Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda
NA DUSTAN NDUNGURU,SONGEA.
WATU wanne wakazi wa jijini Dar es salaam wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Ruvuma kwa tuhuma za kukamatwa na nyara za serikali(meno ya tembo) zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni sita.
Akiongea na waandishi wa habari kamanda wa polisi mkoani hapa Maiko Kamuhanda alisema watu hao walikamatwa katika kijiji cha Suluti kwenye maeneo ya mashamba ya NAFCO wilayani Namtumbo aprili 15 mwaka huu majira ya saa 2.30 asubuhi.
Kamuhanda alisema watu hao walikamatwa na askari wa doria baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema wa kijiji cha Suluti.
Aliwataja majangili yaliyokamatwa kuwa ni John Andrew(30) ambaye ni dereva wa gari,Hemed Geofrey(30),Idd Manase(32) na Modesta Eliakim(25) wote wakazi wa Dar es salaam.
Kamuhanda alifafanua kuwa majangili hayo yalikamatwa yakiwa na vipande 30 vya meno ya tembo ambayo walikuwa wamepakia katika gari ambayo ilikuwa imebandikwa namba bandia DFP 7208 aina ya TOYOTA Landcruiser.
Alisema kwenye kadi ya gari hilo inaonyesha namba T.125 ATD Toyota Landcruiser mali ya Morrice Christopher Meenda na kwamba meno hayo ya tembo walikuwa wakiyapeleka Dar es salaam.
Kamanda huyo wa polisi aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na polisi kwa kutoa taarifa mbalimbali na kwamba mpango uliopo ni kwa jeshi hilo kuendelea kukabiliana na majangili hayo.
Hata hivyo alisema polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment