About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, February 16, 2012

MWANASHERIA MBOGORO NA MTAZAMO MBADALA WA KAULI MBIU YA MIAKA 50 YA UHURU WA TANGANYIKA

 Mwanasheria Edson Mbogoro akifafanua jambo wakati wa mdahalo huo
 Mwanasheria Edson Mbogoro akiwa kwenye moja ya mikutano ya kuimarisha chama cha Chadema mjini Songea
Baadhi ya wananchi waliohudhulia mdahalo huo kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bombambili Jimbo Kuu la Songea hivi karibuni

Na Stephano Mango,Songea
SIAMINI kama kuna Mtanzania ambaye hajawahi kuisikia mahali popote kauli mbiu ya sherehe ya  miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika iliyokuwa inatangazwa kwa nguvu kubwa na Serikali ya kuwa Tumethubutu,tumeweza na tunazidi kusonga mbele.
Mwanasheria na Wakili wa Kujitegemea Edson Mbogoro ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) ameamua kutoa maoni yake juu ya kauli mbiu hiyo ili kuweza kuona kama inaakisi uhalisia wa mambo kwa kipindi hicho cha miaka 50 toka tupate uhuru.
Akizungumza hivi karibuni kwenye mdahalo wa kauli mbiu ya miaka 50 ya uhuru uliofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bombambili mjini hapa ,Mbogoro akiwasilisha mada kwenye mdahalo huo  alisema kuwa ukitafakari kwa umakini maneno yanayounda kauli mbiu ya miaka 50 ya uhuru na kuoanisha na uhalisia wa mambo toka tupate uhuru  utabaini kuwa kauli mbiu hiyo imetiwa chumvi.
“Maoni yangu sio msahafu yanaweza yakakosolewa au kupingwa kwa nguvu ya hoja kwani nayatoa kama mchokonozi kwa ajili ya kuibua mjadala wenye afya zaidi kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu”alisema Mbogoro.
Alisema kuwa uhuru katika ngazi ya mtu binafsi humaanisha uwezo wa kujiamulia mambo yako mwenyewe ambapo katika ngazi ya Taifa au Nchi humaanisha kujitawala,yaani kuondokana na hali ya kuwa chini ya himaya ya kigeni ambayo hushikilia na kuamua mustakabali wa kila jambo kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni nakadharika.
Uhuru humaanisha kujinasua toka kwenye minyororo ya kupuuzwa kifikra ambapo jamii huzaliwa upya na kujenga matumaini mapya ndio maana katika hotuba aliyoitoa siku ya uhuru hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliainisha maadui wakuu watatu ambao ni umaskini,ujinga na maradhi na kusema kuwa adui mkubwa kuliko wote ni umaskini.
Ninamnukuu Mwl Nyerere “…….Tukiweza kumshinda adui umaskini tutakuwa tumeweza kupata silaha itakayotuwezesha kuushinda ujinga na maradhi…namuomba kila raia wa Tanganyika aape kiapo cha kuwa adui wa umaskini, amshambulie adui huyo popote atakapoonekana”.
Mwalimu Nyerere alitutahadharisha kuwa katika kupigana vita dhidi ya maadui hao, hatuna wajomba wa kupigana badala yetu, kwamba tunaweza kupata misaada ya wafadhiri kutoka nje lakini jukumu la kujiletea maendeleo ni letu wenyewe kwanza.
Mbogoro alieleza kuwa Serikali ya uhuru ilijiwekea malengo hayo matatu, ni jambo la dhahiri kuwa tuliposherekea miaka 50 ya uhuru moja ya maswali ambayo tulipaswa kujiuliza ni kiasi gani tumeweza kuupiga vita umaskini .
Alisema kuwa wakati huo tatizo kubwa ni kwamba Mwalimu hakukabidhiwa na wakoloni nchi kama tunavyoiona leo bali alikabidhiwa makabila 120 yenye viongozi wa kimila yaani Machifu, utaifa haukuwepo ambapo kazi kubwa ni kuyaunganisha makabila hayo na kuwa taifa moja lenye umoja na mshikamano
Alifafanua kuwa Mwalimu Nyerere alifuta mfumo wa uchifu uliokuwepo akaunda Wizara ya sanaa ya taifa na vijana ili kumwezesha mtu mweusi kujitambua na kuthamini utu wake na utamaduni wake na kwa mvuto wa Mwalimu ulisaidia kuwaunganisha watanganyika ambapo mbio za mwenge zilihamasisha hisia za uzalendo na utaifa na lugha ya Kiswahili ilisaidia kuwaunganisha watanganyika.
Alieleza kuwa neno kuthubutu kwa mujibu wa kamusi ya standard Swahili/English iliyochapwa na chuo kikuu cha Oxford toleo la 1995, linamaana ya ujasiri wa kuamua na kutenda jambo gumu ambalo ni la hatari, ambalo mafanikio yake hayatabiri, kwa kukubali kupata uhuru, hakuna shaka kuwa tulithubutu kwa vile ulikuwa uamuzi mgumu unaotupelekea ambako hatuna uzoefu nako, kusikotabirika.
Alisema kuwa, mara baada ya kupata uhuru chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere Serikali iliweza kuwa na mipango mizuri na ambayo ilitekelezeka kama vile ujenzi wa viwanda vya kukoboa na kusindika mazao ya biashara kama vile, korosho, kahawa, kutengeneza nguo, viwanda vya kutengenezea zana za kilimo, viwanda vya kusindika chakula na vingine vingi.
