About

Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, May 24, 2013

ASKOFU MTEGA ASANTE NA KWAHERI JIMBO KUU LA SONGEA

Mhashamu Askufu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea Dkt Norbert Wendelin Mtega akizungumza na Wanahabari mara baada ya KUJIUDHURU

Na, Stephano Mango, Songea

JUMATANO Mei 15, mwaka 2013 ni siku ya historia kubwa na  ilioyo dhahiri kwa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea na kwa Waamini wote wa Yesu Kristo na wote wenye mapenzi mema

Ni siku pekee ambayo haikutarajiwa na Wateule, Watakatifu na Wanakanisa pale Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea Dkt Norbert Wendelin Mtega alipoamua kuwatangazia Taifa la Mungu kustaafu ( Kujiudhuru) nafasi yake hiyo

Aliamua kuwatangazia uamuzi wake huo Viongozi mbalimbali wa Kanisa Majira ya saa saba Mchana Hanga Monasteri iliyopo Wilaya ya Namtumbo Mkoa wa Ruvuma nje kidogo ya Wilaya ya Songea, siku ya Jumatano Mei 15, 2013

“…kwa kuzingatia hali yangu ya afya , kwa kuzingatia jinsi nilivyoonja utendaji wangu unavyoonyesha dalili za kuchoka na  pengine kuzorota nikiwa katika mwaka wangu wa 28 wa Uaskofu kwa hiari yangu kabisa niliamua kumuandikia barua Baba Mtakatifu ili aniruhusu kustaafu kabla ya kufikia umri wa sheria na kanuni za kustaafu rasmi” alisema Mtega

Alisema kuwa nafurahi kwa kuwa Baba Mtakatifu leo amenijibu na kunikubalia ombi langu na dakika hii mbele yenu natua jukumu lote la Uongozi juu ya Jimbo Kuu la Songea

Kwa hiari yangu na kwa kuashiriwa na hali ya afya yangu na jinsi kazi inavyonielemea kupita uwezo wangu wa awali, nafanya hivyo kwa ajili ya ustawi wa Taifa la Mungu, na hasa Kanisa lililoko Songea kwa hiyo mimi staki niwe kikwazo na hoja ya Jimbo kuzorota katika siku za mbele

Alisema kuwa kuanzia sasa Msimamizi wa kitume wa Jimbo kuu la Songea katika kipindi ambacho ambaye ameteuliwa na Baba Mtakatifu ni Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa

Ni msimamizi kwa kuwa ataliongoza Jimbo kuu la Songea katika kipindi ambacho Baba Mtakatifu anapitia mchakato wake wa kumteua na kumtuma rasmi Askofu Mkuu mwingine wa Songea

Hakuna shaka kuwa yeye ni msimamizi kwa kuwa yeye anaendelea kuwa Askofu halali kabisa na mwenye mamlaka kamili bado juu ya Jimbo la Iringa, hivyo yeye ni wa kitume kwa sababu ameteuliwa na Baba Mtakatifu.

“Kwa hiyo tangu sasa mamlaka yote ya Uongozi wa , Usimamizi na maamuzi ninajivua kikamilifu kabisa naye Askofu Taricisius Ngalalekumtwa na achukue sasa nafasi yake kikamilifu kabisa” Alisema Dkt Mtega

Alisema kuwa kuanzia sasa saa saba mchana ya mei 15, mwaka 2013 nikiwa mbele yenu kwa moyo wa dhati kabisa na kwa upendo mkubwa kuwashukuru ninyi nyote wakiwemo Mapadre na Watawa na kwa kupitia kwenu nawaaga wale wote mnaowaongoza, waamini na wafadhiri na marafiki wote wa Jimbo kuu la Songea

Mhashamu Askofu Mkuu Dkt Norbert Wendel Mtega ni Askofu wa pili wa Jimbo Kuu la Songea ambaye alishika nafasi hiyo baada ya Askofu Mkuu Hayati Yakob Yafunani Komba

Dkt Mtega kiasili alizaliwa tarehe 17 Agosti 1945 katika Kijiji cha Kinyika, Parokia ya Lupanga , Wilaya ya Ludewa, Jimbo la Njombe, ambapo Jina la Baba yake ni Wendelin Mbwatilo Paulo Mtega

Jina la Mama yake ni Martha Msafiri Petro Mtweve na katika familia yao walizaliwa watoto kumi wakiwemo wavulana sita na wasichana wanne ambapo wavulana wawili walikufa, mmoja ni kaka yake na mmoja ni mdogo wake.

Askofu Mtega aliwapa jina moja Marehemu hao ambalo lilifahamika kwa Boniventura sababu ambazo yeye alizipenda, Yeye alikuwa ni mtoto wa nne katika familia yake hiyo yenye watoto kumi waliozaliwa pamoja naye, na yeye ni wanne katika nane walio hai.

Alibatizwa tarehe 9 Septemba 1945 na Padre Leonhard Wuesst OSB Mmisionari Mbenedikitine Mswisi, ambapo Septemba 10, mwaka 1955 akiwa darasa la Tatu, aliungama kwa mara ya kwanza na kupokea Komunyio ya Kwanza katika Kigango cha Lupanga akiwa na umri wa miaka kumi.

