Watoto wakionyesha vipaji vyao wakati wa mahafari ya darasa la Saba katika Shule ya Msingi Sabasaba iliyopo mjini Songea
Na Stephano Mango,Songea
MCHANGO wa asasi zisizo za kiserikali ni mkubwa sana katika jamii na Taifa kwa ujumla hasa katika harakati za kupinga ujinga,maradhi na umasikini unaowakabili wananchi wengi
Asasi hizo zimekuwa zikitoa huduma za kijamii katika makundi ya watu mbalimbali hasa pale Serikali inapokuwa imeelemewa na mzigo wa matatizo yaliyopo katika jamii husika
Kwa msingi huo pamoja na mambo mengine ndio iliopelekea Serikali kuruhusu kuanzishwa kwa asasi hizo ili waweze kushirikiana nazo kutatua kero mbalimbali zilizopo kwenye jamii kuanzia ngazi ya mitaa,vitongoji,kata hadi Taifa
Baadhi ya asasi zimekuwa zikifanya kazi kubwa ya kulea watoto yatima,wanaoishi katika mazingira hatarishi,kuhamasisha wananchi kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi,kutunza mazingira na namna ya kupambana na umasikini kwa kuanzisha miradi midogo midogo kwa njia ya vikundi vya uzalishaji mali
Katika harakati za kutokomeza umasikini,baadhi ya asasi hizo zimekuwa zikiwajengea uwezo wananchi kwa kuwapatia mafunzo juu ya usimamizi na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na kuwapatia mitaji ya kuanzia ili waweze kujikomboa na umasikini
Mara nyingi asasi hizo ili ziweze kuendelea kuendesha shughuli zake hutegemea misaada ya kifedha kutoka kwa wahisani mbalimbali wa ndani na wa nje kwa ustawi wa jamii wanazozishughulikia
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali la Ruvuma Orphans Association (ROA) Mathew Ngalimanayo alisema kuwa shirika hilo lilinzishwa Aprili mwaka 1999 na kusajiliwa rasmi Aprili 6 mwaka 2001 na kwamba lengo kubwa la kuanzishwa kwa Shirika hilo ni kushughulikia changamoto wanazokabiliana nazo watoto yatima na watoto waishio katika mazingira hatarishi.
Ngarimanayo alisema kuwa lengo jingine ni kuvijengea uwezo vikundi mbalimbali vya wajasiriamali ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kushiriki kikamilifu katika michakato mbalimbali ya maendeleo
Ikiwa ni pamoja na kutekeleza,kufuatilia na kutathimini utekelezaji wa sera mbalimbali za maendeleo na shughuli zinazofanywa na wadau mbalimbali ikiwemo serikali katika ngazi zote za utawala na utendaji
Alisema kuwa shirika hilo pia lilianzishwa kushughulikia changamoto ziletwazo na ugonjwa hatari wa Ukimwi katika jamii kwa kushirikiana na Serikali,na wadau wengine wa maendeleo katika kufanikisha hilo katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu kwa kushirikiana na timu ya watoa huduma kwa wagonjwa majumbani limefanikiwa kuwatambua wagonjwa 516 kati ya hao wagonjwa 489 wamepatiwa huduma na wagonjwa 268 wanaendelea kupata huduma katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambapo jumla ya Tsh. 13,456 zimetumika kugharamia mahitaji ya wagonjwa hao pamoja na mafunzo ya namna ya kuishi na wagonjwa hao
“Tumefanikiwa kuwahudumia wagonjwa 489 kati ya wagonjwa 516 waliotambuliwa ambapo wagonjwa 29 wamepata nguvu na wanaendelea vizuri na shughuli zao za kila siku na wagonjwa 268 wanaendelea kuhudumiwa majumbani na pia Roa imefanikiwa kuwapatia huduma watoto yatima 234 walioko katika mfumo wa Elimu kwa kulipa karo zao,kuwapatia sare,viatu,madaftari na mikoba pamoja na huduma ya afya”.
