Wednesday, August 29, 2012
KADA WA CCM ATIMKIA CHADEMA SONGEA
Na Giden Mwakanosya, Songea
ALIYEKUWA Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mjimwema iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoa wa Ruvuma Magdalena Zuru Gama amejivua uwanachama wa chama hicho na amejiunga katika Chama cha Democrasia na Maendeleo (CHADEMA) na amedai kuwa amefanya uamuzi huo akiwa na akili timamu ambapo ameeleza kuwa ameona chama hicho kinaendelea kukosa maendeleo na baadhi ya viongozi wa mejaa ubinafsi.
Magdalena Gama alitoa kauli hiyo jana kwenye ofisi ya chadema kata ya Mjimwema wakati alipokuwa akikabidhiwa kadi mpya ya CHADEMA baada yakuomba na chama hicho kwa mwenyekiti wa CHADEMA wa tawi la Pachanne lililopo Mjimwema Swedi Milanzi ambako kulihudhuliwa na wanachama wa chama hicho.
Alisema kuwa ameamua kukihama chama cha CCM baada ya kuona baadhi ya viongozi wa CCM wamekuwa na tabia ya ubinafsi na kuonekana kuwa CCM ni ya kwao wao wenyewe na kwamba kila nafasi inayotangazwa kugombea wanafanya kila njia wagombee wao wenyewe na kuwakatisha tamaa wanachama wengine wanaotaka kugombea nafsi hizo.
Alifafanua zaidi kuwa alijiunga na uwananchama wa CCM tangu mwaka 1981 baada ya kupata mafunzo ya elimu ya siasa kwa muda wa miezi 3 hivyo alikuwa mwanachama wa muda mrefu na amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za chama hicho licha ya kuwepo mizengwe ya hapa na pale iliyokuwapo ikifanywa na baadhi ya viongozi ambao walioifanya chama cha CCM ni mali yao,hivyo ameamua kujiunga na chama cha Chadema ambacho ndio chama pekee chenye sera nzuri zenye tija kwa watanzania.
Kwa upande wake mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya chama hicho Samweli Chale alisema kuwa kitendo alichokifanya Magdalena Gama kukihama chama cha Ccm na kukimbilia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ni cha kiungwana kwani Ccm imejaa fitina hasa kwa wale Viongozi wanaoonekana kwa jamii kuwa makini.
Chale ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha Democrasia na Maendeleo (Chadema) kata ya Bombambili alisema kuwa msimamo wa Chadema ni kuboresha zaidi maendeleo mbalimbali ya wananchi na kila malengo makini ya kuhakikisha kuwa chama kinashika dola kuanzia ngazi ya uongozi wa Serikali za mitaa,vitongoji na vijiji na kwamba hakuna chama kingine chenye kipaombele ni Chadema peke.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la vijana Chadema(Bavicha) wa Kata ya Mjimwema John Mkina alieleza kuwa nguvu ya chama inazidi kuongezeka na alidai kuwa baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi wameonesha nia ya kutaka kujiunga na chama hicho hivyo Magdalena Gama ni sehemu ya wananchama wengi waliomba kutaka kujiunga na Chadema ambao wanataraijwa kukaribishwa kwa mikono miwili kujiunga na chama hicho.
MWISHO
Tuesday, August 28, 2012
ASAKWA KWA TUHUMA ZA KUFANYA FUJO NA KUCHANA RAMANI YA SENSA
Na Agustino Chindiye, Tunduru
MKAZI wa Kijiji cha Nampungu wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma aliyefahamika kwa jina la Said Mkepa anatafutwa na Polisi kwa tuhuma za kufanya fujo na kuchana Ramani iliyotakiwa kutumika na karani wa kuandikisha wananchi katika Zoezi la kuhesabu watu katika Sensa ya Watu na makazi inayoendelea nchini kote.
Msako huo umefuatia agizo lililotolewa na Mkuu wa Wiolaya hiyo Chande Nalicho kwa jeshi hilo na akaongeza kuwa kitendo hicho kilichofanywa na mwanachi huyo pamoja na makundi mengine hakiwezi kuvumiliwa.
Akifafanua taarifa hiyo alipotakiwa kuzungumzia maendeleo ya zoezi hilo katika Wilaya yake pamoja na kutaja changamoto mbalimbali zilizojitokeza siku ya kwanza Dc, Nalicho alisema kuwa mbali na kuwepo kwa changamoto hizo Wananchi wengi walijiwekeza kuhesabiwa.
Aidha katika taarifa hiyo Nalicho alibainisha kuwa awali kulikuwa na vitendo vya waandikishaji kugomea zoezi hilo kwa nia ya kushinikiza malipo yao tatizo ambalo lilitatuliwa baada ya mtandao wa Benki ya NMB tawi la Tunduru kuanza kufanya kazi na kufanya fedha zao kupatina na kulipwa usiku kucha wa kuamkia Agosti 26, mwaka huu.
Nalicho aliendelea kufafanua kwa kuyataja matukio mengine yaliyo onekana kuwa kikwazo cha kufanikisha zoezi hilo kuwa ni mgomo wa kuhesabiwa kwa wauzaji wa mnada lililotokea katika kijiji cha Ligunga na Waislam wa Taasisi ya Tabrig ambao walijifungia katika msikiti wa kijiji cha Kajima katika Kata ya Kalulu matukio ambayo alisema kuwa yanaendelea kutafutiwa ufumbuzi na kuhakikisha kuwa wanahesabiwa.
Akizungumzia suala la waumini wa madhehebu hayo Nalicho alisema kuwa tayali kuna taratibu za kuwasiliana na viongozi wa madhehebu hayo zinaendelea ili kutatu mgogoro huo ambapo waumini hao katika maelezo yao wanadai kuwa wao wamehesabiwa kupitia wake zao waliopo Jijini Dar es salaam na kwamba endapo wataendelea kugoma serikali itazuia vibali vyao vya kuendelea kueneza dini Wilayani humo pamoja na kuchukua hatua za kisheria.
Nae Mratibu wa Sensa Wilayani humo Rudrick Charles katika taarifa yake alisema kuwa kwa ujumla zoezi hilo linaendelea vizuri ukioondoa vikundi vidogo vidogo vikiwemo kikundi cha wauzaji mnada waliogomea zoezi hilo katika kijiji cha Lingunga na waislam wa Taassisi ya Tarig ambao alidai kuwa tayari ofisi yake imekwisha patiwa majina ya watu wote na kwamba utaratibu wa kuwakamata unafanyika na kuangalia hatua za kuwachukulia endapo wataendelea kugoma kuhesabiwa.