Tarehe 2 Octoba 1956 akiwa darasa la nne alipata Sakramenti ya Kipaimara ( LC 3034) Parokiani Madunda kwa Askofu Eberhard Spiess OSB.

Alisoma Darasa la kwanza hadi la nne katika Shule ya Msingi ya Lupanga Wilayani Ludewa tangu Mwaka 1953 hadi 1957 na kwa kuwa Shule haikuwa mbali sana na nyumbani kwake, alikuwa ni mwanafunzi wa kutwa.

Jumamosi na Jumapili alikuwa anashinda nyumbani na kuchunga mbuzi na ng’ombe za Baba yake , kazi ambayo alikuwa anaipenda sana, hata hivyo mwaka 1956 alishinda mtihani wake wa darasa la nne ingawa alilalia darasa hilo.

Elimu ya Sekondari alisoma katika Seminari ya Kigonsera na baadaye Seminari ya Likonde mwaka 1962 , ambapo alimaliza kidato cha nne Novemba, mwaka 1964 na kuchaguliwa kwenda kidato cha tano Sekondari ya Serikali ya Tosamaganga Mkoani Iringa na kumaliza kidato cha sita mwaka 1967.

Mwishoni mwa mwaka 1967 alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa katika Kambi la Kitai Wilayani Mbinga na baadae Kambi ya Mafinga na kupata namba ya kijeshi A0468 ambapo alifuzu mafunzo na kutunukiwa cheti kinachotambulika kwa Best Trainee katika Kombania yake D.

Julai 1968 alijiunga na Seminari Kuu ya Peramiho kwa ajili ya Mafunzo ya  Falsafa kwa miaka miwili ambapo alimaliza Novemba mwaka 1969 na Januari 1970 hadi Novemba 1973 aliendelea na masomo ya Teolojia hapo Seminari Kuu ya Peramiho

Alijipatia Stahashahada ( Diploma) ya Teolojia kutoka Chuo Kikuu cha Makerere- Uganda na mara baada ya kutoka huko alipata madaraja mbalimbali katika Kanisa kama vile kuwa Mkleri mwaka 1970 katika Parokia ya Madunda , ambapo mwaka aliingizwa katika huduma ya Ungojezi Mlango na Uzinguaji na baadaye Ushemasi mdogo

Mwaka 1973 alipewa Daraja la Ushemasi Seminari ya Peramiho na Novemba 1973 alipewa Daraja Takatifu la Upadre Parokiani Lupanga ambapo madaraja yote mawili alipewa na aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Njombe Raymond Mwanyika

Novemba 1973 alitolea misa Takatifu ya kwanza katika Parokia ya Lupanga, na kwamba kazi yake ya Uchungaji mara baada ya Upadrisho wake alitumwa Uaskofuni Njombe kuwa Mkurugenzi wa Caritas, Mkurugenzi wa Miito, Mwalimu wa Dini katika shule ya Sekondari ya Njombe, Mlezi wa YCS Jimbo na Paroko Msaidizi wa Pili wa Njombe

Septemba 1976 alijiunga na Chuo cha Kipapa Jijini Roma (Pontificia Universita Urbaniana), Septemba 9 mwaka huo alianza kozi ya lugha ya Kiitaliano ambapo Octoba 10, 1976 masomo ya Chuo Kikuu yalianza nay eye alichukua masomo ya Falsafa

Mwaka 1978 alijipatia Shahada ya kwanza nay a pili ya masomo ya Falsafa na kupewa Magna Cum na Januari 1981 alihitimu Shahada ya Tatu na kupewa Summa Cum Laude, baada ya kurejea Tanzania alifundisha Seminari Kuu ya Peramiho akifundisha masomo ya Falsafa , Historian a Kilatini

Novemba 28, 1985 aliteuliwa kuwa Askofu wa Tatu Jimbo la Iringa na kupewa daraja hilo la Uaskofu Januari 6, 1986 mjini Roma na Baba Mtakatifu John Paulo II, ambapo Julai 6, 1992 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea kuchukua nafasi ya Hayati Askofu Mkuu Yakobo Yafunani Komba

Tarehe 20 Septemba 1992 alisimikwa kuwa Askofu Mkuu wa Pili wa Jimbo Kuu la Songea ambapo 2013 anatimiza miaka 27 ya Uaskofu na miaka 21 ya Uaskofu Mkuu na 40 ya Upadre na 68 ya umri

Mei 19, 2013 amewaaga rasmi Waamini katika Kanisa Kuu la Kiaskofu Songea na kuongoza misa maalumu akiwa Askofu Mkuu Mstaafu na kuwataka waumini wamuombee kwani Mei 31, 2013 anaenda nje ya nchi kwa matibabu

“ Mwenyezi Mungu awabariki sana, na awaneemeshe, Niombeeni kama vile nami nitakavyokuwa nawaombeeni, Amina” Alimalizia kwa kusema Askofu Mtega

