About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, December 30, 2011

WABUNGE WATAKIWA KUWASAMBAZIA WAPIGA KURA WAO KATIBA YA MWAKA 1977

Na Stephano Mango,Songea
WABUNGE wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania wametakiwa kuona umuhimu wa kuwafikishia wapigakura wao Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ili waweze kuisoma na kuijadili kwa umakini kabla ya kutoa maoni yao wakati Tume itakayoundwa na Rais Jakaya Kikwete kwa lengo la kutoa maoni ya kuandika Katiba mpya itakapokuwa inapita katika maeneo yao
Wito huo umetolewa jana na wananchi kwenye mdahalo wa wazi wa mapitio na uchambuzi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Jimbo la Peramiho uliofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ufundi(Trade) wa Kanisa Katoliki la Peramiho ulioitishwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Songea(Sonngo) kwa ufadhiri wa The Foundation For  Civil Society
Akizungumza kwenye mdahalo huo Deo Mbunda alisema kuwa wananchi wengi hawaijui Katiba ya mwaka 1977 kutokana na usiri mkubwa uliowekwa na Serikali kwa kushindwa kuzisambaza kwenye maeneo mengi kutokana na sababu zilizojificha na kuwafanya wananchi washindwe kuzipata kwa urahisi
Mbunda alisema kuwa kwa kuwa Serikali toka mwaka 1977 walipoitengeneza Katiba hiyo imeshindwa kuisambaza hivyo jukumu hilo lichukuliwe na Wabunge wetu ambao tuliwachagua kwa kura nyingi waweze kutuwakilisha hivyo nao waone umuhimu wa kutuletea Katiba hiyo ili nasi tuzipate na kuweza kuzisoma kisha tuweze kutoa maoni ya kuandika Katiba mpya
“Mwaka 2010 ulifanyika uchaguzi mkuu wa Wabunge,Madiwani na Urais ambapo wagombea wote waliweza kutumia nguvu kubwa kubandika mabango yao ya kushawishi wananchi waweze kuwachagua ni vema basi nguvu ileile waliyoitumia viongozi hao kwa wale walioshinda waitumie kuwasambazia wananchi Katiba ya mwaka 1977 ili tuweze kuzisoma kwa umakini na kutoa mwanga katika Katiba ijayo”alisema Mbunda
Akizungumzia jambo hilo Mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama alisema kuwa Katiba ya mwaka 1977 zimesambaa katika maduka mengi ila kutokana na wananchi wengi hawakuwa na mahitaji ya Katiba hiyo na kwa kuwa sasa watanzania wamekuwa wakijadili uwepo wa Katiba mpya ndio maana wanajitokeza kwanza kuisaka katiba ya mwaka 1977
Mhagama alisema kuwa kila mmoja wetu ana haki ya kutoa maoni yake na kuijadili katiba iliyopo hivyo kwa Jimbo la Peramiho nitazileta Katiba hizo kwenye Ofisi ya kila Kijiji ili wananchi waweze kuisoma na kujadiliana wenyewe kwa wenyewe na kutoa maoni yao kwa amani na utulivu wakati utakapofika badala ya kuwa jambo la watu wachache
Awali akifungua mdahalo huo Mwenyekiti wa Sonngo Siwajibu Gama alisema kuwa mdahalo huo ni muhimu sana kwani unalengo la kuwajengea uwezo wananchi wa kuielewa katiba ya mwaka 1977 na kuwapa ujasiri wakati wa kutoa maoni wakati tume itakapo pita kuchukua maoni ya kuandika Katiba mpya
Gama alisema kuwa Sonngo imetoa fursa ya kutoa elimu ya uraia kwa wananchi ili waweze kuwa wazi katika mjadala wa Katiba mpya kwa kuweza kutoa maoni yao kwa mambo yatakayoleta mabadiliko chanya katika uandikaji wa Katiba mpya kwa faida ya vizazi vilivyo na vijavyo na kwamba kila mtu akielewa vizuri Katiba ya mwaka 1977 ataweza kutoa maoni yake kwa usahihi zaidi
MWISHO

No comments:

Post a Comment