Mwisho
Monday, August 27, 2012
NAPE AGOMA KUSALIMU AMRI YA CHADEMA, ATAKA MAPAMBANO
* Agoma kuomba radhi, asema tuhuma atazithibitisha mahakamani
* Amtaka Dk. Slaa kuandaa bilioni 3 na shilingi moja
* Ni kwa kudai CCM inaingiza siala nchini.
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye amewataka Chadema kwenda mahakamani haraka badala ya kusubiri kuombwa radhi kama walivyotaka ili kusafishwa dhidi ya madai ya chama chao kupewa mabilioni ya fedha na mataifa tajiri.
Aidha amemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Wilbrod Slaa kuiomba radhi CCM la sivyo itamburuza mahakamani kudai fidia ya sh. bilioni 3 na shilingi moja, kwa kuituhumu uongo kwamba imeingiza silaha kutoka nje ya nchi tena bila kulipia ushuru.
Nape alisema hayo leo Agosti 27, 2012, kweneye mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba mjini Dar es Salaam.
"Bila shaka mmesikia jana Chadema wakinitaka niombe radhi au wananipeleka mahakamani kudai fidia ya sh. bilioni 3, kwa madai eti nimesema Chama hicho kinapata mabilioni ya fedha kutoka kwa mataifa tajiri. Mkubwa hatishiwi nyau, nawataka waende haraka mahakamani wala wasisubiri hizo siku saba", alisema Nape.
Alisema, CCM inao ushahidi wa kutosha kuhusu madai aliyotoa Nape dhidi ya Chadema na kwamba huyo tayari kutoa uthibitisho huo mahakamani badala ya kuomba radhi.
"Nadhani wakienda mahakani itapendeza zaidi maana huko ndiko pazuri kutoa uthibitisho kuhusu tuliyosema, na ninawahakikishieni tukishathibitisha na Msajili wa Vyama akaupata uthibitisho huo chama chao kinafutwa", alisema.
Kuhusu CCM kumburuza Dk. Slaa mahakamani, Nape alisema, ameshawaagiza wanasheria wa Chama, kuandaa barua ya kusudio la mashitaka hayo, na Dk. Slaa atapelekewa ili aamue kama ataomba radhi au atakuwa tayari kwenda mahakamani.
"Wakati wanakwenda mahakamani, Chadema wamwambie babu yao ajiandae kuomba radhi au kuburuzwa mahakamani kuilipa CCM fidia ya sh. bilioni 3 na shilingi moja kwa kuizushia CCM uongo kwamba inaingiza silaha nchini tena", alisema Nape.
Saturday, August 25, 2012
WASHAURIWA KUTOHARIBU SENSA WILAYANI TUNDURU
Na Steven Augustino, Tunduru
HALMASHAURI ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma imewahimiza viongozi wote kushiriki na kuwajibika katika nafasi zao ili kufanikisha zoezi la kuhesabu watu kupitia zoezi la Sensa ya watu na makazi kwa matumaini kuwa takwimu hizo zitasaidia Wilaya hiyo kugawanywa na kuwa Wilaya mbili.
Sambamba na faida hizo pia Wilaya hiyo kongwe iliyoundwa na wakoloni mwaka 1941 imetangaza kujivunia matokeo hayo kwa kuzitumia takwimu hizo katika mazoezi ya ugawaji wa Vitongoji, Vijiji,Kata Tarafa,Wilaya penngine na kilio chao cha kuomba kupatiwa mkoa wa Kusini kati (Selous) kikafanikiwa ili kuwawezesha wananchi wake kujikwamua kutoka katika lindi la umaskini uliopindukia.
Kufuatia hali hiyo kamati za Ulinzi na Usalama za Kata Wilayani humo zikaongezewa meno kwa kuzitaka kuwachukulia hatua watu wote waanao wapotosha kwa kuwajataza wananchi wasikubali kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya watu na makazi ainayotarajiwa kufanyika Agositi 26 mwaka huu huku wakihamasishwa kuijulisha jamii kuwa watakaogoma kuhesabiwa pia hawatapatiwa vitambulisho vya Taifa.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Faridu Khamis wakati akiongea na madiwani wa halmashauri hiyo katika kikao cha madiwani hao kilichofanyika katika ukumbi wa Boma mjini hapa na kuongeza kuwa watu hao wanaotumia kivuli cha uislam hawana nia nzuli nanchi yetu.
Khamisi pia aliwataka madiwani wa halmashauri hiyo kutumia nafasi zao kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wao juu ya faida za kuhesabiwa kuwa ni pamoja na kuwrzesha Serikali kupanga mipango yake kulingana na idadi yao kauanzia ngazi za vitongoji, vijiji, Kata.Tarafa, Wiaya , Mkoa na Taifa alisema endapo zoezi hilo litafanikiwa
Wilaya ya Tunduru itanufaika zaidi ya faida hizo.
Alisema pamoja na ukongwe huo Wilaya hiyo ambayo ukubwa wake ni sawa na mkoa wa Mtwara ambao kwa sasa umegawanywa na Wilaya 6 eneo lake lina kilometa za mraba zinazofanana na ukubwa hivyo anaamini kuwa endapo wananchi wote watatoa ushirikiano katika zoezi hilo sifa sitahili zitapatikana na kuifanya igawike katika maeneo madogo ya utawala na kuharakisha maendeleo yao.
Wakiongea kwa nyakati tofauti Mwenyekiti wa kamati ya sensa, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Chande Nalicho na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Ephraem Ole nguyaine mbali na kubaliki kwa kampeni ya orodha ya watakao hesabiwa kutumika wakati wa kugawa vitambulisho vya taifa waliwahimiza waandikishaji wa sense kujaza kwa makini nyalaka husika pamoja na fomu zitakazo takiwa kujaza majina ya watu watakaogomea zoezi hilo.
