MKAZI mmoja wa kijiji cha Kihuru wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma amehukumiwa na mahakama ya wilaya adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwenda jela kwa kosa la kumbaka msichana wa miaka 15.
Akisoma hukumu hiyo hakimu mkazi katika mahakama ya wilaya ya Mbinga Joakim Mwakyolo alisema kuwa mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kuwa Dickson Komba alitenda kosa hilo la ubakaji.
Mwakyolo alisema kuwa mahakama imemtia hatiani Komba na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwenda jela ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Mara baada ya kusomewa hukumu hiyo mshitakiwa alibubujikwa na machozi huku akiangua kilio mahakamani hapo na kuomba kwa sauti apunguziwe adhabu.
Awali mwendesha mashitaka wa polisi inspekta Mwamba alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa Komba alitenda kosa la kumbaka msichana huyo akiwa anaenda dukani machi 5 mwaka jana majira vya saa 3 usiku.
Aliendelea kudai kuwa pamoja na kumfanyia kitendo hicho pia alimpora simu moja aina ya Nokia yenye thamani ya shilingi 130,000 na fedha tasilimu shilingi 15,000 mali ya Essau Dukila.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment