Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ardhi Plan Gombo Samandito akiwaonyeshwa wananchi RAMANI zilizopitishwa na Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya upimaji wa viwanja kata ya Mshangano
Na Joseph Mwambije,Songea
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma imezindua mradi wa upimaji viwanja zaidi ya 18,000 unaofanywa na Kampuni binafsi ya Ardhi Plan Limited kwenye Kata ya Mshangano baada ya kuibuliwa na wananchi wenyewe baada ya kuona wanaishi katika makazi holela kwa muda mrefu.
Mradi huo umezinduliwa juzi na Meya wa Manispaa ya Songea Charles Mhagama aliyewakilishwa na Mwenyekiti wa huduma za jamii na elimu wa Manispaa hiyo Genifrida Haule aliyekata utepe kuzindua mradi huo.
Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo Haule alisema Mradi huo utawainua kiuchumi wananchi wa Kata ya Mshangano kwa sababu wataweza kukopaa kupitia makazi yao na kwamba wataweza kuishi katika makazi bora,
‘Suala la upimaji viwanja ni hatua kubwa ya maendeleo kwa kuwa baada ya upimaji miundombinu ya maji na umeme itakuja na wananchi wameongeza kipato kwa kuweza kukopa na kuendesha miradi kupitia viwanja vyao na nyumba zao huku viwanja vikipandishwa thamani’alisema.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo Afisa Mtendaji wa Kata ya Mshangano Stan Kibiki alisema Kata hiyo ina Kaya 1508 zenye wakazi 7540 na mitaa mitano ya Mshangano,Namanyigu,Chandarua,Mitendewawa na Muhumbezi.
Alisema kuwa wananchi baada ya kuona kwa muda mrefu wanakaa na kuishi katika makazi holela yasiyopimwa wakaamua kuibua Mradi wa upimaji viwanja hasa baada ya kupeleka maombi ya kupimiwa viwanja Halmashauri lakini ilishindwa kuwapimia kwa kile ilichodai kuwa haina fedha.
“Mwaka 2010 Kata yetu ilipata bahati ya kupata mradi wa upimaji viwanja ulioendeshwa na Manispaa ya Songea lakini fedha ilikuwa kidogo na hivyo waliweza kupima viwanja 347 tu katika Mtaa mmoja wa Namanyigu katika eneo dogo na hivyo tatizo la wananchi kuishi katika makazi holela likabaki palepale’alisema katika taarifa hiyo.
Alisema kuwa wananchi katika kutatua tatizo hilo kwa kushirikiana na viongozi wao waliamua kutafuta njia mbadala kwa kutumia sheria namba 8 ya ya mipango miji ya mwaka 2007 walitafuta Kampuni ya Ardhi Plan Limitedya Dares-salaam ili iweze kuwapimia viwanja katika maeneo yao.
Alisema Mitaa ambayo michoro yake imekamlika ni Mshangano,Namanyigu, na Mitendewawa yenye jumla ya viwanja 18,000 na mitaa mingine itafuata baadaye na kufafanua kuwa mchoro namba 9 wa Beroya wenye viwanja 800 umekamilika na kazi ya kuchonga barabara inaendelea.
Afisa Mtendaji huyo alisema mradi huo umesaidia kutoa ajira kwa wananchi kwa kuwa mchoro mmoja umetoa ajira kwa wananchi 40 ambao walikuwa wanalipwa sh. 4000 kwa kutwa na kwamba michoro23 ya mradi huo itatoa ajira 920.
Alisema katika uchongajio barabara mchoro mmoja unatoa ajira kwa watu 80 ambapo kila mmoja analipwea sh. 5000 na kwamba wananchi 2760 wanawake na wanaume watakuwa wamepata ajira katika zoezi la uchongaji wa barabara.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni hiyo inayopima viwanja hivyo Gombo Samandito anasema kuwa Mradi huo ni wa aina yake hapa Nchini na kwamba hakujawahi kuwa na mradi kama ule wa kupima viwanja 18,000 kwa muda mfupi tangu nchi ipate uhuru na kwamba dhamira yao ni kuona wananchi wakiishi katika makazi bora.
Naye Diwani wa Kata hiyo Faustin Mhagama anasema mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe hivyo kwa kuwa mradi huo una manufaa kwa wananchi wake umekuwa ukipigwa sana mawe,lakini hata hivyo anasema atasimamaimara kupigania haki za wananchi wake.
Anasema kuwa kwa mradi huo wananchi wamenufaika kwa kuweza kuuza viwanja vyao kwa bei kubwa lakini pia Halmashauri imepunguziwa gharama ya kulipa fidia ambayo mara nyingi imekuwa ikichelewa kulipa au kushindwa kulipa na kuzua malalamiko na migogoro kwa wananchi.
MWISHO
No comments:
Post a Comment