Mwisho
Thursday, August 23, 2012
WANANCHI WAHAMASISHWA KULIPIA GHARAMA ZA UPIMAJI WA VIWANJA
Na Stephano Mango, Songea
WANANCHI wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ambao wamepiwa ardhi yao katika Kata ya Mshangano kwa kutumia Kampuni ya Ardhi Plan wametakiwa kulipia gharama za upimaji ili wananchi wengine waweze kuonyeshwa na kuuziwa maeneo haya kwa kuyaendeleza
Wito huo umetolewa jana na Diwani wa Kata ya Mshangano Faustini Mhagama wakati akiwahutubia mamia ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kata hiyo na kuhudhuriwa na Viongozi wa Kampuni ya Ardhi Plan yenye makao makuu Jijini Dar Es Salaam
Mhagama alisema kuwa Mradi ulioibuliwa na wananchi wa Kata hiyo wa kurasimishiwa ardhi yao umekamilika ambapo jumla ya viwanja elfu 18,000 vimepiwa kwa kutumia kampuni ambavyo wananchi wanapaswa kuvilipia haraka ili viweze kugawiwa Septemba 3 mwaka huu kama makubaliano ya awali wakati wa mradi unaanza mwaka 2011 yalivyofikiwa
Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawapa fursa wananchi kuweza kuishi kwenye maeneo yaliyopimwa, pia watatumia maeneo hayo kwa kupata mkopo na kuendesha miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto
Alisema kuwa ili wananchi waweze kuonyeshwa na kupewa maeneo yao rasmi na kuonyeshwa mipaka ya maeneo yenye shughuli za kijamii wanapaswa kulipia gharama za upimaji zilizokubaliwa kwenye mikutano ya hadhara wakati wa mradi unaanza
Akisoma makubariano yaliyofikiwa wakati wa mradi unaanza mwaka 2011 kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mshangano alisema kuwa gharama za mradi huo zinatolewa na wananchi wenyewe kwa kutoa ardhi badala ya kusubiri Serikali mpaka ipate uwezo wa kifedha ambapo kwa wale wenye maeneo madogo yaani kiwanja kimoja mpaka viwili wanatozwa gharama ya fedha shilingi laki moja(100,000/=) kwa kiwanja kimoja na laki mbili(200,000) kwa viwanja viwili kama gharama za upimaji
MWISHO
Tuesday, August 21, 2012
WANANCHI WAHIMIZWA ULINZI SHIRIKISHI WA MALIASILI ZA TAIFA
Na Steven Chindiye, Tunduru
WAKAZI wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma wamehimizwa kutoa ushirikiano katika ulinzi wa maliasili za Taifa zikiwa ni juhudi za kuwafanya wananchi wote kufaidi matunda ya rasilimali zetu.
Sambamba na maagizo hayo pia wito umetolewa kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwa kujitoa kwa hali na mali katika ukamilishaji wa miradi ya ujenzi wa majengo ya ofisi za askari wa vijiji zikiwa ni juhudi za serikali na wadau wa maendeleo kujidhatiti na uzuuiaji wa vitendo vya
ujangili.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Chande Nalicho wakati akifungua mafunzo ya siku 15 kwa wanajumuiya wanaojishughulisha na uhifadhi wa maliasili kwa jamii za Jumuiya za hifadhi za Nalika na Chingoli.
Akifafanua taarifa hiyo Nalicho mbali na kupongeza juhudi za uendeshaji wa mafunzo hayo alisema kuwa kupitia mafunzo hayo serikali ina amini kuwa kila mtu atatimiza wajibu wake na kutokomeza ujangili.
Awali akizungumzia faida za mafunzo hayo Mkurugenzi wa mradi wa kuhifadhi Ushoroba mtambuka wa Selous – Niassa Kumrwa Ngomelo alisema kuwa mradi huo unaofadhiliwa kwa hisani ya Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya wananchi wa Ujerumani – KfW, unalenga kuwashirikisha wananchi katika uhifadhi wa Rasilimali za maliasili hususani Wanyamapori kwa kuunda jumuiya za uhifadhi (Wildlife Management Areas).
Alisema mafunzo hayo yanalenga kupambana na tatizo la ujangili ambao wananchi pia wamekuwa ni miongoni mwa washiriki wa vitendo hivyo na kufichiana siri kwa matukio hayo.
Wakizungumzia hali ya Ujangili Wilayani Tunduru afisa wanyama pori Peter Mtani na mshauri idara ya maliasili Wilaya ya Tunduru mradi wa Wanyamapori Selous – Niassa Elias mungaya walisema taifa lisipo chukua hatua za makusudi kudhibiti Uwindaji haramu kupitia uanzishwaji wa jumuiya hizo ubinafsishaji na uwindishaji wa kitalii hauta kuwa na faida yoyote kwa watalii na wawindaji hao hawata waakuta wanyama katika misitu hiyo.
Akiongea kwa niaba ya wanajumuiya hao, mwenyekiti wa jumuiya ya Chingoli Dauda Mohamedi alisema kuwa baada ya mafunzo hayo wajumbe hao watatekeleza majukumu yao bila uoga tofauti na awali ambapo kulikuwa na tabia za kutupiana majukumu kati ya viongozi wa Serikali na Jumuiya hizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mratibu wa mfunzo hayo Meys Mkwembe alisema kuwa katika kipindi hicho wanajumuiya hao kujifunza mbinu za kuwashirikisha wananchi kupambana na Ujangili pia watajifunza masomo ya Utawala bora,Uongozi bora kwa vikundi,Kanuni za uhifadhi,Rushwa kama kikwazo kikuu cha utawala bora na sera ya wanyamapori, ufugaji nyuki, uvuvi na sera za ardhi katika uhifadhi wa maliasili.
Mwisho
Sunday, August 19, 2012
WAILAM WATAKIWA KUSHIKA MAFUNDISHO YA DINI
Na Stephano Mango, Songea
WAISLAM nchini wametakiwa kuhakikisha kuwa wanauendeleza uadilifu na mafundisho ya dini hiyo ili kudumisha amani na usalama wa watanzania na majirani zao hapa duniani ili kuweza kujenga jamii iliyo bora kiroho na kimwili.
Maombi hayo yalikuwa ni sehemu ya Ibada ya swala ya Idd el fitr iliyofanyika katika Msikiti wa mkoa wa Ruvuma uliopo mjini Songea iliyohudhuriwa na maelfu ya waumini wa Dini hiyo wakiongozwa na mufti wa Tanzania Sheikh Issa Shaaban bin Simba na Mgeni Rasmi kitaifa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu.
