Daraja la Mkenda linalounganisha nchi ya Msumbiji na Tanzania
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu akiwa na Viongozi mbalimbali wakipita juu ya daraja la Mkenda wakielekea nchi jilani ya Msumbiji
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu akipata maelekezo ya ujenzi wa daraja linalounganisha nchi ya Msumbiji na Tanzania lililojengwa kivukoni Mkenda kutoka kwa Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Abraham Kissimbo
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu (katikati) akipokea maelezo ya jengo lililojengwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) kutoka kwa Meneja wa TRA mkoa wa Ruvuma Apily Mbaruku kushoto na Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Oley Sabaya kulia
Na Stephano Mango,Songea
WANANCHI wa kitongoji cha Mkenda kilichopo katika kijiji cha Nakawale kata ya Mhukuru wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Miundombinu kuona umuhimu wa kuwakumbuka kwa kuwajengea barabara kwa kiwango cha lami ili waweze kusafirisha bidhaa zao yakiwemo mazao ya kilimo kiurahisi.
Ombi hilo wamelitoa jana kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu wakati alipofanya ziara ya kutembelea kitongoji hicho kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambako Serikali imefanikiwa kujenga daraja la kudumu ambalo linaunganisha na nchi hiyo jirani katika mto Ruvuma.
Mmoja wa wakazi wa kitongoji hicho Ramadhani Hussein alisema kuwa kitendo cha Serikali cha kujenga daraja la Mkenda kwenye mto Ruvuma kumepelekea kuwepo kwa maendeleo makubwa kwa wananchi wa eneo hilo kutokana na biashara zinazofanyika kati yao na wananchi wa nchi jirani ya Msumbiji.
Hussein alisema kutokana na hali hiyo ni vyema Serikali ikafikiria kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Songea mjini hadi Mkenda yenye urefu wa kilometa 124 hali itakayokuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa tarafa ya Mhukuru ambayo ipo mpakani.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha FRELIMO kijiji cha Congress nchini Msumbiji John Bosko ambaye alihudhuria mkutano huo wa hadhara alimwomba Mkuu wa mkoa wa Ruvuma kufanya mawasiliano na Serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha kuwa barabara ya kutoka Songea hadi Mkenda inajengwa haraka na kwamba barabara kutoka Mkenda hadi Maputo inajengwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Kwa upande wake Meneja wa wakala wa barabara mkoa wa Ruvuma(TANROADS) Mhandisi Abraham Kissimbo alisema kuwa Serikali imedhamira kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kwamba mpaka sasa tayari michoro imekamilika na kinachosubiriwa ni utekelezaji.
Naye Mkuu wa mkoa wa Ruvuma aliwaeleza wananchi hao kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kufanyia matengenezo barabara zote zikiwemo za mipakani ili zipitike kiurahisi na kwamba aliwahimiza wananchi kujikita kwenye kilimo ili barabara hizo zitakapokamilika waweze kusafirisha mazao yao pamoja na bidhaa zingine.
Aidha Mwambungu aliwataka wakazi wa kitongoji hicho kujitokeza kwa wingi kuchangia nguvu zao kwenye ujenzi wa kituo cha polisi hasa ikizingatiwa kitongoji hicho cha Mkenda kipo mpakani mwa nchi ambapo kwa siku za usoni unatarajia kuwa mji mdogo hali itakayopelekea pia kuwepo na vitendo vya uharifu na kwamba alichangia shilingi milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
No comments:
Post a Comment