Alifafanua kuwa kwa kipindi hicho watoto waishio kwenye mazingira hatarishi waliofikiwa na huduma ya elimu ni watoto 234 ikiwa watoto wa shule ya msingi 145,watoto wa sekondari 84,watoto wa elimu ya juu 3 na watoto wa shule za ufundi 2 ambapo jumla ya Tsh 15,630,500/= zimetumika kugharamia mahitaji ya kielimu ya watoto wao
Alieleza kuwa hakuna taasisi ama kikundi chochote cha watu kinachoweza kumaliza changamoto,kero,na matatizo yanayohusiana na Vvu/Ukimwi na watoto waishio katika mazingira hatarishi bali kwa wadau wote kuungana na kushughulikia jambo hilo kwa kushirikiana hivyo ni vema kila mdau akatimiza wajibu wake kadri ya uwezo na nafsi yake
Amezitaja changamoto wanazokutana nazo kuwa ni ukosefu wa fedha za kutosha wa kuendeshea shughuli za shirika hilo kadiri ya malengo na mipango iliyopo,mwitiko hasi wa baadhi ya wananchi na watendaji wa Serikali kuhusu dhana ya mifuko ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi
Ngarimanayo alieleza kuwa kutokana hilo Roa kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la The foundation for civil society la Jijini Dar es Saam limefanikiwa kuhamasisha wananchi wa mitaa na kata katika Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Songea kufungua na kuiendesha mifuko ya kusaidia watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwenye maeneo yao.
Alisema wamefanikiwa kuwakumbusha wananchi juu ya wajibu wao wa kimsingi wa ulinzi,matunzo na malezi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kila mtaa kuwa na kamati ya kuratibu na kusimamia masuala ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuanzisha mfuko maalumu wa kila mtaa wa kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na watu wa makundi mbalimbali katika kata hizo wamehamasishwa juu ya masuala ya Vvu/ Ukimwi na kuendesha zoezi la upimaji Vvu/Ukimwi kwa hiyari.
Alifafanua kuwa suala la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ni bomu kubwa ambalo linazinyemelea familia zetu na taifa kwa ujumla hivyo kila mwananchi anatakiwa aamke na kutambua kuwa watoto hao wanaongezeka siku hadi siku katika jamii zetu ni jukumu la wadau wote kuwahudumia kwa kuwapa mahitaji muhimu ya kibinadamu
“Kila mdau popote alipo aliangalie suala hilo na achukue hatua stahiki ya kupunguza wimbi hilo kwani kwasasa takwimu za watoto hao mkoani Ruvuma imefika jumla ya watoto 32,532 ambapo sababu zinazosababisha hali hiyo ni pamoja na mimba za utotoni,kuzaa nje ya ndoa,umasikini wa kipato katika familia,mifarakano ya wanandoa,magonjwa mbalimbali,ajali za barabarani na maafa mengine “alisema Ngarimanayo
Alisema kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii mwaka 2006 na 2008 ilifanya zoezi la utambuzi wa watoto hao katika Wilaya za Mkoa wa Ruvuma na wakaweka utaratibu ambao wananchi walipaswa kuchukua na kuhakikisha watoto hao wanasaidiwa katika jamii wanamoishi
Alieleza zaidi kuwa katika ngazi za mitaa,Kata,Wilaya viliwekwa vyombo ambavyo vinaweza kukaa na kujadili kwa kina masuala ya watoto hao na kuweka mikakati ya kumaliza tatizo hilo kwa kutumia Kamati za Ukimwi kuanzia ngazi ya mitaa hadi Wilaya kwani Kamati hizo zingekuwa zinafanya kazi yake kikamilifu tatizo la watoto hao lingekwisha
Ameitaja mipango ya shirika hilo ya baadaye kuwa ni kuendelea kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuanzisha mifuko ya jamii ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi,kugharamia gharama za masomo kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia karo,sare za shule,vifaa vya darasani na gharama zingine zinazohusiana na masuala ya elimu na kujenga uelewa kwa jamii juu ya haki na wajibu wa watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Katika hilo Serikali inatakiwa kusimamia kikamilifu mpango wa mifuko ya jamii ya kusimamia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi ili waweze kusaidiwa na jamii wanamoishi kwa kutumia kamati maalumu ya kuratibu watoto hao kuanzia ngazi ya mitaa hadi Wilaya ili kuweza kuleta ustawi na maendeleo ya watoto hao na hilo linawezekana endapo kila moja akitimiza wajibu wake
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana 0755-335051
www.stephanomango.blogspot.com
No comments:
Post a Comment