Immam wa Msikiti huo, Sheikh Shaaban Mbaya katika maombi maalum ya kuliombea taifa na viongozi wake wapate afya njema na uwezo wa kuwatumikia watanzania ili wawe na amani, alisema kuwa waumini wa kiislamu hawatakiwi hata kidogo kumbagua muislam au asiye kuwa muislam katika maisha yao ya kila siku.
Alisema, mafundisho ya dini hiyo yana sisitiza upendo na amani ili kuenzi uumbaji wa mwenyezi Mungu, ambaye ni mwingi wa rehema na kwamba viumbe vyote vya ardhi, majini na hewani ameviumba yeye mwenyewe bila ubaguzi kwa manufaa ya viumbe kwakuwa vinategemeana.
Alieleza zaidi kuwa waumini hao wafuate mafunzo toka kiongozi wao, Mtume Muhammad (SAW) ambaye aliweza kuwatunza mayatima na watu wasiokuwa na uwezo kiuchumi ambao wasiowaislamu na waislamu ili wapate furaha ya maisha yao ya kila siku licha ya shida na upweke waliokuwa nao.
"Ndugu waumini haina maana wakati huu wa sikukuu mkajipamba kwa nguo safi na mkala vyakula vizuri wakati mioyo yenu na matendo yenu hayampendezi mwenyezi mungu," alisema Immam Sheikh Shaaban Mbaya na kusisitiza kuwa ni vyema wakaona umuhimu wa kuendeleza mafundisho waliyoyapata mwezi Mtukufu wa ramadhani kwa manufaa ya watu wote.
Aidha, Sheikh Mbaya alisema, Uchoyo na tamaa za mali, matendo mabaya na uroho wa madaraka na kudhalilisha wengine ndiyo chanzo cha kuvuruga amani iliyopo kuanzia ngazi ya familia, kijiji wilaya taifa na kimataifa.
Mwisho.
Thursday, August 16, 2012
KADA WA CCM RUVUMA AKUTWA CHOONI GESTI AKIWA AMEKUFA
Na Stephano Mango, Songea
MJUMBE wa Kamati ya Utendaji wa Jumuiya ya wanawake Tanzania(Uwt) Mkoani Ruvuma Amina Chimata (55) mkazi wa mjini Tunduru amefariki dunia akiwa chooni kwenye nyumba ya kulala wageni ya Tulia iliyopo karibu na kituo cha mabasi Songea
Habari zilizopatikana jana mjini hapa ambazo zimethibitishwa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (Ccm) Mkoa wa Ruvuma Verena Shumbusho zimesema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa za asubuhi wakati Chimata alipokuwa akijiandaa kwenda kuhudhuria kikao cha Kamati ya Siasa ya chama hicho mkoa
Shumbusho alifafanua kuwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Siasa mkoa walikuwa tayari wameshafika kwenye eneo la Ccm Mkoa kwa ajiri ya kuanza kikao hicho na ghafla mmoja wa wajumbe alipigiwa simu toka kwa muhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Tulia kuwa aende haraka kwenye nyumba hiyo kwani Chimata tangu alivyoingia bafuni na baadae aliingia chooni kwenda kujisaidi hajatoka kwa muda mrefu
Alifafanua zaidi kuwa baada ya mjumbe huyo kupokea taarifa hiyo aliwasiliana na viongozi wa Ccm Mkoa kisha walikwenda kwenye eneo la tukio ambako walikuta mlango wa choo hicho ukiwa umevunjwa na Chimata akiwa amelala kwenye sakafu ya choo hicho huku Polisi wakiwa tayari wameshaanza kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo ambapo mwili wa Chimata ulichukuliwa na kupelekwa kwenye Hospital ya Serikali ya Mkoa wa Songea kwa ajiri ya uchunguzi zaidi ambako ilithibitika kuwa Chimata alikuwa tayari amefariki dunia kwa ugonjwa wa shinikizo la damu na kisukari
Alisema kuwa kutokana hilo kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa na badala yake wajumbe walikutana wakiwa na huzuni ili kuweza kupanga kuusafirisha mwili wa marehemu kwa mazishi
Kwa upande wake Katibu wa Uwt mkoa wa Ruvuma Mariam Yusuph alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema kuwa Uwt Mkoa wa Ruvuma na Taifa kiujumla imepata pigo kubwa sana kutokana na kuondokewa na kiongozi huyo ambaye alikuwa ni msaada mkubwa sana kwenye jumuiya na chama kwa ujumla
Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeki alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo alidai kuwa lilitokea agosti 15 mwaka huu majira ya saa 4:30 asubuhi katika nyumba ya kulala wageni ya Tulia na uchunguzi wa awali umebainisha kuwa Chimata katika uahi wake alikuwa anasumbuliwa na magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu kwani baada ya tukio hilo kutokea alikutwa akiwa amehifadhi dawa ya magonjwa hayo kwenye mfuko wake
MWISHO
Wednesday, August 15, 2012
MADHEHEBU YA KIKRISTO WAITAKA SERIKALI KUZUIA VIBALI VYA MIHADHARA NCHINI
Na Steven Augustino, Tunduru
VIONGOZI wa madhehebu ya Dini Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma wameiomba serikali kuingilia kati na kuzuia vibali vya Mihadhara na makongamano ya kidini yanayo chochea na kukashifu imani za madhehebu mengeni zikiwa ni juhudi za kulinda amani ya nchi yetu.
Wito huo umetolewa na Ujumbe wa Viongozi wa Madhehebu ya dini za kikristo wilayani humo wakati wakiongea na Mkuu wa Wilaya hiyo Chande Nalicho katika kikao kilicho fanyika katika Ukumbi wa mapumziko ya Ikulu ndogo mjini hapa.
Wakifafanua taarifa hiyo kwa nyakati tofauti, mwenyekiti wa viongozi wa madhehebu hayo Fr. Mathias Nkhoma wa kanisa la Anglikana, fr. Bosco Chinguile wa kanisa katoliki na Mchungaji Mwanja Mangoni wa kanisa la Bibilia walisema kuwa mtindo wa serikali kuachilia vitendo vya
Mihadhara inayo kashfu madhehebu ya Dini zingine kinaweza kuhahatarisha tunu ya amani yetu.