Ni dhahiri kuwa Mhashamu Askofu Mtega amejiudhuru nafasi yake hiyo kubwa ndani ya kanisa na kusababisha sintofahamu miongoni mwa Taifa la Mungu, kila mmoja katika fikra zake anawaza kilichosababisha ang’atuke

Safari yake ya kiuchungaji ni ndefu inatupasa tuielewe na kuitathimini kwa dhati ili tuweze kuliimarisha Taifa la Mungu kwani sote tu mashahidi wa safari yake hiyo kwa ubora na udhaifu wake katika misingi ya Imani, Upendo, Amani na Mshikamano miongoni mwa jamii ya Kanisa, yatosha kusema Askofu Mtega asante na kwaheri Jimbo kuu la Songea

MWISHO

                         Mwandishi wa Makala

                         Anapatikana 0715-335051

                          www.stephanomango.blogspot.com

Friday, May 17, 2013

ALIYEKUWA DEREVA WA HALMASHAURI YA NAMTUMBO AKAMATWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA KUKUTWA NA MENO YA TEMBO.

Na Gideon Mwakanosya,Songea
JESHI la polisi mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na idara ya maliasili mkoani humo wamemtia mbaroni aliyekuwa dereva wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Buruhani Mtini [48]mkazi wa Bombambili Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kukutwa na vipande nane vya meno ya Tembo yenye uzito wa jumla ya kilo 18 vyenye thamani ya shilingi milioni 48 yakiwa ndani ya sanduku wakati akiyasafirisha kwa kutumia baiskeri.

 Habari zilizopatikana jana mjini Songea ambazo zimethibitishwa na kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeki zimesema kuwa tukio hilo limetokea mei 10 mwaka huu majira ya saa 4.45 asubuhi huko katika eneo la Lwinga lililopo Namtumbo mjini karibu na kituo kikuu cha mabasi .

Alisema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio kwenye eneo la lwinga chini ya kituo kikuu cha mabasi maafisa wa idara ya maliasili kwa kushirikiana na askari polisi wa wilaya ya Namtumbo walifanikiwa kumkamata Mtini akiwa na vipande nane vya meno ya tembo yenye uzito wa kilo 18 ambayo inadaiwa inatokana na kuwawa kwa tembo wawili wenye thamani ya USA Dola 15,000 kwa kila mmoja na kufanya jumla ya tembo wote wawili USA Dola 30,000 sawa na thamani ya Tanzania Tsh 48,000,000.

 Alifafanua zaidi kuwa Mtini alikamatwa akiwa na meno ya tembo ambayo alikuwa ameyafunga ndani ya sanduku akiwa anayasafirisha kwa kutumia baiskeri kwenda kwenye kituo kikuu cha mabasi ya mjini Namtumbo ambako yalikuwa yanatarajiwa kupelekwa Songea mjini ili yaanze tena kupelekwa jijini Dare esalaam.

 Alibainisha zaida kuwa mtuhumiwa Mtini baada ya kukamatwa wakati wa kumpekua alikutwa na msumeno mdogo ambao ulikutwa umehifadhiwa ndani ya sanduku ambao unasadikiwa ndio uliyotumika kukatia meno hayo na mzani mdogo [SPRING BALANCE]ambao unadaiwa ni kwa ajili ya kupimia uzito wa meno hayo.

Kamanda Nsimeki aliongeza kuwa vilevile walipoendelea kumpekua kwenye mifuko ya nguo alizo vaa walimkuta akiwa na kitambulisho cha utumishi kinachoonyesha kuwa ni mfanyakazi wa halmashauri wa wilaya ya Namtumbo aliyeajiriwa kama dereva lakini taarifa zaidi kutoka ndani ya halmashauri ya wilaya hiyo zinadai kuwa alisha achishwa kazi siku nyingi baada ya kupata ajari ambayo ilisababisha kifo akiwa na gari la halmashauri hiyo tangu mwaka 2006.

Hata hivyo kamanda Nsimeki alisema kuwa kufuatia tukio hilo polisi kwa kushirikiana na idara ya maliasili inaendelea kufanya upelelezi wa kina na utakapo kamilika mtuhumiwa Mtini atafikishwa mahakamani kujibu shistaka linalo mkabili.
           MWISHO.
Top of Form
Bottom of Form
Top of Form
Bottom of Form
Top of Form
Bottom of Form
Top of Form
Bottom of Form

Friday, May 10, 2013

MFUMO WA KONGANO BUNIFU SULUHISHO LA MAENDELEO

Na, Mwandishi Wetu, Morogoro
MFUMO wa kongano bunifu umetajwa kama mkombozi utakaoleta maendeleo endelevu Tanzania kama utazingatiwa na wadau mbalimbali.
Meneja wa Programu ya Fanikiwa Kibiashara (BDG) ambayo inafanya kazi chini ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Sosthenes Sambua, alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati wa mafunzo ya kuwezesha kongano mbalimbali nchini kujenga ubunifu na ushindani.

