MWANDAAJI: SONGEA NETWORK OF NON – GOVERNMENTAL ORGANIZATIONS (SONNGO)
MADA: MAPITIO YA KATIBA YA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA 1977 ILIYOFANYIWA MAREKEBISHO 2005
MTOA MADA: ODDO EGINO HEKELA
AFISA KAZI RUVUMA , NA MKURUGENZI WA KAMPUNI YA KAZI BUREAU SERVICES CO.LTD
P.O. BOX 1050, SONGEA
TEL: 0784 332 378/ 0655 332 378/0755 094 862
E- MAIL: odo.egino@yahoo.com
MADA: MAPITIO YA KATIBA YA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA 1977 KAMA ILIVYOFANYIWA MAREKEBISHO 2005.
1.0 UTANGULIZI
1.0 MAANA YA KATIBA
Katiba ni sheria mama ya nchi inayotoa au kuweka Utawala na eneo la utawala, madaraka ya viongozi na mgawanyo wa majukumu katika miimili yote mitatu ya Serikali yaani Bunge, Mahakama na watendaji wa Serikali (Parliament, Judiciary and Executives).
2.0 KATIBA YA KUDUMU (1977) KAMA ILIVYOFANYIWA MAREKEBISHO 2005.
Katiba hii ilipatikana kupitia tume ya Rais yenye wajumbe 20 yaani 10 kutoka Bara na 10 kutoka Visiwani (Zanzibar ). Katiba hii iliitwa Katiba ya kudumu. Kabla ya kuandaliwa Katiba hii tume hii ilianza kuandika Katiba ya CCM baada ya kuunganisha vyanma vya TANU na ASP tarehe 5/2/1977. Katiba iliweka misingi mikuu ya madaraka na majukumu
i. Mfumo wa chama kimoja
ii. Uraisi wenye nguvu zaidi na
iii. Mfumo wa Serikali mbili.
Katiba ya kudumu ilipitishwa na Rais na baadae aliteua Bunge la kawaida kujigeuza kuwa Bunge la Katiba na kupitisha Katiba ndani ya masaa matatu tu. Katiba hii imefanyiwa marekebisho mengi kufuatia mahitaji ya Taifa kwa nyakati mbalimbali hadi 2005. Mabadiliko makubwa ni yale ya kuruhusu tena uwepo wa vyama vingi na uanzishwaji wa tume ya uchaguzi ya Taifa (NEC), ongezeko la viti maalum na uwiano wao (2005).
3.0 SERIKALI YA WATU
Katika sehemu ya pili ya Katiba, Ibara ya 8 (1) ya Katiba ya mwaka 1977, na marekebisho ya 2005, inasema;
· Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii. Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote.
· Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi.
· Lengo kuu la Serikali ni ustawi wa wananchi.
· Serikali itawajibika kwa wananchi.
· Wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao .
Sheria iliyoundwa kutoa maelekezo ni sheria ya Serikali na watu ya 1984 na. 15.
Swali ni je?
Uwanja wa demokrasia umepanuliwa na kuwapa wananchi madaraka ya kuweka Serikali kama wapendavyo? Na nini kifanyike?
3.1 UJENZI WA UJAMAA NA KUJITEGEMEA
Ibara ya 9 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania 2005 inatoa msingi huu kwa kutamka uelekeo wa nchi ni wa ujamaa na kujitegemea. Kwa hiyo sera na shughuli zote za Serikali zielekeze nguvu katika ujenzi huo.
Mambo yaliyowekewa mkazo na Katiba hii ni:
· Utu na haki za binadamu.
· Utawala wa sheria.
· Utajiri wa Taifa unakuwa kwa manufaa ya umma.
· Ulinganifu na ushirikishwaji wa wananchi katika maendeleo ya nchi.
· Kazi kama shughuli halali.
· Heshima ya binadamu inahifadhiwa.
· Hakuna ubaguzi wa rangi, jinsi, kabila, dini wala hali ya mtu.
· Dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu na upendeleo zinaondolewa nchini.
· Utajiri wa Taifa unanufaisha umma.
· Hakuna ulimbikizaji wa mali .
· Demokrasia inatawala zaidi.
Swali ni je?
1. Tunauhitaji wa kuendelea na msingi wa ujamaa na kujitegemea? Kama ndio kwa uelekeo gani?
2. mali asili ya nchi imewekewa misingi ya umiliki kwa faida ya umma?
4.0 SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO
Ibara ya 34 (1) inasema kutakuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo itakuwa na mamlaka ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya muungano, na pia juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara.
Swali ni je?
Hakuna uwezekano wa kuwa na Serikali tatu yaani Tanganyika , Zanzibari na Muungano?
4.1 MADARAKA YA RAIS
Ibara ya 33 (2) ya Katiba 1977 na marekebisho ya 2005, inasema Rais atakuwa Mkuu wa Nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Rais anapewa madaraka yafuatayo na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania .
Upana wa Madaraka ya Rais
· Mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa umma. Ibara ya 36(1) ya katiba 1977,iliyorekebishwa 2005
· Kuwateua watu kushika nafasi za madaraka. Ibara ya 36 (2) ya Katiba 1977, iliyorekebishwa 2005.
· Madaraka ya kuwapandisha vyeo au kuwafukuza kazi Ibara 26 (3) ya Katiba 1977, 2005.
· Kudhibiti nidhamu katika watumishi wa Serikali Ibara ya 36 (4) 2005.
· Hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote , isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au sheria nyingine Ibara ya 37 (1) ya Katiba 2005.
· Madaraka ya kutangaza vita, Ibara ya 44 (1) ya Katiba 2005, inatoa madaraka kwa Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania .
· Uwezo wa kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele za mahakama kwa kosa lolote bila ya masharti au kwa masharti Ibara ya 45 (1) (a) (b) 2005.
· Kuibadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote iwe adhabu tahalifu Ibara ya 45 (1) (c), 2005.
· Kufuta adhabu yoyote au sehemu ya adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa ajili ya kosa lolote au kuhozi (kuchukua) kitu cha mtu mwenye hatia ambacho vinginevyo kingechukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 45 (d) ya Katiba 2005.
Swali ni je?
Akitoa upendeleo wowote nani atakuwa na jukumu la kuuliza au kupinga katika madaraka makubwa kiasi hicho?
4.2 UTEUZI WA MAWAZIRI
Katiba inampa madaraka hayo Rais ya kuteua mawaziri wake wa kusaidia Serikali yake. Ibara ya 55 (1) ya Katiba 1977, iliyorekebishwa ,2005.
Ibara ya 55(4) ya katiba 1977, iliyorekebishwa 2005 inasema; Mawaziri na manaibu mawaziri wote Katiba inataka watokane na Wabunge waliounda Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Swali ni je?
Hakuna uwezekano wa kupata mawaziri wasio wabunge kwa mujibu wa Katiba?
4.0 MADARAKA YA BUNGE
i. Bunge letu linaundwa na sehemu mbili yaani Rais na Wabunge. Kwa mujibu wa Ibara ya 62 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano 2005. Kwa hiyo Bunge letu linapoteza uwezo wa kujitegemea ukilinganisha na Bunge la Uingereza na Marekani kwa kuwa shughuli zake zinawezeshwa na Rais wa Nchi. Na maamuzi yake yanachujwa na Rais wa Nchi kwa mujibu wa Ibara ya 63 (1) Rais kama sehemu moja ya Bunge atatekeleza madaraka yote aliyokabidhiwa na Katiba hii kwa ajili hiyo.
Bunge letu lina uwezo wa kupendekeza kwa Rais kuhusu kumuondoa mtu au kumweka mtu madarakani kutokana na utovu wa nidhamu au wizi uliotendeka katika kusimamia Serikali lakini siyo kumuondoa, au madaraka ya kumwondoa mtu kama huyo yapo kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Swali ni je?
Kwa kufanya hivyo hatuoni kwamba Bunge linapunguziwa uwezo kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba 1977, iliyorekebishwa, 2005?
ii. Madaraka ya kutunga sheria katika Ibara ya 63 (3) (d) ya Katiba ya 2005, Bunge linapewa uwezo wa kutunga sheria ili ifanye kazi inahitaji mkono wa Rais na ridhaa yake. Baada ya Bunge kutunga sheria haiwezi kufanya kazi kama rais hajasaini na kuifanya kuwa sheria katika nchi.