Walisema ili kudhibiti hali hiyo inafaa sasa vyombo vya usalama kuanza kuchukua hatua za kisheria kwa watu ambao wamekuwa wakitumia majukwaa ya mihadhara, mikutano na makongamano ya kidini kuwachochea chuki waumini wa dini nyingine zikiwa ni juhudi za Serikali kulinda amani hiyo inayotishiwa kutoweka miongoni mwa wananchi wake kwa chuki za
mwamvuli wa itikadi za kidini.
Nao Mchungaji kiongozi wa kanisa la biblia Tanzania Hosea Lupondo, Rev.Stephano Milinga wa Kanisa la Pentekoste, Rev. Mussa Mandingo wa kanisa la Upendo, Rev. Helman Ponera (EAGT), Rev. Emmanuel Kanduru (TAG) na Mch.Anderson Kasembe wa CAG Church walisema kuwa kauli hiyo wameitoa kufuatia uwajibikaji mdogo wa Serikali udhaifu uliotumiwa na baadhi ya viongozi wa Dini nyingine kusambaza madukani na mitaani Kanda, CD na DVD zinazo kashfu dini nyingine hasa zinazo chokonoa Ukristo.
Walisema wanaposoma alama za nyakati wanagundua kuwepo kwa viashiria vya kuzuka kwa uvunjifu wa amani hasa pale dini nyingine inapo tumia uzembe wa usimamizi wa sheria na kuacha waumini hao kutamba na kutumia lugha za kuudhi hasa pale wanapofikia hatua za kugusa waziwazi vipengele nyeti vya imani za waumini wa kikristo kuwa hailengi kuwepo
kwa mahusiano miongoni mwao.
Katika taarifa hiyo viongozi hao walibainisha baadhi ya maneno nyeti ambayo yamekuwa yakisemwa mara kwa mara na viongozi wa Dini nyingine kuwa ni pamoja na “ Yesu ni Mwislamu, makafiri wa kwanza ni Wakristo, Ukristo umeenzishwa na Paulo, Wakristo ndio wanaoruhusu ndoa za jinsia moja, wakristo ndio freemason na mengine mengi kama kivutio kwa waumi wake, na wakapendekeza kwa kuyataka madhehebu hayo kutumia majukwaa
hayo kueneza uzuri wa Dini yao kwa kutumia Vitabu vyake ili kuwavutia waumini wake.
Viongozi wengine waliokemea uchochezi huo kwa dini za kikrsto na majina ya makanisa yao kwenye mabano ni Mch. Geofrey Japhet (Tabernacle), Rev. Madaraka Bukuku, ( Moravian) Mch. Gerod Makota (F.G.B.F) na Mch.Yotham Mtanga wa KKKT ambao pamoja na mambo mengine waliahidi kutoa ushirikiano kwa kuwahamasisha waumini wao kushiriki
kikamilifu katika mazoezi ya Sensa na utoaji wa maoni yatakayo tumika wakati wa kuandika katiba mpya.
Awali akisoma taarifa ya Viongozi hao Katibu wa Ujumbe wa Viongozi hao Fr.Dominic Mkapa alisema kuwa maamuzi hayo yalipitishwa na waumini wa Kikristo yaliyotolewa katika kongamano la pamoja la kutathimini hali ya vitendo hivyo lililofanyika katika Viwanja vya kanisa la Biblia Tanzani Agosti 10 mwaka huu na kubaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali na kutoa mapendekezo hayo kuwa ni njia bora ya kuleta ustawi na maendeleo kwa watu wote.
Akiongea katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya hiyo Chande Nalicho pamoja na kukiri kuwepo kwa vitendo hivyo aliahidi kutoa ushirikiano kwa viongozi hao na kuahidi kuzifanyia kazi kero hizo kwa kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Mwisho
Tuesday, August 14, 2012
WAANDISHI WAASWA KUIKUMBUSHA SERIKALI KUTIMIZA AHADI ZA WAZEE
Na Stephano Mango, Songea
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuona umuhimu wa kuisukuma Serikali ili iweze kutimiza ahadi yake ya kuwajali na kuwathamini wazee nchini ili waweze kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika maisha yao kutokana na uzembe wa baadhi ya watumishi wa umma
Wito huo umetolewa jana na Katibu Mkuu Mtendaji wa Mtandao wa Kinga Jamii Tanzania Iskaka Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake kuhusu kusuasua kwa ahadi mbalimbali ambazo serikali ili ahidi kuzitekeleza
Msigwa alisema kuwa waandishi wa habari wanawajibika kufuatilia na kuikumbusha Serikali juu ya matamko yake mbalimbali katika hotuba za viongozi wake, Sera ya Wazee ya mwaka 2003, Mkukuta na mengineyo kuhusu ustawi wa hali za wazee katika afya,kulipwa pensheni wazee wote, kusamehewa kulipa kodi za majengo, uwakilishi, kuzuia vitendo vya ukatili kwa wazee na uwepo wa mabaraza ya wazee
“Kwa sababu wazee kwa masikitiko makubwa tumeona kwamba nia njema ya serikali ya kuboreshwa maisha ya wazee inakwamishwa na utendaji usioridhisha wa baadhi ya watumishi wa umma katika sekta mbalimbali unaofanywa kwa makusudi” alisema Msigwa
Alifafanua kuwa ukosefu wa huduma ya uhakika ya afya ya wazee pamoja na kuwepo sera inayotoa haki ya wazee kupatiwa huduma hii bure bado haipatikani na hata pale inapotolewa bado madawa hayapatikani,pato duni miongoni mwa wazee na wategemezi wao, Ukandamizaji wa haki za wazee ikiwemo haki ya kuishi-(wazee kuuawa kwa hisia za uchawi) ukosekana kwa mfumo wa hifadhi ya jamii/Kinga ya kijamii ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wazee nchini
Alisema kuwa wazee wanapaswa kuthaminiwa utu wao kwani uzee sio ugonjwa bali ni hatua muhimu katika maisha ya mwanadamu ,kwani tunapaswa kuuona uzee ni ufahari si tu kwake yeye tu bali kwa jamii pana kwa sababu Taifa lisilo na wazee ni taifa lililokufa
Alieleza kuwa miongoni mwa wajibu wa waandishi wa habari ni kupaza sauti za wanyonge wakiwamo wazee ili zisikike kwenye majukwaa tofauti tofauti ya watoa maamuzi ili kuweza kuleta ustawi stahiki kwa wazee
MWISHO
Sunday, August 12, 2012
KADA WA CCM APANDISHWA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA UDHALILISHAJI
Na Gideon Mwakanosya,Songea
ALIYEKUWA mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) kata ya Bombambili manispaa ya Songea mkoa wa Ruvuma Alfonsi Haule(54) ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Sokoine amepandishwa kizimbani kujibu shtaka la udhalilishaji kijinsia.
