Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu
Na Mwandishi Wetu,Songea
SERIKALI ya Mkoa wa Ruvuma imewaagiza Maafisa kilimo wa Wilaya zote Mkoani humo na Mawakala wa pembejeo kusimamia vizuri ugawaji wa vocha za pembejeo za Mkoa huo ambao umepewa mgao wa vocha 64,417.
Maagizo hayo yametolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ,Said Mwambungu wakati akifunga kikao cha pembejeo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Songea Club kilichohudhuriwa na wadau zaidi ya 500.
Aliwataka mawakala wa kugawa pembejeo kutoongozwa na maslahi ya fedha bali wanapaswa kuifanya kazi hiyo kwa moyo wa kupenda na kuwajali wananchi jambo ambalo litaondoa malalamiko na kufanya falsafa ya kilimo kwanza ifanikiwe.
Alisema kuwa katika msimu uliopita wa 2010/2011 Mkoa huo ulifanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kilimo cha mahindi na kuwapongeza wakulima kwa kuitikia falsafa ya kilimo kwanza.
‘Kwa kweli Mkoa wa Ruvuma umepiga hatua kubwa katika msimu huu na matokeo yake mnayaona ambapo tumekuwa na mahindi mengi na hadi sasa tumetumia shilingi bilioni 7 kulipa madeni na kununua mahindi na yaliyopo zinahitajika shilingi bilioni 8 kuyanunua’alisema.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa kila ambaye anaidai serikali baada ya kuuza mahindi yake atalipwa na hivyo hakuna haja kwa mwananchi kuwa na wasiwasi wa kutolipwa pesa yake hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kupeleka mahindi yao kwenye hifadhi ya Taifa ya chakula.
Mwambungu alisema agenda yake kubwa na kipaumbele chake ni maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma hususani katika suala la kilimo kwa kuwa Mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kulima zao la mahindi Nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Songea, Thomas Sabaya alisema mawakala wasumbufu katika zoezi la ugawaji wa vocha wataondolewa katika kazi hiyo na wale watakaohujumu zoezi hilo watachukuliwa hatua kisheria kama walivyochukuliwa maofisa wa Manispaa waliotuhumiwa na wizi wa vocha 459 katika msimu uliopita.
MWISHO
No comments:
Post a Comment