Alieleza zaidi kuwa ujenzi wa mashirika imara ya uchukuzi na usafirishaji wa anga, nchi kavu na majini na mashirika ya ugavi na kwamba asilimia ya 90 ya watanzania walikuwa wanajua kusoma na kuandika na kwamba wakati Serikali ya awamu ya kwanza inaondoka madarakani ilikuwa imeshaweka msingi wa mapinduzi ya viwanda na teknologia ambapo kilichotakiwa ni marekebisho ya uendeshaji kwa ajili ya kuleta ufanisi zaidi.
Alisema kuwa wakati huo tulithubutu kuweka misingi mizuri ya maendeleo, swali la kujiuliza je tumeweza?, katika kujibu swali hilo viongozi wa Serikali wanatumia takwimu kuonyesha kiwango cha mafanikio kama vile idadi ya watu, upatikanaji wa maji,  afya,  miundombinu, vyuo vikuu, shule za msingi na sekondari toka wakati tunapata uhuru hadi sasa na vitu vingine.
Alisema kuwa kwa mtu wa kawaida ambaye anaheshi mu ukweli hawezi kujisifia hatua ya maendeleo tuliyoipiga kwani hailingani kabisa na umri wetu wa nusu karne kama Taifa, kwani tungeweza kufanya mara 50 zaidi ya hapa tulipo, hivyo hatujaweza bali tumeshindwa.
Alisema kuwa tunatakiwa kujilinganisha na nchi kama Malaysi, Indonesia, Singapore, Thailand, Veirtnam na nyingene ambazo tulipata nazo uhuru katika kipindi  kinachokaribiana zikiwa na hali duni kama tulivyokuwa nayo sisi wakati tunapata uhuru.
Alisema kuwa, mazuri yote ya awamu ya kwanza yameyeyushwa na awamu zilizofuata, kwani Mwalimu Nyerere aliacha viwanda 12 vya nguo vinavyofanya kazi lakini leo vimebaki vitatu ambavyo vinasuasua, aliacha mashirika ya umma 380 ambayo mengi yamebinafsishwa.
Alifafanua kuwa viwanda vya kuyeyusha chuma na kutengeneza vipuri na zana mbalimbali vya  Mang’ua na Kilimanjaro, Tanzania Scania Assembly Plan, Kibaha Mgololo kilichopo Mufindi, vimeuzwa kwa bei chee, tumerudi kwenye utegemezi hata kwenye kijiti cha kuchokonolea mabaki ya vyakula kwenye meno ni made in china.
Alieleza kuwa leo tunasubiri wafadhili hata kwa ajili ya kutujengea matundu ya vyoo vya watoto wetu mashuleni, ujinga umeongezeka kwa maana asilimia 90 ya watu wanaojua kusoma na kuandika alioiacha hayati Mwalimu Nyerere imepungua hadi kati ya asilimia 65 na 70.
Alieleza zaidi kuwa hatuna umeme wa uhakika baada ya miaka 50 ya kujitawala, ni asilimia 3 tu ya kilimo chetu ndio kinatumia trekta, asilimia 26 wanyama kazi na asilimia inayobaki bado ni jembe la mkono.
Alisema kuwa Tanzania ni nchi maskini ikiwa katikati ya utajiri kwa asilimia 18 ya maji baridi dunia yafaayo kwa kunywa na umwagiliaji yako Tanzania, nchi ya tatu barani Afrika  kwa uzalishaji  dhahabu nyingi baada ya Afrika Kusini na Ghana.
Alifafanua kuwa Tanzania ni nchi ya barani Afrika kwa kuwa na Ng’ombe wengi baada ya Ethiopia, pia inazalisha madini yenye thamani kubwa aina ya Tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee lakini ni nchi inayoongoza kwa kupokea misaada mingi barani Afrika kuliko nchi yoyote ile
Alisema kuwa ni nchi ya tatu Duniani kwa kupokea misaada mingi baada ya Afghanistan na Iraq, misaada Tanzania imeongezeka toka dola za kimarekani 39.19 mwaka 1961 hadi dola za kimarekani bilioni 2.89 mwaka 2009 lakini misaada hiyo imekuwa kama ndoo ya maji inayovuja kwani imeshindwa kutukwamua.
Alisema ukosefu wa falsafa ya kuiongoza nchi kumepelekea utafunaji wa wazi wa rasilimali za taifa kwani ufisadi umetamalaki kwenye ofisi za umma,mikataba mibovu na kuwafanya wawekezaji kuja nchini kuchuma rasilimali zetu zote na kuwaacha watanzania wakiwa maskini.
“Uongozi wa umma umekuwa dili kwa baadhi ya watu kujineemesha mchana kweupe na kuwafanya watanzania wengi kubaki maskini na kusababisha maadui watatu waliotangazwa wakati tunapata uhuru, umaskini, ujinga na maradhi kushindwa kutokomezwa”alisema Mbogoro.
Alisema kuwa katika mazingira hayo hatuna sababu ya kusema kuwa tumeweza bali tumeshindwa bila kulekebisha matatizo ya msingi yanayotukabili kama Taifa kusonga mbele ni kujidanganya na kwamba kauli mbiu sahihi ya kuadhimisha miaka 50 ya uhuru ilipaswa kuwa Tumethubutu, Tumeshindwa, Tumekwama, Tunahitaji kujikwamua.
Alimalizia kwa kusema kuwa, nimejaribu kuonyesha tulikotoka na tulipo na si zaidi kuhusu tunakokwenda kwa sababu ni kiza kinene, hivyo kama taifa tunahitaji kujitazama upya kwenye kioo cha ukweli na tukubali vile kinavyotuonyesha kisha tujadiliane vya kutosha ili tujinasue na kusonga mbele.
Mwandishi wa Makala
Anapatikana 0715-335051
www.stephanomango.blogspot.com


No comments:

Post a Comment