MKUU WA WILAYA YA SONGEA THOMAS OLEY SABAYA
Na Gideon Mwakanosya,Songea
NYUMBA kumi na tatu zimeezuliwa kata ya Ruvuma Manisipaa ya Songea kutokana na mvua ya mawe iliyo ambatana na upepo ambayo ilinyesha jana kuanzia majira ya saa tisa mchana hadi saa kumi .
Uchunguzi uliofanywa na mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com katika kata za Mshangano ,Bombambili ,Mfaranyaki ,Lizaboni, Ruhuwiko ,Majengo ,Subira na Ruvuma umebaini kuwa kata ya Ruvuma mtaa wa mjumbe Saidi Ndenyende ndio ulioathirika sana na mvua hizo.
Hata hivyo mitaa yote ya katikati ya mji wa Songea mvua hizo zimeangusha baadhi ya miti ya kivuli ,nguzo za umeme , nyaya za simu na zile za kuingizia picha za runinga .
Akiongea kwa uchungu Laita Swedi alisema “Umekuja upepo mkali ulioambatana na mvua ya mawe nikasikia kishindo kwuuuuuapo ndipo niliona mbingu na bati likawa limeondolewa nyumbani mwangu na kuacha vyumba vitatu vikinyeshewa mvua “Alisisitiza Laita Swedi .
Naye Stella Komba wa kata hiyohiyo ya Ruvuma ameleza kuwa yeye alikuwa anatoka hospitali ambako alikuwa amempeleka mwanaye kwa matibabu lakini alipoikaribia nyumba yake akakuta imeezuliwa na paa limetupwa mbali na nyumba yake hivyo kuacha vyumba zaidi ya vinne kuwa wazi .
Mtandao huu ulilifanya juhudi ya kumtafuta Mwenyekiti wa mtaa Said Ndenyende ili aweze kueleza iwapo amewatembelea waathirika wa mvua hizo lakini taarifa zilizo patikana nyumbani kwake alikuwa amekwenda shambani kwake eneo la Sanangula umbali wa kilometa 24 kutoka katikati ya mji wa Songea ,pia mtendaji wake hakupatikana ofisini kwake .
Mtaaramu mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema yeye ni fundi wa ujenzi kama angeweza kufanya ukandarasi wa kutengeneza nyumba hizo kila nyumba angeitengeneza kwa shilingi milioni mbili na kwamba nyumba zote kumi na tatu zingegharimu shilingi milion ishirini na sita .
Mtandao huu, bado unaendelea na uchunguzi wa uharibifu uliofanywa na mvua hizo hasa upande wa mazao ,miti ya kupandwa na mifereji ya maji,Hata hivyo jitihada za kumpata mkuu wa wilaya ya Songea Thomas Ole Sabaya ili aweze kutoa tathimini ya hasara iliyojitokeza hakuweza kupatikana kwa kuwa alikuwa kwenye shughuli maalumu za kikazi.
Mwisho.
Poleni sana.
ReplyDelete