Mwendesha mashitaka ambaye ni wakili wa serikali kanda ya Songea Juntwa Tulibake mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa wa Ruvuma Aziza Lutala alidai kuwa Mei mosi mwaka huu majira ya saa za usiku katika eneo la Bombambili wakati wa mkesha wa Mwenge isivyo halali Haule alimdhalilisha kijinsia kigogo mmoja wa Jumuiya ya Umoja wa wanawake Tanzania UWT ambaye jina lake limehifadhiwa(………….). Wakili Tulibake alifafanua zaidi mahakamani hapo kuwa mshitakiwa Haule alifanya tendo hilo bila ridhaa ya mlalamikaji kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa kifungu namba 138D(I) ya sheria ya kanuni ya adhabu ya sura namba 16 ya sheria.
Alisema kuwa udhalilishaji uliofanywa na mtuhumiwa anadaiwa kuwa alimvyua nguo za ndani na hijabu kwa lengo la kutaka kumfanyia kitendo cha aibu mlalamikaji .
Hata hivyo wakili Tulibake aliiomba mahakama iangalie uwezekano wa kupanga tarehe nyingine ya kutajwa shauri hilo kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Mshitakiwa Haule alikana shitaka na yupo nje kwa dhamana hadi Septemba 10 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani. Mwisho.
Friday, August 10, 2012
WASIMAMIZI NA MAKARANI WA SENSAWAONYWA
Na Steven Augustino, Tunduru
SERIKALI ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma imewaonya wasimamizi na makarani wa SENSA wanaojiona kuwa hawataweza kufanya kazi hiyo wajiondoe wenyewe haraka na kuwapisha wanaoweza kufanya kazi hiyo bila kushurutishwa ili kufanikisha zoezi hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Chande Nalicho wakati akifungua mafunzo ya wasimamizi na makarani wa Sensa ya watu na makazi iliyopangwa kufanyika Agosti 26 mwaka huu katika kumbi za Tunduru Sekondari, Nakapanya, mbesa na Ligoma Wilayani humo.
Akifafanua taarifa hiyo Nalicho alisema kuwa baada ya mafunzo hayo watatakiwa kusaini Mkataba na serikali unaoelekeza hatua atakazo chukuliwa karani au msimamizi endapo atavurunda zoezi hilo na kwamba wale wanaojiona kuwa waliteuliwa kimakosa ama waliomba nafasi hizo kwa lengo la kujinufaisha kwa fedha wajiondoe mapema ili nafasi zao ziweze kuzibwa kabla mkondo wa sheria hauja chukua nafasi yake.
“Serikali imetumia fedha nyigi katika kuhakikisha kuwa zoezi hilo linatekelezwa kwa ufanisi wa kutosha hivyo hatuwezi kuwavumilia watu wenye nia mbaya na watakao hujumu utekelezaji wake”alisema Nalicho.
Awali akitoa taarifa za mafunzo hayo mratibu wa Sensa Wilayani humo Rudrick Charles alisema kuwa kutokana na maelekezo yaliyotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) wilaya ya Tunduru iliekezwa kuteua jumla ya makarani na waandamizi 1,141 watashiriki mafunzo hayo na kusambazwa katika maeneo ya vituo 796 yaliyotengwa kwa ajili ya kuhesabia watu.
Charles aliendelea kufafanua kuwa kati ya maeneo hayo 796, maeneo 230 kati ya hayo yatumiwa na wataalamu watakao tumia dodoso refu lenye maswali 62 ambapo wadodosaji watakuwa 2 katika kila eneo, pia dodoso fupi lenye maswali yapatayo 37 litatumika katika maeneo yaliyobaki, pia kutakuwa na makarani wa akiba 35 na makarani waandamizi 80.
Akiongea kwa niaba ya wawezeshaji wa makarani hao Mwenyekiti wa timu hiyo Halima Nyenje alimuondoa mashaka Mkuu wa Wilaya huyo kuwa wakufunzi hao wamejipanga kuhakikisha kuwa Makarani hao wanaiva ili waweze kutoa huduma sahihi kwa jamii na kuifanya ihamasike kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya Wilaya na Taifa.
Wakiongea kwa uchungu baadhi ya wanachi katika kijiji cha Namasakata Walimweleza Mkuu wa Wilaya hiyo kuwepo kwa kundi la watu wanaopita na kuwahamasisha wananchi kugomea zoezi hilo na wakamuomba mkuu wa Wilaya huyo awaruhusu wawakamate na kuwafunga kamba wachochezi hao ombi ambalo liliridhiwa.
Wilaya ya Tunduru ina tarafa 7 kata 35, Vijiji 148, Majimbo mawili ya uchaguzi ya Tunduru Kusini na Tunduru kaskazini inakadiliwa kuwa na wakazi 315,051 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002 na sense ya maoteo ya mwaka 2012.
Mwisho
Thursday, August 9, 2012
DC NALICHO AAGIZA POLISI WAMKAMATE AFISA MTENDAJI
Na Augustino Chindiye, Tunduru
MKUU wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Chande Nalicho ameliagiza Jeshi la polisi kumsaka na kumkamata Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mkowela Mohamed Mkopi ili kujibu tuhuma za kuingiza Ng’ombe bila ridhaa ya wananchi wa kijiji hicho.
Agizo hilo alilitoa jana wakati akiongea na Wananchi katika maadhimisho ya Sikukuu ya wakulima Nanenane yaliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Nakapanya Wilayani humo.
Akifafanua taarifa hiyo Nalicho alisema kuwa maagizo hayo ameyatoa kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa afisa huyo aliandika kibali cha kuwaruhusu wafugaji wa kabila la Kisukuma kuingiza kundi la ng,ombe 270 mwanzoni mwa mwezi huu.
Sambamba na maagizo hayo Nalicho pia akatumia nafasi hiyo kuiagiza idara ya Mifugo Wilayani humo kufuatilia na kumpelekea takwimu za idadi ya makundi ya ng’ombe waliosambaa katika vijiji vya wilaya hiyo.