Mafunzo hayo ya siku nne yanayoendelea mjini hapa yanaendeshwa na Scandnavian Institute for Competitiveness and Development (SICD) pamoja na Pan African Competitiveness Forum (PACF) kwa kushirikiana na BDG, Programu inayoendeshwa chini ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Sambua ambaye alikuwa mmoja wa wakufunzi katika mafunzo hayo, amewaambia waandishi wa habari kuwa mfumo wa kongano una nafasi kubwa ya kuleta hali bora ya maisha kwa Watanzania kwa kuwa unashirikisha nguzo tatu muhimu katika uundwaji wake ambazo ni serikali, wanataaluma au watafiti na wazalishaji katika jamii husika.

Alisema katika ushirikiano huo kongano huja na ubunifu na njia mpya za uzalishaji na kujenga ushindani si tu wa ndani bali pia nje ya nchi, hivyo kuleta maendeleo.

Akitoa mfano wa mataifa mengine alisema nchi kama Sweden, Ujerumani, Italia, Hispania, na Uholanzi zimekuwa zikitumia mfumo huu wa kongano kwa zaidi ya miaka 20 na kuwa bado wanaendelea kuwekeza katika mfumo huo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya washiriki katika mafunzo hayo walitoa shukrani kwa waandaaji wa mafunzo hayo na kuahidi kufanyia kazi ujuzi watakaopata kuimarisha kongano zao.

Tuesday, May 7, 2013

NAPE AZUNGUMZA NA WANAHABARI KAULI YA LISSU

 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI ILIYOTOLEWA NA NAPE NNAUYE

                                      Nape Nnauye
 
IJUMAA iliyopita Mei 3, 2013 Msemaji wa kambi ya Upinzani Bungeni Masuala ya katiba na Sheria Ndg. Tundu Lissu katika hotuba yake pamoja na kuzishutumu taasisi zingine, lakini pia alitoa tuhuma kadhaa dhidi ya CCM.

Tuhuma hizo zilielekezwa kwenye maeneo kadhaa hasa yahusuyo suala la mchakato wa uundwaji wa katiba mpya unaoendelea nchini na ushiriki wa makundi tofauti katika mchakato huo.

Katika kuipa uzito hoja hiyo, Lissu alitoa malalamiko mengi dhidi ya CCM kwa madai kuwa tumeteka mchakato huo kwa kujaza Makada wa CCM katika Mabaraza ya Katiba yaliyoundwa kwenye ngazi ya kata hivi karibuni.

CCM Kama ilivyo taasisi yoyote makini na wenye uzalendo  kwa nchi yao, katika mchakato wa uundwaji wa katiba mpya ina jukumu la kuwahamasisha wanachama na wasio wanachama wake kushiriki mchakato wa katiba nchini kutokana na kutambua umuhimu wake.

Tofauti ya CCM na Chadema katika hili ni,  wakati CCM tunahamasisha watu washiriki kwenye mchakato wa katiba nchini, Chadema wao wanahamasisha watu wavuruge au wasishiriki kabisa mchakato huu.

Mfano mzuri ni jitihada zao za kuziria mchakato huu kwa visingizio vya kitoto kabisa. Juhudi zao za kumtaka Prof. Baregu, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, ambaye wao Chadema walimpendekeza kwenye tume, ajitoe kwenye tume zinafahamika na wala sio SIRI.

CCM inampongeza kwa dhati Prof. Baregu kwa uzalendo na ukomavu wa kisiasa aliouonyesha kwa kuwakatalia kujitoa kwenye tume na kuweka mbele masilahi ya taifa lake. Kukataa kwa Prof. Baregu kujitoa kwenye tume kwa hoja za kitoto kabisa za Chadema ilipaswa kuwa fundisho kwa vibaraka hawa.

Ilivyo fanya CCM, kuhamasisha wanachama na watanzania kwa ujumla kushiriki mchakato huo, ndivyo taasisi nyingine pia zilivyofanya. Zikiwemo taasisi za dini ambazo zimekuwa zikihamasisha zoezi hili kupitia mikusanyiko ya Ibada, Taasisi zisizo za Kiserikali yaani NGOs kwa kufanya makongamano na makundi mengine kwa kuendesha midahalo, dhambi kwa CCM inatoka wapi?.

Ifahamike kuwa mawasiliano na mjadala juu ya zoezi la mchakato wa uundwaji wa katiba mpya nchini hayakuanza jana ndani ya CCM, bali yalianza siku nyingi kwa  Chama kuunda kamati   iliyopitia na kuja na maoni ya CCM juu ya nini kiwemo kwenye katiba mpya.

Taarifa hiyo  haikufanywa Siri. Iliwasilishwa mbele ya vikao kadhaa vya Chama na kisha kutangazwa kwa umma. Hivyo hoja kwamba mawasiliano ndani ya Chama juu ya mchakato huo wa Katiba nchini umelenga kuhujumu mchakato huo hayana maana yoyote, badala yake hoja hiyo imebeba mtazamo finyu wa wanasiasa wenye tabia za nguruwe za kula watoto wake mwenyewe pindi apatapo njaa.

