Na Gideon Mwakanosya,Songea
CHAMA cha akiba na Mikopo cha New Muungano SACCOS kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kimetoa mafunzo kwa wanachama wake 130 ya elimu ya ujasiliamali na elimu ya ushirika ili kuwasaidia wajasiliamali hao kufanya kazi kwa umahili zaidi.
Akifungua mafunzo hayo ya siku mbili Katibu wa New Muungano SACCOS Biatha Komba kwenye ukumbi wa shule ya msingi Mfaranyaki alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwasaidia wanachama wake kujua elimu ya ushirika na ujasiliamali ili wanapokopa mikopo yao waitumie kwa matumizi sahihi kama walivyoomba.
Komba alisema kuwa pia wananchama wake ni lazima wajue sheria ,kanuni na misingi ya ushirika ili wanapofanya kazi zao za kila siku wasipatwe na usumbufu wa aina yeyote katika mitaji,na masoko kwa biashara wanazofanya.
Aliainisha changamoto ambazo zinaikabili chama hicho kuwa ni pamoja na mfumuko mkubwa wa taasisi zisizo rasmi za kifedha ambazo zimekuwa zikifanya kazi ya kukopesha wafanyabiashara na wafanyakazi wakiwemo walimu fedha, vitendea kazi vya kisasa kama kompyuta,fotokopi mashine pamoja na usafiri kwaajiri ya kuwafuata wanachama na kupeleka fedha benki.
Kwa upande wake Afisa Tawala wa Tarafa ya Songea Magharibi Blanka Luambano ambaye ndio alikuwa mgeni rasmi aliupongeza mradi wa SELF kwa kuifadhiri SACCOS hiyo ambayo imeonekana kuwa ni msaada mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Alisema kuwa New Muungano SACCOS ni miongoni mwa taasisi chache za fedha ambazo zimejikita zaidi katika kusaidia kuondoa umasikini kwa wafanyabiashara wadogo na kwamba kwa muda wote imekuwa ikiwahimiza wanachama wake kukopa fedha kwaajiri ya kukuza biashara zao wanazozifanya kila siku.
No comments:
Post a Comment