya mwaka 2010/2011 iliyosomwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Zakaria Nachoa kwa wadau wa Elimu katika Ukumbi wa Songea Club hivi karibuni imebaini kuwa hakuna mimba iliyoripotiwa kwa wanafunzi wa Shule kwa Kata zote 21 za Manispaa hiyo.
Nachoa alisema mbinu iliyotumika katika kuzuia suala la mimba ni pamoja na ushirikiano wa karibú baina ya wazazi,walimu,wadau wa Elimu na Viongozi wa Elimu ngazi zote za Manispaa na hatimaye kufikia kufuta kabisa tatizo la mimba katika Shule za Msingi zote za Manispaa ya Songea.
Taarifa ya mandeleo ya Elimu katika Manispaa hiyo imetaja pia mafanikio zaidi yaliyojitokeza katika sekta ya Elimu ni pamoja na ufaulu kwa Wanafunzi waliomaliza Elimu ya Msingi 2010 ambapo Manispaa hiyo imekuwa ya kwanza Kimkoa, na kuzipita Wilaya za Songea,Mbinga,Namtumbo na Tunduru.
Hata hivyo changamoto kadha zimejitokeza katika tathmini elimu Manispaa ya Songea ambapo kuna uhaba wa vitabu vya kiada,jambo ambalo linapelekea kitabu kimoja cha kiada kutumiwa na wanafunzi 11 ama zaidi.
Changamoto zingine zilizotajwa katika tathmini hiyo ni uhaba wa walimu darasani, hivi sasa kuna walimu 820 wakati mahitaji ni walimu 1259 hivyo Manispaa ya Songea kuwa na upungufu wa walimu 439 darasani ,jambo ambalo linahitaji msaada toka Serikali kuu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea amewaambia wadau wa Elimu kuwa kuna upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa,vyoo na nyumba za walimu,ameomba wadau wa Elimu kujipanga kwa hatua za awali za ujenzi wa maboma ili wanafunzi wote watakao faulu 2011 waweze kupata nafasi kidato cha kwanza.
Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa madawati wadau wamesema ni vema kujipanga upya kwani suala la miti ya kutengenezea madawati lipo kwenye uwezo wao, isipokuwa Serikali iwezeshe Manispaa ya fedha kwa vifaa vya kiwandani ili kuondoa tatizo la madawati hatimaye wanafunzi wapate mazingira bora ya kujifunzia na kuleta usikivu,wanaposoma ili kuongeza ufaulu.
Mkurugenzi wa Manispaa pia alitoa taarifa ya maendeleo ya Elimu ya watu wazima mbele ya Mwenyekiti wa kikao cha tathmini Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Sabaya kuwa Manispaa ya Songea ina watu 2883 ambao hawajui kusoma kuhesabu na kuandika sawa na asilimia 40% ya watu wazima wote wa Manispaa hiyo ambapo Mkuu huyo wa Wilaya akatia mkazo kwa Kata zote kuendeleza kwa kasi Elimu ya watu wazima ili kufuta kabisa asilimia ya wasiojua kusoma,kuandika na kuhesabu katika Manispaa ya Songea.
“Naagiza kisomo sasa kipambe moto kata zote waratibu Kata,walimu wakuu,watendaji ngazi zote wajibikeni ipasavyo” alisisitiza Bwana Sabay.
Mwenyekiti huyo wa Kikao hicho ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Sabaya amewaagiza viongozi wa Elimu Manispaa,Waratibu Kata,walimu na wadau wa Elimu kusimamia kikamilifu malengo ya kukuza taaluma katika Manispaa kwa kuhimiza mahudhurio ya wanafunzi,walimu kufundisha kikamilifu,wakaguzi kufuatilia ufundishaji na viongozi kutekeleza wajibu wao kwa kutoa stahiki zote za walimu ikiwemo malipo ya likizo,matibabu na posho zao za kujikimu.

MWISHO

No comments:

Post a Comment