Chadema ni kama nguruwe ambaye huweza kuzaa watoto wake kisha akishikwa njaa huanza kuwala watoto wake mwenyewe. Mchakato wa katiba nchini ni matunda ya viongozi wa CCM akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM Taifa, kutangaza kuanza kwa mchakato huu. Hatuwezi kuuzaa wenyewe mchakato halafu tukauhujumu wenyewe mchakato huo.

Itakumbukwa umezuka utamaduni mbaya kwa baadhi ya Wabunge wa CHADEMA kutumia Bunge kama jukwaa la kuwashambulia isivyo sawa watu ambao hawana fursa ya kuingia Bungeni kujibu mashambulizi hayo. Utamaduni huu ni wa hovyo unakiuka haki za msingi ambazo zinataka mtu anayetuhumiwa/kushutumiwa apewe fursa ya kusikilizwa. Watanzania lazima tuukatae utamaduni huu.

Hivi karibuni baadhi ya Wabunge wa CHADEMA wamefanya vitendo vya aibu vilivyowakera sana Watanzania. Hili bado limo kwenye akili na midomo ya watu na  sasa Chadema wanatafuta namna ya kuficha aibu yao(nitoke vipi) kwa kurukia hoja ya Mabaraza, kuzusha na kushutumu watu kwa uongo uliokubuhu.

Vituko vyote hivi vya Chadema vimeongezeka baada ya katibu mkuu wa CCM hivi karibuni mjini Morogoro kutoa maelezo ya kina na hoja nzito dhidi ya ukibaraka wa Chadema kwenye suala zima la mchakato wa Katiba.

Nchi nyingi hasa za Afrika zilizokumbwa na machafuko moja ya ajenda kubwa ilikuwa ni swala la katiba mpya. Sasa hapa nchini Chadema wanaona watanzania wanaendelea na mchakato bila machafuko wanakosa majibu kwa mabeberu wanaowafadhili kuchafua nchi yetu, ndio maana kila kukicha wanakuja na visa na vituko kusumbua mchakato wa katiba.

Walianza kwa kukataa matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ikiwemo kutomtambua rais. Wakatangaza hadharani nchi haitatawalika kisa wamenyimwa ridhaa na watanzania. Mchakato ulipoanza wa katiba mpya wabunge wao wakazira na kutoka nje ya bunge, baada ya muda wakarudi.

Juzi bungeni wametishia kujitoa kwenye mchakato wa katiba ifikapo tarehe 30/04/2013, leo ni tarehe 
05/05/2013
!! Wamezoea kutishia nyau, tumechoka na vitisho vya vibaraka hawa. Tunapongeza msimamo wa Tume ya mabadiliko ya Katiba kwa kupuuza hoja ya kufuta mabaraza ya katiba. Chadema wakisusa na wasuse tu.

Tunawasihi watanzania wote wapuuze utoto na ukibaraka huu wa Chadema kwani ugonjwa wao tumesha ufahamu WANAUMWA KIFAFA CHA SIASA. Kila ugonjwa huu ukipanda wanatupa mateke sana. Tuwaombee ipo siku huenda mwenyezi Mungu atawarehemu watapona.

Mwisho

Nape Moses Nnauye
Chama Cha Mapinduzi
Ideology and Publicity Secretary

Wednesday, May 1, 2013

KWENYE TAIFA LA MBUZI HAKUNA MAANDAMANO WALA WANAMAGEUZI

JUZI nimeota ndoto ambayo licha ya kutafakari sana bado sijaweza kuipatia tafsiri yake.

Baada ya kujiuliza sana nimeona niwashirikishe wapendwa wasomaji ndoto yangu hiyo na labda nitapata watu wenye vipawa wanisaidie kunieleza maana ya ndoto hii.

Ni ndoto ambayo (kama ile njozi ya Mwanakijiji) imeniacha nikiwa na huzuni tele kwa yale ambayo niliyaona. Ndoto inahusu taifa la mbuzi.

Nilijikuta nimepata nafasi – kwenye hiyo ndoto - kutembelea nchi moja ambayo wananchi wake wote ni mbuzi.

Wote walikuwa mbuzi wakifanya shughuli mbalimbali za maisha. Wakulima, wafanyakazi maofisini, wasomi, maskini na matajiri kati yao wote walikuwa mbuzi.

Walikuwa ni mbuzi wa kila rangi, jinsi, makabila na dini. Japo walikuwa na tofauti zao hizo mbalimbali kitu kimoja kilikuwa dhahiri wote walikuwa ni mbuzi. Taifa hilo la mbuzi lilitawaliwa na chui.

Mbuzi wameshika hatamu

Chui waliamua aina na namna ya maisha ya mbuzi katika taifa lile na hakukuwa na namna yoyote ambayo mbuzi waliweza kutaka kitu tofauti na kile wanachotaka chui na wao wakakipata.

Kila ambacho chui walitaka walipata hata kama kingekuwa na madhara kwa mbuzi. Chui walishika hatamu ya uongozi wa kila kitu; walitawala Ikulu, Mahakama, Majeshi, Polisi, Bunge na hata Vyombo vya Habari.