Aidha katika maagizo hayo Nalicho aliwaahidi wananchi hao kuwa baada ya kupokea takwimu hizo atafanya kikao na wataalamu kupitia miongozo na taratibu zilizo waruhusu wafugaji hao kuingia ovyo katika maeneo ya vijiji hivyo na kwamba wafugaji watakaobainika kuvamia
maeneo hayo bila idhini ya wananchi wataondolewa.
Akifafanua taarifa hiyo Nalicho alisema kuwa maelekezo hayo ameyatoa baada ya kubaini kuwa Wilaya yake hivi sasa inakabiliwa na migogoro na malalamiko mengi kutoka kwa wakulima na Wafugaji huku kila upande ukidai kuwa na haki ya kufanya shughuli zake katika maeneo husika hali inayotishia kuzuka kwa mapigano kwa makundi hayo.
Aidha Nalicho pia akatumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kukopa matrekta ili yawasaidie kuondokana na kutegemea jembe la mkono na kuboresha kilimo chao pamoja na kuwataka wananchi kujitokeza bila uoga na kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya watu na makazi na kutoa maoni yao katika zoezi la utoaji wa maoni wakati wa kuandika Katiba mpya.
Awali akisoma Risala ya maadhimisho hayo Kaimu afisa Kilimo na Mifugo Wilayani humo Hasan Simba mbali na kukiri kuwepo kwa kero hiyo aliahidi kukusanya kwa haraka takwimu hizo ili kuisaidia Wilaya kuondokana na migogoro hiyo pamoja na kuwahamisha wafugaji hao katika maeneo ya vyanzo vya maji na hifadhi za taifa wanakoripotiwa kuvamia.
Simba aliendelea kufafanua kuwa hadi sasa jumla ya wananchi 41 wa Wilaya hiyo wamejitokeza kuomba kukopa matrekta hayo ambapo kati yao 24 tayari wamekwisha katimiza taratibu zote na kulipia matrekita hayo kati ya matrekta 100 yaliyopelekwa na serikali Mkoani Ruvuma.
Nje ya viwanja vya mikutano hiyo wakulima Juma Mtukula, Joyce Mpugale na Mohamedo Swalehe wakapaza sauti zao kwa kuiomba Serikali kuandaa utaratibu madhubuti wa kuwatafutia wakulima masoko ya uhakika ya mazao yao pamoja na kupeleka pembejeo kwa wakati ili waweze kuendana na kauli mbiu ya kilimo kwanza.
Mwisho
Wednesday, August 8, 2012
WAZEE WAITAKA SERIKALI KUTUMIA BUSARA MGOGORO NA MALAWI
WAZEE nchini wameitaka Serikali kutumia busara na hekima katika kutatua mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa ulioibuliwa kwa mara nyingine tena na viongozi wa nchi ya Malawi hivi karibuni na kusababisha hofu miongoni mwa jamii ya watanzania
Wito huo umetolewa jana na Katibu Mkuu wa mtandao wa Kinga Jamii Tanzania Iskaka Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa
Msigwa alisema kuwa mgogoro huo toka umeibuliwa na nchi ya Malawi na viongozi wetu kuendelea kutoa matamko makali kuhusu jambo hilo kumeendelea kuzua hofu miongoni mwa jamii ya wazee, wanawake na watoto
“ Penye hofu na wasiwasi, hapana amani wala usalama miongoni mwa jamii kutakapopelekea ukosefu wa maendeleo hivyo ni lazima serikali ikawa makini kwa kujiimarisha kijeshi mipakani licha ya kuitaka jambo hili kumalizwa kwa busara kwani adui anayetuchokoza ana malengo na ajenda zaidi ya Ziwa Nyasa kama tunavyodhani"alisema Msigwa
Alisema kuwa Serikali inawajibika kumaliza mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo ili nchi hizo ziendelee na mahusiano yaliyokuwepo toka awali badala ya kufikiria vita ambavyo vitaleta maafa makubwa kwa wazee, wanawake na watoto kwani jambo hilo halihitaji kupimana ubavu
Alieleza kuwa inawezekana kabisa mgogoro huo ukamalizika pasipo umwagaji wa damu au upotezaji wa maisha ya watu kwa vita badala yake watumie busara kwa kuangalia ramani zilizopo kwenye taarifa mbali mbali za miaka ya enzi za ukoloni hasa zilizoko kwenye maktaba wakati Tanzania inaitwa Tanganyika; na Malawi inaitwa Nyasaland ukweli kuhusu mipaka yetu utapatikana.
MWISHO
Tuesday, August 7, 2012
NGOMA ACHAGULIWA KUWA MAKAMU MWENYEKITI WA NAMTUMBO
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Namtumbo Titus Ngoma
Na Stephano Mango, Songea
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wamemchagua Titus Ngoma kwa kura 24 kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo atakayeongoza kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia agosti mwaka huu
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Baraza la Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Stivin Nana alisema kuwa Madiwani katika halmashauri hiyo wapo 24 na wote kwa ujumla wao wamemchagua Diwani wa Kata ya Kitanda kushika nafasi hiyo
Nana alisema kuwa sheria na kanuni za mabaraza ya Madiwani zinasema wazi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri akichaguliwa ataongoza kwa kipindi cha miaka mitano, lakini nafasi ya Umakamu Mwenyekiti na Kamati mbalimbali za Madiwani zinachaguliwa kila baada ya mwaka mmoja
Alisema kuwa awali nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Diwani wa Kata ya Hanga Kassim Ntala ambaye aliongoza nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja na kwamba awamu hii hakugombea tena nafasi hiyo
Alifafanua kuwa mchakato wa kumpata Ngoma ulianza ndani ya Chama cha Mapinduzi (Ccm) Wilaya ya Namtumbo na kupelekwa Ccm mkoa wa Ruvuma na kurudishwa kwenye Wilaya kwa ajiri ya uchaguzi wa kumpata mgombea mmoja kwani wagombea walikuwa watatu ambao ni Daniel Nyambo ambaye alipata kura 4, Gidion Mpilime alipata kura 6 na Titus Ngoma alipata kura 14 ndani ya chama na kwamba ndani ya Baraza la Madiwani alichaguliwa kwa kura 24
MWISHO
Sunday, August 5, 2012
NANI ANAMWAMINI WAZIRI MKUU AU RAIS
| ||
Na Ansbert Ngurumo
|
Friday, August 3, 2012
KIKWETE AMSAFISHA CHENGE, ASEMA HAKUNA RUSHWA KWENYE KASHFA YA RADA
| ||
Rais Jakaya Kikwete Na Martin Malera
|
Wednesday, August 1, 2012
CCM YAMSHUKIA TUNDU LISU
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye
L Yadai orodha yake inalenga kupotosha tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.
