Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kanali Edmund Mjengwa
Na Cresencia Kapinga,Mbinga
SERIKALI wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma imeagiza kuwachukulia hatua kali za kisheria viongozi wa kijiji na kata wakiwamo Madiwani pamoja na makatibu tarafa ,ambao maeneo yao yatakumbwa na uchomwaji moto bila wahusika kuchukuliwa hatua yoyote.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kanali Mstaafu Edmund Mjengwa kwenye kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa jumba la maendeleo uliopo wilayani humo.
Kanali Mjengwa alisema kuwa ipo tabia ya viongozi kama vile Watendaji wa Vijiji na kata pamoja na Madiwani wao ambao wamekuwa wakiona matukio ya uchomaji moto kwenye maeneo yao lakini hakuna hatua wanazozichukuwa.
"Naagiza ya kwamba kuanzia sasa tukio la moto likitokea kijijini kwako na zisipochukuliwa hatua za kuuzima,viongozi wa eneo husika watakuwa wa kwanza kuchukuliwa hatua za kisheria vinginevyo muhusika afikishwe katika vyombo vya sheria ili sheria ichukuwe mkondo wake" alisema Kanali Mjengwa.
Aidha amewaagiza Madiwani wa Wilaya hiyo kuwaelimisha Wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwani imeonekana wananchi wengi hawajui umuhimu wake hivyo kufanya vitendo vya ukataji wa miti na uchomaji moto kuwa ni vya kawaida na ni sehemu ya maisha yao ya kila siku pasipo kujua athari zake.
Pia amewaagiza makatibu tarafa wote wa wilaya hiyo kuwachukulia hatua watu wote ambao wamejenga kwenye vyanzo vya maji ili kuvinusuru vyanzo hivyo kukauka na kusababisha wananchi waingie kwenye janga la ukosefu wa maji kutokana na watu kufanya makazi kwenye vyanzo hivyo.
Alisema kiutaalamu maeneo ya vyanzo vya maji hayapaswi kuwekwa makazi ya watu kwani yanaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo magonjwa ya mlipuko na kukauka kwa vyanzo hivyo kutokana na baadhi ya watu wengine kulima kwenye vyanzo hivyo bila kujari hathari ambayo inaweza kutokea hapo baadae.
Tatizo hili la vyanzo vya maji kuathirika linaonekana sana kule Mbinga. Hata kijijini kwangu, ambako naenda kila ninapoweza, kuna mifereji ambayo ilikuwa na maji mengi wakati nilipokuwa mtoto, lakini leo au maji ni haba sana, au yamekauka. Kuna sehemu kijijini kwangu ambazo zilikuwa na chemchemi na maji kububujika, lakini leo ni kavu. Ni janga kubwa tumejiletea, na tusipoangalia, tutalazimika kusafiri mbali kwenda kutafuta maji.
ReplyDelete