Kote huko walikuwepo mbuzi wakifanya kazi na shughuli mbalimbali, lakini waliokuwa na umiliki walikuwa ni chui.

Kulikuwa na nyimbo zikiimbwa mara kwa mara kuwa chui wameshika hatamu. Na kwa kweli walishika hatamu bila wasiwasi.

Chui hawakuwahofia mbuzi hata siku moja na hivyo waliendelea kuwatawala wapendavyo. Kwenye hilo taifa la mbuzi; ambalo nililiona kwenye ndoto.

Chui walijenga zizi zuri la mbuzi

Kwenye hili taifa la mbuzi nchi nzima ni kama zizi la mbuzi. Zizi limejengwa vizuri, mipaka yake inaeleweka na chui wakijua kuwa ni maslahi yao kwa mbuzi kuishi zizini basi wameweka vyombo mbalimbali vya ulinzi kuwalinda ndani au kuzuia wanyama wengine wasiingie.

Hii haikatazi chui kuamua kula mbuzi wao. Mipaka imewekwa kwa ajili ya kulinda maadui wa nje tu na pale ambapo maadui wa nje wanatengeneza urafiki na chui basi hawaoni tatizo kuruhusu wageni hao kula na kutafuna vitoto vya mbuzi na kubeba mali za urithi wao.

Zizi hilo la mbuzi kwa kweli lilikuwa linavutia na kwa kuangalia kwa haraka haraka makundi mengi ya mbuzi yalikuwa yanafurahia kuishi ndani ya zizi hilo.

Wenyewe walikuwa wanasema kuwa chui ameleta ‘amani, umoja na mshikamano’ na hivyo mbuzi wote ni lazima washukuru na kulinda na kuienzi amani hiyo iliyoletwa na chui.

Mbuzi waliojipendekeza kwa chui kwa hakika waliishi na kujisikia kama vile na wao ni chui wadogo au siku moja watageuka kuwa chui.

Kwa kadiri nilivyowaona walikuwepo mbuzi ambao hata walianza kujipaka rangi rangi waonekane kama chui. Ati wengine waliacha kula majani na kuanza kula nyama.

Utawala wa chui kisaikolojia kwenye zizi la mbuzi

Taifa la mbuzi ambalo nililiona ndotoni, chui waliwatawala mbuzi kifikra, waliwafanya duni kiasi kwamba hawakuwa na kitu chochote ambacho wangeweza kufanya bila ya kutaka kupata baraka kutoka kwa chui; au uongozi wa chui.

Na hakuna kitu kibaya sana katika maisha ya kiumbe kama kutawaliwa kifikra. Niliwaza katika ndoto hiyo jinsi ambavyo wanadamu wanawatawala wanyama wengine kifikra na kuwafanya wafanye vitu ambavyo kwa hulka yao hawawezi kufanya.

Wanadamu wameweza kuwamiliki mbwa, ng’ombe, farasi, punda, paka na kuku. Lakini pia wanadamu wameweza kuwamiliki tembo na kuwafundisha.

Kitu ambacho wanadamu wameweza kuwafanya ni kutawala fikra na hulka za wanyama hao kiasi cha kuwamiliki na kuwaweka kwenye utumishi wa binadamu.

Ndivyo hivyo ilivyokuwa kwa chui dhidi ya wale mbuzi. Chui waliweza na zaidi ya kuweza kuwamiliki na kuwatawala mbuzi.

Walikuwepo mbuzi wapendwa wa chui

Nikaona pia jinsi baadhi ya mbuzi kutokana na njaa na hamu ya kutaka kuonekana ni wa muhimu walivyokuwa wanajipendekeza kwa chui. Hawa walikuwa wasaliti wa mbuzi wenzao.

Walikuwa wachongezi na mipango yote ya mbuzi kutaka kujikomboa ilijulikana kwa chui. Sababu ni uwepo wa mbuzi waliokuwa wanapenda kuonekana na chui.

Baadhi ya mbuzi waliamua kabisa kujitenga na mbuzi wenzao na kutwa kucha waliimba sifa za chui.

Ooh Chui wajenga nchi

Ooh Chui ndio nambari wani

Ooh Chui bila wao haiwezekani

Ooh Chui wadumu!!

Nyimbo kama hizo zilisikika hata kwa baadhi ya watoto wa mbuzi.

Na chui hawakuwa wanyimi. Waliwatuza mbuzi wasaliti na wale walionunuliwa. Mbuzi hawa walipewa vyeo katika kambi za chui, walipewa ajira na hata wakati mwingine waliwekwa kwenye Baraza la Chui na kwa hakika na wao walijiona wamefika. Mbuzi katika himaya ya chui.

Mbuzi hawatakiwi kujitambua wanaonewa

Katika hilo taifa la mbuzi kulikuwa na sheria nyingi sana na mazoea ya kila aina. Lakini kubwa kuliko yote ilikuwa ni marufuku kwa mbuzi kulalamika kuwa wanaonewa.

