About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Sunday, December 11, 2011

WATANZANIA WATAKIWA KUTUMIA BIDHAA ZINAZOTENGENEZWA NA WAHITIMU WA VETA NCHINI

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya  Nyanda za juu kusini Monica Mbelle

Na Gideon Mwakanosya,Songea

WATANZANIA wametakiwa kutumia bidhaa za ndani zinazotokana na malighafi za hapa nchini badala ya kuendelea  kutumia bidhaa za China ambazo  asilimia kubwa ubora wake ni mdogo na zimekuwa zikahiribika baada ya muda mfupi na kuiletea hasara Serikali.
 
Ushauri huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na  Mkurugenzi wa VETA Kanda ya  Nyanda za juu kusini Monica Mbelle wakati akizungumza kwenye Mahafali ya 26 ya Chuo cha Ufundi stadi Songea Mkoani Ruvuma .
 
Alisema kuwa katika miaka ya hivi karibuni Taifa limeshuhudia bidhaa nyingi zenye ubora mdogo zikitoka nje ya Nchi ukilinganisha na za hapa Nchini ambazo zimekuwa na ubora mkubwa lakini zimekuwa zikikosa soko kutokana na dhana potofu iliyojengeka miongoni mwa jamii na Serikali kwamba bidhaa bora ni zile zinazotoka ng’ambo.
 
‘Tumeshuhudia Ofisi zetu zikiwa zimejaa fenicha za kutoka nje ya Nchi ambazo baada ya mwaka mmoja zinakuwa zimeharibika na Serikali inaingia gharama nyingine kuagiza tena bidhaa hizo wakati tuna mafundi wetu wanaotengeneza bidhaa bora kuliko hizo’alisema na kuongeza kuwa
 
Inatakiwa jamii na Serikali kubadilika na kuwatumia mafundi waliohitimu VETA kwa kuwaunga mkono kwa kununua bidhaa zao zenye ubora wa hali ya juu tofauti na bidhaa za nje ambazo alidai zina ubora mdogo.
 
Alisema kwa sasa wanawatumia mafundi wao badala ya Wakandarasi kujenga Vyuo kila Wilaya ambapo wamekiteua Chuo cha Ufundi stadi Mpanda kufanya kazi hizo kwa Nyanda za juu kusini na kwa sasa wanajenga Chuo cha VETA Makete na baada ya kumaliza huko watakuja kujenga  madarasa Veta Songea baada ya wanafunzi kuwa wengi.
 
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi Songea  Gideon Ole Lairumbe alisema wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali katika Chuo hicho zikiwemo wazazi kuleta wanafunzi wa darasa la saba wenye uwezo mdogo wa kuelewa masomo na ukosefu wa vitendea kazi.
 
Hata hivyo aliishukuru Mamlaka ya Mawasiliano Nchini(TCRA) kuwapa msaada wa Kompyuta nane zenye thamani ya Tsh milioni 3.5 ambazo zilikabidhiwa siku hiyo na  Afisa wa Mamlaka hiyo Deograsias Nyoni ili ziweze kusaidia kwenye mafunzo ya Kompyuta Chuoni hapo ambapo alisema kuwa elimu ya Kompyuta na mawasiliano ni muhimu katika dunia ya leo.
MWISHO

No comments:

Post a Comment