Na Augustino Chindiye,Tunduru
WAGANGA na wauguzi wa Wilaya ya Tunduru wameonywa kuacha tabia za ubabaishaji wakati wa utekelezaji wa majukumu na shughuli zao za kila siku na kwamba Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo hata husika katika utetezi wa mtumishi yeyote pindi sheria itakapotakiwa kufuata mkondo wake.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Alex kazula wakati akijibu swali juu ya kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya utendaji mbovu dhidi ya wataalamu wa idara hiyo huku kukiwa na taarifa za mgomo baridi kutoka kwa Madaktari,Maafisa Tabibu na Wauguzi wa Wilaya hiyo huku ofisi yake ikidai kuto kuwa na taarifa zozote juu ya kinacholalamikiwa na wataalamu hao.
Katika taarifa hiyo Dkt. Kazula alikiri kuwa hivi sasa Hospitali yake imegubikwa na wimbi kubwa la malalamiko mbalimbali kutoka kwa wagonjwa na watu wanaokwenda kuuguza wagonjwa katika Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati kuwa wataalamu wake hawawajibiki ipasavyo wanapokea fedha kutoka kwa wagonjwa na wamekuwa na majibu mabaya na wakati mwingine wamekuwa wakiwatukana wateja wao.
Dkt. Kazula aliendelea kueleza kuwa malalamiko mengine aliyoyapokea ni pamoja na kushamiri kwa matukio ya VIFO visivyo vya lazima ambavyo hutokea kwa wagonjwa wanaoenda kutibiwa na kulazwa katika Hospitalini hali ambayo imekuwa ikizusha manung`uniko kutoka kwa wananchi kuwa Wataalamu hao wamekuwa hawajitumi katika kutekeleza wajibu wao wa kutoa tiba sahihi na kuokoa maisha ya wateja wao.
Alisema sambamba na malalamiko hayo pia ofisi yake inazo taarifa za malalamiko ya Waganga na Wauguzi hao kutoa huduma kwa upendeleo ambapo wagonjwa wasio na uwezo kifedha hawapatiwi huduma kabisa na kwamba ukiona Daktari au Muuguzi anahangaikia mgonjwa kwa nguvu zote ujue amepokea chochote (RUSHWA) kutoka kwa mgonjwa huyo.
Kufuatia hali hiyo Dkt. Kazula amesema milango ipo wazi kwa wagonjwa na wauguzaji kwenda kutoa malalamiko na ushahidi dhidi ya watumishi hao ili atayebainika sheria ifuate mkondo wake ikiwa ni pamoja na mhusika kufukuzwa kazi.
Wakati hayo yakiendelea baadhi ya wagonjwa na wauguzaji wa wagonjwa wanaolazwa katika hospitali ya Wilaya hiyo nao waliibua malalamiko ya kuwepo kwa hali mbaya na harufu kali katika vyoo vilivyopo Hospitalini hapo.
Walisema kufuati hali hiyo wamekuwa wakilazimika kutoka nje hasa nyakati za usiku ili kupata hifadhi katika mapori yaliyopo eneo la uwanja wa Ndege uliofungwa baada ya kupoteza siza za kutua ndege.
Mwisho
No comments:
Post a Comment