Mbuzi waliaminishwa kuwa chui wanawatawala kwa ‘nia njema’ na kuwa yote ambayo chui wanafanya ni kwa ajili ya kuwanufaisha wao mbuzi.

Elimu ya mbuzi ilikuwa duni, lakini chui walisema kuwa wanajitahidi kuongeza bajeti ili kuinua kiwango cha elimu. Chui walikuwa wakifanya haraka kuonesha idadi ya mashule ilivyoongezeka chini ya utawala wao na jinsi ambayo chini ya awamu nyingine ya utawala wa chui watoto wanaoenda shule kwa mara ya kwanza ni karibu asilimia 100 japo wanaofeli ni karibu asilimia hiyo hiyo.

Mbuzi wakilalamika kuhusu barabara, chui hawacheleweli kuwaonesha barabara mbalimbali zilizojengwa au ‘kuunganisha’ sehemu mbalimbali za zizi (ili mbuzi wasiwe na tatizo la kutoka upande mmoja wa zizi kwenda upande mwingine) au kujengwa kwa ‘kiwango cha lami.’

Na kweli niliona chui wakishindana kufungua barabara mbalimbali na madaraja makubwa. Niliona kwenye ndoto hiyo baadhi ya mbuzi waandamizi wakiwasifia chui kwa kuboresha barabara.

Chui walikuwa wanakula mbuzi na mazao ya mbuzi

Kitu pekee ambacho kilikuwa ni siri iliyo wazi ni kuwa chui walikuwa wanakula mbuzi na pamoja na mbuzi walijipa uhalali wa kila ambacho mbuzi wanazalisha.

Pamoja na yote ambayo chui walikuwa wanajisifia kuwa wameyafanya kwa niaba ya mbuzi, ukweli mmoja ulikuwa wazi, chui walikuwa wanawatunza mbuzi kwa ajili ya siku za kuwala.

Na siku hiyo ikifika chui walikuwa wanajua cha kuchagua. Walikuwa wanakula vile vilivyonona; japo hawakuwa na mwiko wa kula vilivyokonda.

Mbuzi wengine waliona hili na wakajaribu kulihalalisha kuwa kama chui anawatendea mema kiasi hicho na kuwatengenezea zizi lao vizuri basi wana haki (mara moja moja) ya kula mazao waliyoyapanda.

Yote niliyaona kwenye hiyo ndoto ya taifa la mbuzi. Nikaona na mengine.

Taifa la mbuzi halina migomo, maandamano wala kupinga utawala wa chui.

Kati ya vitu vilivyonishangaza sana katika taifa hili, japo kwa kweli havikunishangaza sana kwa vile najua tabia ya chui, ni kuwa mbuzi hawakutakiwa kuandamana au kugoma.

Mbuzi wachache walipojaribu kugoma tu, wengine hawakuwa tayari kuwaunga mkono kwa sababu wakiwaunga mkono chui watakasirika na kasheshe linaweza kutokea zizini.

Katika zizi hilo la mbuzi hakukuwa na migomo; mbuzi wagome halafu ‘wakale wapi’? Hivyo mbuzi niliwaona wakiendelea kulalamika chini kwa chini, lakini hawakuwa na ujasiri wa kupinga.

Maandamano ya mbuzi yaliwahi kujaribiwa lakini chui hawakuchelewa kuwashughulikia; na waliwashughulikia kwa kuwatuma watumishi wakubwa kabisa wa chui – mbwa.

Mbwa ambao waliamini kuwa wanaleta ulinzi maridhawa wa mbuzi – kumbe wanawatumikia chui.

Hili la mbwa nitalisema kidogo baadaye. Mbuzi hawaandamani zizini kwani chui hawapendi kupingwa; hawapendi kukosolewa na kwa hakika kabisa kama kuna kitu ambacho chui hawataki kabisa kionekane zizini ni aina yoyote ya mwamko wa mabadiliko ya kifikra.

Nasikia kuna mbuzi walishawahi kuwekwa kifungoni na wengine kubambikiziwa kesi kwa sababu tu walisema neno baya (wenyewe chui waliita la kichochezi) kwa wakubwa.

Katika kuhakikisha kuwa chui wanatawala kwa raha basi mfumo mzima wa kisiasa wameudhibiti vizuri sana.

Mbwa wa watawala hawajali mbuzi

Sasa katika vitu ambavyo nilivona kwenye ndoto ya hilo taifa la mbuzi, ni kuwa mbwa wanaolishwa na kutunzwa na chui hawajali kinachowatokea mbuzi.

Ikumbukwe kuwa mbwa wote ni watumishi wa chui na chui huamua mbwa ale nini, alale wapi na apate nini kama zawadi. Na mbwa wanavyopewa sifa kwa kweli hawana huruma. Wanaweza kumnga’ata yeyote, popote na kwa lolote kwa sababu tu wanaweza.

Baadhi ya mbuzi wamejaribu mara kwa mara kuwashawishi mbwa wageuke na kujali mbuzi. Bahati mbaya sana mbwa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu utii wao uko kwa chui.

