Na Mwandishi Wetu,Songea.
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linawasaka majambazi wawili ambao walivamia gari lililokuwa limebeba abiria 14 kutoka Mbamba bay kwenda Mbinga na kufyatua risasi tano ambazo ziliwajeruhi watu wawili akiwemo mtoto wa umri wa mwaka mmoja na nusu ambaye alikuwa amepigwa risasi kwenye mguu wa kushoto akiwa amebebwa na mama yake mzazi kisha majambazi hao walifanikiwa kuwapora abiria fedha Shilingi 930,000 na baadaye walikimbia na kutokomea kusikojulikana.
Akizungumza na mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com Ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amesema kuwa tukio hilo lilitokea Octoba 3 mwaka huu majira ya saa 1.30 asubuhi huko katika Kijiji cha Ng’ombo kilichopo katika Kata ya Kilosa Wilaya ya Nyasa .
Kamuhanda amesema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio Dereva wa gari lenye namba za usajili T 554 ASE Toyota Hilux Joseph Hamza (35) akiwa anaendesha gari hilo lililokuwa na abiria 14 waliokuwa wanatoka Mbamba bay kuelekea Mbinga Mjini akiwa katikati ya daraja ghafla aliwaona watu wawili wakiwa wamefunga vitambaa usoni huku wakiwa na Bunduki mbili ambao walilivamia gari hilo kisha walianza kufyatua risasi hewani ambazo ziliwajeruhi abiria wawili .
Amefafanua kuwa watu hao wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi ambao walikuwa na siraha za SMG na SAR waliwapiga risasi Rehema Haule (11) ambaye alijeruhiwa vibaya kwenye mguu wa kushoto wakati akiwa amebebwa na mama yake mzazi na Castory Kinunda (31) Mkazi wa Mbamba bay alijeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi na majambazi hao kwenye mkono wa kushoto .
Amebainisha zaidi kuwa majambazi hao baada ya kufyatua risasi hewani walianza kuwapekua abiria mmoja hadi mwingine ambapo baadae walifanikiwa kuwapora abiria hao shilingi 930,000 na baada ya kuwanyang’anya fedha hizo walikimbia na kutokomea porini .
Alieleza zaidi kuwa majeruhi Rehema baada ya kupigwa risasi kwenye mguu wa kushoto alikimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya Liuli ambako alifariki dunia muda mfupi wakati akiendelea kupata matibabu na majeruhi Kinunda kwasasa hivi amelazwa katika hospitali ya Serikali ya Mbinga akiendelea kupata matibabu na hali yake bado ni mbaya.
Kamanda Kamuhanda amesema kuwa Polisi baada ya kupata taarifa ya tukio hilo walienda kwenye eneo la tukio na kuwakuta baadhi ya abiria ambao walielezea tukio hilo lilivyotokea na kwamba upelelezi wa awali umefanyika ambao umebaini kuwa majambazi hao wametokea Kyela Mkoani Mbeya kwa kupitia Ziwa Nyasa.
MWISHO
No comments:
Post a Comment