NA GIDEON MWAKANOSYA ,SONGEA
JESHI la polisi mkoani Ruvuma limemtia mbaroni Anna Mhenga (25) mkazi wa Bombambili katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kumtupa mtoto wake mwenye umri wa siku moja kwenye eneo la msitu wa milima ya Chandamali ambako alichimba shimo na kumfukia .
Habari zilizopatikana jana mjini Songea ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Michael Kamhanda zilisema kuwa tukio hilo lilitokea machi 24 mwaka huu majira ya saa za mchana huko katika eneo la msitu wa Chandamali uliopo katika Manispaa ya Songea.
Kamanda Kamhanda alisema inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio Anna alijifungua mtoto wa jinsia ya kike kisha aliondoka eneo la nyumbani kwake na alielekea kwenye eneo la msitu mkubwa wa miti wa Chandamali ambako aliamua kuchimba shimo na kukifukia kichanga alichotoka kujifungua .
Alifafanua kuwa inadaiwa kuwa Anna alijifungua mtoto huyo akiwa na ujauzito wa miezi 7 kisha alifikia uamuzi wa kumtupa mtoto wake kwa kumfukia jambo ambalo liliwafanya majirani wamshitukie ambapo mmoja kati yao ambaye ndiye raia mwema alitoa taarifa katika kituo kikuu cha Polisi cha Songea.
Alieleza zaidi kuwa Polisi baada ya kupata taarifa ya tukio hilo walifanikiwa kumkamata Anna ambapo katika mahojiano ya awali mtuhumiwa alikataa kuhusika na tukio hilo na baada ya upelelezi zaidi wa Polisi alikiri kuwa ni kweli alikuwa na ujauzito .
Alifafanua zaidi kuwa machi 26 mwaka huu majira ya saa za asubuhi mtuhumiwa Anna alipelekwa kwenye Hospitali ya Serikali ya mkoa Songea kupimwa ambako ilibainika kuwa mazingira yote yalionyesha kuwa mtuhumiwa alitokakujifungua .
Alieleza zaidi kuwa Polisi baadaye waliendelea kumhoji na alikubali kuwa ni kweli alijifungua mtoto wa jinsia ya kike ambaye alidai kuwa amemzika kwenye msitu mkubwa wa miti uliopo eneo la Chandamali .
Kamanda Kamhanda alibainisha zaidi kuwa inadaiwa mtuhumiwa baadaye aliwapeleka askari Polisi kwenye msitu wa Chandamali ambako aliwaonyesha mahali alipomfukia mtoto huyo ambapo walichukua jukumu la kufukua eneo hilo na kukuta maiti ya kichanga ikiwa ndani ya shimo.
Alisema kuwa maiti ya kichanga huyo baadaye ilichukuliwa na kupelekwa kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo katika hospitali ya Serikali ya mkoa Songea na Polisi bado inaendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo .
MWISHO
No comments:
Post a Comment