Ilitokea mara kwa mara ambapo chui mkuu alitoa zawadi mbalimbali kwa mbwa wakali zaidi na waliofanya kazi vizuri ya kuhakikisha zizi liko tulivu, lina amani.

Niliona baadhi ya mbwa wakipewa tuzo za mashada ya maua ati za utumishi uliotukuka.

Lipo Bunge la mbuzi

Kati ya mambo mengi ya ajabu niliyoyaona katika ndoto yangu ni lile Bunge la mbuzi. Katika Bunge hilo nilishangaa kuona kuwa mbuzi wanagombania kujipendekeza kwa chui.

Lilikuwa ni Bunge la ajabu kwani kuanzia spika hadi mtumishi wa Bunge hilo wote wamegawanyika au wanaunga mkono utawala wa chui au wanajaribu kutetea maslahi ya mbuzi.

Hata hivyo wanaojaribu kutetea maslahi ya mbuzi hawakuwa na nguvu zaidi ya kupiga kelele kwani mamlaka yote ya kuendesha mambo yalikuwa mikononi mwa chui.

Katika Bunge la mbuzi niligundua chui wametamalaki; lakini mbuzi nao walijitahidi kujitutumia na kuwasumbua chui. Chui ikabidi wabadili kanuni ili kuwadhibiti mbuzi.

Hata hivyo wapo mbuzi waliojitambua

Wakati usingizi ukikaribia kuniisha katika ndoto yangu nilishangaa kuona kikundi kikubwa cha mbuzi wamejikusanya chini ya jabali wakifanya mikakati ya mabadiliko ya utawala wao zizini.

Nilisogea kwa karibu na kuangalia na kutazama. Niliowadhania kuwa ni mbuzi kumbe walikuwa ni simba wanaotawaliwa na chui.

Walikuwa ni simba ambao walitawaliwa kifikra na chui kiasi cha kujisahau ukuu wao. Walikuwa ni simba ambao chui wamewalazimisha kuvaa ngozi za mbuzi.

Lakini si tu kuvaa ngozi za mbuzi, pia kufikiria kama mbuzi, kuishi kama mbuzi katika zizi la mbuzi.

Nilichoona ni taifa la simba lililogeuzwa la mbuzi likitawaliwa na chui kama taifa la mbuzi.

Siku moja mmoja wa wale simba akiwa katika Bunge la mbuzi alilalamika kidogo na kudai kuwa inawezekana vipi ‘akili ndogo (za chui) kutawala akili kubwa (za simba)?’ Chui walikasirika.

Mbuzi mmoja ambaye kwa kweli ni simba alijaribu kuunguruma kidogo na kusema: “Chui mkuu dhaifu”! Ungeona jinsi chui walivyotaharuki. Kwa mbali nilianza kuona matumaini kwamba yumkini simba wameanza kujitambua kuwa wao siyo mbuzi.

Usingizi ukanitoka bila ya kujua hitimisho la hilo taifa na kama kuna uwezekano hilo taifa lipo duniani.

Nilipokaa kitandani nikitweta huku nikinywa maji ya baridi nikakumbuka kisa nilichokisikia utotoni.

Kuliwahi kutokea kuku kujikuta ametamia mayai ya mwewe pamoja na mayai yake. Jinsi alivyopata mayai ya mwewe sikumbuki, lakini vifaranga vyote vilipototolewa yule kuku alivilea vyote vizuri kabisa na vyote vilikuwa pamoja kama ndugu.

Kwa kadiri vilivyokuwa vikikua ndivyo tofauti yao ilivyozidi kuonekana. Hata hivyo vile vifaranga vya mwewe viliishi kama vifaranga vya kuku.

Na vyenyewe vilikuwa vinatafuta vijidudu ardhini kwa kutifuatifua kama vifaranga vya kuku. Cha kushangaza japo labda si sana, ni kuwa mwewe walipopita angani kuku alikimbia na vifaranga vyake pamoja na vile vya mwewe. Vyote vilijificha.

Hadi siku moja akatokea mmbeya mmoja ambaye aliona vifaranga vya mwewe vikiishi kama kuku na kuwaogopa mwewe.

Ilifika mahali hata wakati wa kunywa maji vile vimwewe vidogo navyo viliinua jicho juu kuangalia kama kuna mwewe. Mmbeya huyo aliwaita chemba wale vifaranga wa mwewe na kuwaonesha kioo wajiangalie. Nusura wakimbie walipoona wanaangaliana na mwewe.

Ndipo wakatambua ukweli kuwa wao si kuku ni mwewe. Hawakuamini lakini wakajaribu kuruka. Ilikuwa rahisi kwao kuliko walivyotarajia na walijihisi kama minyororo fulani imeachilia. Na walipoenda juu wale ‘ndugu zao’ walianza kuwakimbia. Mwewe hageuki kuku kwa kufugwa.

Simba hata avishwe ngozi ya mbuzi hawi mbuzi. Ila kama anaamini ni mbuzi nani atamfungua?

‘Well’ ni matumaini yangu taifa la mbuzi halipo duniani!