Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Shule ya Tanga Expedito Luambano(aliyesimama)
Na Mwandishi Wetu ,Songea
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoani Ruvuma inamshikilia Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Shule ya Tanga iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 20,000 kutoka kwa mwananchi ambaye jina lake limehifadhiwa wa Kata hiyo ambaye alikwenda Ofisini kwake kuomba asaidiwe kulipwa deni toka kwa Mfanyabiashara mmoja ambaye naye jina lake limehifadhiwa.
Akizungumza na mtandao huu wa www.stephanomango.com Ofisini kwake Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoani Ruvuma Daudi Masiko amesema tukio hilo limetokea Octoba 2 mwaka huu majira ya saa za mchana huko kwenye eneo la nane nane Msamala Songea Mjini.
Masiko amemtaja anayeshikiliwa na Takukuru kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi elfu 20,000 Expedito Luambano (36) ambaye ni Kaimu Afisa Mtendaji wa Shule ya Tanga ambapo amebainisha zaidi kuwa siku chache zilizopita Luambano akiwa Ofisini kwake alifikiwa na mwananchi mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa ambaye alikuwa anataka asaidiwe na Ofisi hiyo ili Mfanyabiashara anayemdai aweze kumlipa deni ambalo ni la muda mrefu.
Amefafanua zaidi kuwa mwananchi huyo akiwa kwenye Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata hiyo alishawishiwa na Luambano kuwa atafute shilingi elfu 20,000 ili aweze kumsaidia kumsaka Mfanyabiashara huyo anayemdai aweze kulipwa deni .
Ameeleza kuwa mwananchi huyo alikubaliana na maelezo aliyopewa na Luambano kisha alitoka kwenye Ofisi hiyo kwa makubaliano kuwa wangekutana kwenye eneo la nane nane lililopo Msamala kwenye bar iliyopo kwenye eneo hilo.
Amesema kuwa mwananchi huyo baadae alishtuka na kupata wazo kwenda kwenye Ofisi za Takukuru ambako alitoa taarifa na kuwaeleza kwa kina juu ya maelezo aliyopewa na Afisa Mtendaji Luambano ambapo baadae Maafisa wa Takukuru waliweka mtego kisha walimtaka mwananchi huyo awasiliane na Afisa Mtendaji mahali watakapokutana kupeana fedha hizo.
Mkuu wa Takukuru Mkoani Ruvuma Masiko amesema kuwa baada ya mwananchi huyo kufanya mawasiliano na Afisa Mtendaji Luambano Takukuru ilimpatia fedha shilingi elfu 20,000 na kumtaka ande mahali walipokubaliana kupeana fedha hizo huku maafisa wa Takukuru wakiwa wanamfuatilia kwa karibu na walipofika kwenye eneo la tukio alimkuta Luambano akiwa anamsubiri kwenye bar ambako alimkabidhi fedha hiyo na baada ya muda mfupi maafisa wa Takukuru waliizingira bar hiyo na kumkuta Luambano akiwa na fedha shilingi elfu 20,000 aliyopewa na mwananchi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa.
Amefafanua zaidi kuwa Luambano ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Serikali wa Mtaa wa Tanga anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi elfu 20,000 ambayo ni kosa chini ya kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007
MWISHO
No comments:
Post a Comment