L Anataka kuwaokoa wa Chadema katika sakata hilo.
L Yasema tuhuma za rushwa kwa wabunge lisigeuzwe la kisiasa
NA MWANDISHI WETU
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimelaani juhudi zinazofanywa na baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kupotosha na kuuficha ukweli juu ya tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.
Akizungumza na waandishi a habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alisema, zipo juhudi za baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kulifanya suala la tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge kuwa la kisiasa kwa malengo yao.
"Mfano mzuri wa juhudi hizi ni kitendo cha Tundu Lissu, ambaye ni mbunge wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kkambi ya upinzani Bungeni cha kutoa aliyoiita orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara na TANESCO na kwamba ndio watuhumiwa wa rushwa inayozungumziwa", Alisema Nape na kuongeza;
"Cha kushangaza orodha yake ilikuwa na wabunge wa CCM peke yake wakati wote tunajua kuwa yapo majina ya baadhi ya wabunge wa vyama vingine hasa Chadema, yanayotajwa katika orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa hii".
Nape alisema juhudi hizo za Lissu na wenzake zinalengo la kuuficha ukweli na kujaribu kuwalinda watuhumiwa wa uhalifu wanaotokana na Chadema.
"Tunamtaka Lissu na wengine wanaofanya juhudi hizo kuacha mara moja, na badala yake tuvipe nafasi vyombo vinavyohusika vichunguze na matokeo ya uchunguzi huo yatangazwe hadharani ili tuwajue wabunge waliotusaliti", alisena Nape.
Alisema CCM inalaani vitendo vya rushwa hasa vinapohusishwa na viongozi ambao wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kwamba rushwa ya namna hiyo inavuruga sana uchumi wa nchi, hivyo wanaohusika nayo haitoshi kuwaita wala rushwa tu bali ni zaidi ya wahujumu uchumi.
"Wakikithibitika ni muhimu hatua kali zichukuliwe kulikomesha kabisa hili na iwe fundisho kwa wengine", alisema Nape.
Nape alisema CCM inawapongeza watendaji wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini wakiongozwa na Waziri wao Prof. Sospeter Muhongo, Manaibu wake, Massele na Simbachawene na Katibu Mkuu, Maswi kwa uzalendo, ujasiri na umahiri wao mkubwa waliouonyesha kwa muda mfupi waliokaa kwenye wizara hiyo.
"Tunaamini uzalendo walioonyesha katika kusimamia wizara hii,utaigwa na watumishi wengine wa umma katika kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali za nchi zinalindwa ili kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania yanatimia. Tunaunga mkono jitihada zao", alisema Nape.
Alisema, pia CCM inalipongeza bunge kwa kuendelea kusimamia serikali na rasilimali za nchi katika kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa ya maendeleo.
"Tunawaomba waheshimiwa wabunge wazidi kutanguliza masilahi ya taifa mbele na uzalendo mkubwa katika shughuli zao za kila siku", alimalizia.
mwisho
L Yadai orodha yake inalenga kupotosha tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.
L Anataka kuwaokoa wa Chadema katika sakata hilo.
L Yasema tuhuma za rushwa kwa wabunge lisigeuzwe la kisiasa
NA MWANDISHI WETU
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimelaani juhudi zinazofanywa na baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kupotosha na kuuficha ukweli juu ya tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.
Akizungumza na waandishi a habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alisema, zipo juhudi za baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kulifanya suala la tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge kuwa la kisiasa kwa malengo yao.
"Mfano mzuri wa juhudi hizi ni kitendo cha Tundu Lissu, ambaye ni mbunge wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kkambi ya upinzani Bungeni cha kutoa aliyoiita orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara na TANESCO na kwamba ndio watuhumiwa wa rushwa inayozungumziwa", Alisema Nape na kuongeza;
"Cha kushangaza orodha yake ilikuwa na wabunge wa CCM peke yake wakati wote tunajua kuwa yapo majina ya baadhi ya wabunge wa vyama vingine hasa Chadema, yanayotajwa katika orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa hii".
Nape alisema juhudi hizo za Lissu na wenzake zinalengo la kuuficha ukweli na kujaribu kuwalinda watuhumiwa wa uhalifu wanaotokana na Chadema.
"Tunamtaka Lissu na wengine wanaofanya juhudi hizo kuacha mara moja, na badala yake tuvipe nafasi vyombo vinavyohusika vichunguze na matokeo ya uchunguzi huo yatangazwe hadharani ili tuwajue wabunge waliotusaliti", alisena Nape.
Alisema CCM inalaani vitendo vya rushwa hasa vinapohusishwa na viongozi ambao wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kwamba rushwa ya namna hiyo inavuruga sana uchumi wa nchi, hivyo wanaohusika nayo haitoshi kuwaita wala rushwa tu bali ni zaidi ya wahujumu uchumi.
"Wakikithibitika ni muhimu hatua kali zichukuliwe kulikomesha kabisa hili na iwe fundisho kwa wengine", alisema Nape.
Nape alisema CCM inawapongeza watendaji wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini wakiongozwa na Waziri wao Prof. Sospeter Muhongo, Manaibu wake, Massele na Simbachawene na Katibu Mkuu, Maswi kwa uzalendo, ujasiri na umahiri wao mkubwa waliouonyesha kwa muda mfupi waliokaa kwenye wizara hiyo.
"Tunaamini uzalendo walioonyesha katika kusimamia wizara hii,utaigwa na watumishi wengine wa umma katika kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali za nchi zinalindwa ili kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania yanatimia. Tunaunga mkono jitihada zao", alisema Nape.
Alisema, pia CCM inalipongeza bunge kwa kuendelea kusimamia serikali na rasilimali za nchi katika kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa ya maendeleo.
"Tunawaomba waheshimiwa wabunge wazidi kutanguliza masilahi ya taifa mbele na uzalendo mkubwa katika shughuli zao za kila siku", alimalizia.
mwisho
Subscribe to:
Posts (Atom)