Na Stephano Mango,Songea
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linawashikilia watu 11 ambao ni raia wa nchi za Bangradeshi na Pakstani ambao wanadaiwa kuwa wamefukuzwa toka Msumbiji kwa kupigwa mijeredi na kunyang’anywa fedha pamoja na mali walizokuwa nazo na askari wa nchi hiyo.
Akizungumza na mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amesema kuwa raia hao wa Pakstani na Bangladeshi wamekamatwa jana majira ya saa za asubuhi huko katika kijiji cha Magwamila kilichopo mpakani mwa Msumbiji na Tanzania.
Kamuhanda amewataja waliokamatwa ambao ni raia wa Bangladeshi kuwa ni Shahed Alzam (29), Amar Ahmed (25),Gavan Halifa (40),Mhamed Parvas (23),shojal Meya (28) na Sohal Meya (28), Raia toka Pakstani waliokamatwa amewataja kuwa ni Hassan Bilar (20),Fawad Yasin (20),Mohamed Awadh (20),Aftal Hussein (24) na Hasad Ashar (45).
Amefafanua kuwa watu hao baada ya kukamatwa na kuhojiwa na polisi kwa kushirikiana na Idara ya uhamiaji Mkoani humo wamedai kuwa katikati ya mwezi uliopita waliondoka Pakstan wote kwa pamoja na walisafiri kwa ndege hadi Jijini Dar es Salaam ambako walitafuta usafiri wa basi hadi Mtwara mjini.
Ameeleza zaidi kuwa raia hao wa Nchi za Pakstani na Bangladeshi wakiwa Mtwara mjini walifanikiwa kupata usafiri kwa kutumia magari hadi Msumbiji lakini lengo lao kubwa ni kuelekea Afrika Kusini kutafuta maisha ambako wamedai kuwa waliambiwa na wenzao ambao wako Afrika kusini kuwa huko maisha ni mazuri.
Amebainisha zaidi kuwa watu hao wakiwa Msumbiji huku wakiwa wanatafuta namna ya kufika Afrika kusini walikamatwa na askari wa Msumbiji kisha walipelekwa mpakani mwa nchi hiyo na Tanzania huku wakiwa wanapigwa mijeredi na baadae wakawatelekeza kwenye Kijiji cha Magwamila ambako walikutwa wakiwa hawana kitu chochote.
Amesema kuwa raia hao wa Bangladeshi na Pakstani kwasasa wameondolewa Magwamila wapo katika Kituo kikuu cha Polisi cha Songea wakati wanafanya utaratibu wa kuwasiliana na idara ya uhamiaji ili iangalie ni namna gani wahamiaji hao haramu watawachukulia hatua .
MWISHO
No comments:
Post a Comment