Mratibu wa Mradi wa TOT juu ya uchanganuzi na uchambuzi wa sera ya maendeleo ya wanawake na Jinsia Wilaya ya Songea Samwel Chiwangu akieleza neno la utangulizi wakati wa mafunzo hayo jana |
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Charles Mhagama akifungua mafunzo hayo, kulia ni Katibu wa mafunzo Mathew Ngarimanayo na kushoto ni Mwenyekiti wa mafunzo Fatuma Misango |
Washiriki wa mafunzo hayo wakiendelea kusikiliza mada mbalimbali kutoka kwa wawezeshaji |
Washiriki wakiendelea na mafunzo |
WANANCHI WATAKIWA KUHESHIMU HAKI ZA BINADAMU
Na Stephano Mango,Songea
WANANCHI wametakiwa kuheshimu haki za binadamu kwa kuzingatia kanuni,taratibu na sheria ili kila mtu aweze kuishi kwa amani na upendo katika jamii yake na nchi kwa ujumla kuliko kujichukulia sheria mkononi na kusababisha kukatisha uhai wa mwenzio
Wito huo umetolewa jana na Mratibu wa mafunzo ya uchanganuzi na uchambuzi sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia Wilaya ya Songea Samwel Chiwangu yaliyoitishwa na Asasi ya Ruwodefu ambayo yanayofanyika kwa siku tatu kwenye ukumbi wa Saccos kwa ufadhiri wa shirika la The Foundation For Civil Sociaty
Chiwangu alisema kuwa inasikitisha kusikia matukio ya ukatili wa kijinsia yakiendelea kushamiri kwa kasi kubwa mkoani Ruvuma tofauti na utamaduni uliozoeleka miongoni mwa wananchi wa jamii za mkoa huo hali ambayo inatishia ustawi wa jamii
Alisema kuwa taarifa ya vifo vya kujinyonga,kupigana,kuchinjana kutokanana na mahusiano ya kimapenzi na matatizo mengine ya kijamii vinashamiri kila siku hali ambayo inaonyesha mashaka makubwa kwa wananchi
“Wanaharakati tunapaswa tusikitike sana na taarifa hizo na tuchukue hatua kukomesha hali hiyo, kwani mtu unayempenda huwezi kumuua kwa sababu za kukunyima penzi au kumkuta mpenzi wako na mwanaume au na mwanamke mwingine hivyo kama kweli unampenda utamlinda na vishawishi vinavyoweza kupunguza upendo wake kwako na sio kumuua”alisema Chiwangu
Alisema kuwa haki ya kuishi ni haki kubwa kuliko zote na kwamba hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuondoa uhai wa mwenzake kwa sababu yoyote ile kwani mwenye uwezo na mamlaka hayo ni mwenyezi mungu pekee yake ni vema kazi yake tukamuachia
Alisema kuwa jambo hilo halipaswi kuvumiliwa hata kidogo hivyo ni vema viongozi wa dini na wakijamii pamoja na Serikali kushirikiana kikamilifu kudhibiti jambo hilo kwani kabla vifo havijatokea kunakuwepo na dalili za kutokuwa na amani miongoni mwa wapenzi hao tujaribu kusuluhisha migogoro kwa taratibu za mila na desturi na kwamba ikishindikana basi sheria itumike kudhibiti vifo hivyo
Akifungua mafunzo hayo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Charles Mhagama alisema kuwa wanawake nchini wanatakiwa kuacha uwoga wa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwenye vyombo vya habari ili kuweza kujenga mazingira ya kukomesha ukatili mbalimbali wa kijinsia uliokithili miongoni mwa jamii zinazotuzunguka
Mhagama alisema kuwa vyombo vya habari ni wadau muhimu sana katika harakati za ukombozi wa mwanamke wa kimapinduzi hasa wakati huu ambao taifa letu linaelekea kwenye miaka 50 ya uhuru ili kuweza kuzibaini changamoto mbalimbali za wanawake zilizokuwa zinawakabili wanawake miaka hiyo na sasa tuweke mikakati mingine ya kuzikabili changamoto za sasa
Awali Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Ruwodefu Hieromina Lugomi alisema kuwa mafunzo hayo yanalengo la kuwajengea uwezo wananchi kutambua fursa zilizomo ndani ya sera ya wanawake na jinsia ili waweze kunufaika nayo
Lugomi alisema kuwa watu wanaohudhuria mafunzo hayo kwa lengo la kupata elimu,kubadilishana mawazo na kuangalia maeneo muhimu yaliyopo kwenye sera hiyo na kuishawishi Serikali iyafanyie kazi maeneo hayo ni pamoja na vikundi vya wajasiriamali, viongozi wa dini, viongozi wa siasa,na vikundi vya wafanyabiashara
Alisema kuwa washiriki watapata fursa ya kujadili kwa upana haki za binadamu,madhumuni ya sera ya wanawake na jinsia, malengo ya sera, maana ya jinsia, usawa wa kijinsia,mgawanyo wa madaraka, umiliki wa rasilimali sheria ya ndoa na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia
MWISHO
No comments:
Post a Comment