About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, June 22, 2012

WAZEE WAIOMBA SERIKALI KUU KUISAIDIA WILAYA YA TUNDURU


Na Augustino Chindiye, Tunduru
WAZEE wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma wameiomba serikali kuu kuisaidia Wilaya yao kwa hali na mali ili iweze kupiga hatua za kimaendeleo.

Sambamba na ombi hilo wazee hao pia wamebainisha kero za ucheleweshaji wa pembejeo kwa ajili ya matumizi ya kilimo hali ambayo ilidaiwa kuwa ni miongoni mwa vikwazo vya wakazi wa wilaya hiyo kupata mavuno ya kuwatosheleza kwa chakula na biashara katika harakati za kujiongezea vipato.

Wazee hao walitoa ombi hilo wakati wakiongea na Mkuu wa Wilaya hiyo Chande Nalicho katika kikao cha kujitambulisha kwa wazee hao kilichofanyika katika ukumbi wa Boma Mjini hapa.

Ndawambe Salum, Ajulu Kalolo na Mapunda Chikambo ni miongoni mwa wazee waliotoa ombi hilo huku wakibainisha kuwa wakazi wa Wilaya hiyo ni wavivu na hawapendi kujituma na kwamba serikali isipotoa msukumo wa matumizi ya nguvu ya dola watabaki katika lindi la
umasikini wa kupindukia.

Wazee hao waliendelea kubainisha kuwa Wilaya hiyo iliyozaliwa na kutangazwa kuwa Boma mwaka 1941 sawa na Mji mkuu wa Nchi ya Kenya Nairobi imekuwa haipigi hatua za kimaendeleo kutokana na viongozi wake kuwa wapole na wasiopenda kutumia mabavu ya nguvu za dola.

Wakifafanua kero ya ucheleweshaji na ukubwa wa bei za pembejeo walisema kuwa wakulima wengi wamekuwa wakishindwa kumudu bei ya mbolea za ruzuku kutokanana kukosa kipato hali ambayo imekuwa ikiwanufaisha wajanja wachache wakiwemo watendaji wa vijiji ambao wamekuwa wakiziuza  haki za wazee hao baada ya kukosa fedha za kumudu kuchangia.

Kuhusu zao la Korosho ambalo ndio tegemeo kwa wakulima wengi wazee hao walidai kuwa hadi sasa Sulphur ya Ruzuku iliyotolewa na Serikali bado haijafika na ni kitendawili kisicho kuwa na mteguzi kutokana na kila kiongozi anaye hojiwa majibu yake huonekana kutotoa matumaini huku mikorosho yao ikiwa imefikia kuhitaji kupuliziwa.

Aidha wazee hao pia wakatumia nafasi hiyo kumuomba Mkuu wa Wilaya hiyo kuwa mkali katika usimamizi wa shughuli zote za kimaendeleo na kutoa msukumo wa kipekee katika elimu ili nao waweze kupiga hatua.

Akijibu hotuba hiyo pamoja na mambo mengine Dc, Nalicho kufuatilia kero zao akaahidi kuwa msimamizi mzuri wa maendeleo na kuiwezesha wilaya hiyo kupiga hatua za kimaendeleo.

Dc, Nalicho alimaliza kwa kuwataka wazee na wananchi wa Wilaya hiyo kutoa ushirikiano katikia utekelezaji wa miradi iliyopangwa kutekelezwa wilayani humo.
Mwisho

No comments:

Post a Comment