Na Stephano Mango,Mbinga
SERIKALI kwa kushirikiana na wadau wa zao la kahawa Wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma imechangisha jumla ya shilingi milioni 215 kwa ajili ya kununulia madawa yatakayotumika kupambana na wadudu waharibifu wa zao hilo .
Katibu tawala wa wilaya hiyo Idd Mponda alisema fedha hizo zimetumika kununulia madawa aina ya SUBA ambayo hutumika kuulia wadudu aina ya vidung’ata ambao wamekuwa wakishambulia miti ya kahawa.
Alisema kuwa jumla ya hekta 48 ya zao hilo zimeshambuliwa na wadudu hao na kusababisha uzalishaji wa kahawa kushuka.
Mponda alisema kufuatia jitihada zilizofanyika kuanzia Julai mwaka jana hadi sasa za kutokomeza wadudu hao mashamba mengi yameonekana kwenda vizuri na kwamba katika msimu wa mwaka 20011/12 uzalishaji unatarajia kuongezeka hadi kufikia tani 9,000.
"Kinachotakiwa kwa wakulima ni kuhakikisha wanazingatia yale wanayoelekezwa na wataalamu wa kilimo na kwamba wajiunge pamoja na kuanzisha mashamba darasa ili iwe rahisi kwa maofisa ugani kuwafikia", alisema Mponda.
Kuhusu wanunuzi wa zao hilo alisema wanapaswa kuzingatia masharti yaliyowekwa na uongozi wa wilaya hiyo na kwamba kwa wale ambao watabainika kutorosha kahawa kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kunyang’anywa leseni ya biashara hiyo.
Pia alisema wakati umefika kwa wakulima wa zao hilo kuwa makini na wafanyabiashara wajanja wanaozunguka vijijini kununua zao hilo kwani baadhi yao wamekuwa wakiwarubuni wakulima kuwa bei ya kahawa imeshuka kwenye soko la dunia ili wanunue zao hilo kwa bei ya chini jambo ambalo sio sahihi.
No comments:
Post a Comment