Swali ni je?
iii. Madaraka ya Bunge la jamuhuri ya muungano wa Tanzania dhidi ya Serikali ya Zanzabar ni madogo sana Ibara ya 64 (3) (4) ya 2005. Baraza la wawakilishi la Zanzibar ndilo lenye madaraka makubwa na maswala ya Zanzibar .
Swali ni je?
Baraza la wawakilishi katika serkali ya mapinduzi la Zanzibar haliwezikukinzana katika maamuzi na Bunge la muungano?
5.0 SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBARI
Katika sura ya nne ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, iliyorekebishwa ,2005 Ibara ya 102 (1) inataja kuwa kutakuwa na serikali ya Zanzibar itakayojulikana kama Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibari na ambayo itakuwa na madaraka na mambo yasiyo ya Muungano kwa mujibu wa masharti ya Katiba yenyewe.
Swali ni je?
Kwa nini katika Katiba hakuna madaraka ya Serikali ya Tanganyika ? Je kuna umuhimu wa kuanzisha Serikali hiyo?
Swali lingine ni je? Ni muhimu kuwa na Serikali za Majimbo ili kupunguza uwezekano wa kuwa na Serikali nyingine ya tatu yaani Tanganyika ?
6.0 UHURU WA MAHAKAMA
Sura ya tano ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, iliyorekebishwa, 2005 Ibara ya 107 (1) ya Katiba ya 1977, 2005 inaunda mamlaka ya kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano kuwa ni Mahakama.
Ibara ya 107 (B) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatamka kuwa Mahakama itakuwa huru katika utekelezaji wa shughuli zake kwa mujibu wa sheria na katiba za nchi. Ambapo mwaka 2002 iliundwa sheria ya Uhuru wa Mahakama sheria namba 3 ya mwaka 2002.
Swali ni je?
Kweli Mahakama zetu zipo huru mbali na madaraka ya Rais wa nchi katika kutekeleza majukumu yake?
i. Nani anamchagua Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi?
ii. Nani anachagua Majaji wa Mahakama Kuu?
iii. Je anayewachagua anaweza kuwa chini ya maamuzi au hizo posti ziwe za ushindani kama walivyofanya Kenya ? Ibara ya 118 ya Katiba 1977, iliyorekebishwa, 2005.
7.0 HAKI ZA BINADAMU
i. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 14 – 24 ya katiba ya 1977, iliyorekebishwa mwaka 2005, inatoa haki za raia wa Tanzania . Miongoni mwa ya haki hizo ni haki ya kuishi .
Swali ni je?
wakati Mahakama imepewa uwezo wa kutoa adhabu ya kifo. Katiba inatoa haki ya kuishi je? Kunauwezekano wa kufuta adhabu ya kifo?
ii. Katiba imetoa haki ya kumiliki mali kwa raia wa Tanzania lakini kuna baadhi ya mali huwezi kumiliki kama madini, mafuta na vito vya thamani kwa mujibu wa sheria ya Ardhi na madini. Hivyo wakati upande mmoja unatoa upande mwingine unanyang’anya.
Swali ni je?
Ardhi na madini yaliyomilikiwa kiasili yawekewe dhamana ya fidia na umiliki kwa wanaokutwa katika eneo hilo ?
Ibara ya 8 ya katiba 1977, 2005 inasema Serikali inawekwa na wananchi kwa ajili ya rasilimali zao na lengo kuu ni ustawi wao.
8.0 MADARAKA YA SERIKALI ZA MITAA (LOCAL AUTHORITY)
Sura ya nne ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, iliyorekebishwa, 2005 inaunda serikali za mitaa na madaraka yake. Ibara ya 145 (1) ya Katiba ya 2005, inatoa muundo wa Serikali ya Mitaa kila Mkoa, Wilaya, Miji, Kata ka Kijiji cha Tanzania .
Lengo la Serikali ya Mitaa ni ushirikishwaji wa madaraka katika maeneo yao hasa maamuzi ya maendeleo yao .
Swali ni je?
Kuna haja ya kuongeza madaraka hayo katika kukusanya mapato ya uzalishaji katika maeneo yao ? Mfano maeneo ambayo kuna makaa ya mawe, dhahabu, chuma na madini mengine katika maeneo hayo asilimia ya kodi au mrahaba unabaki katika Serikali yao uelekezwe kwao ili kuleta mabadiliko katika eneo husika?
HITIMISHO
Tumejaribu kupitia maaeneo kadhaa ya Katiba yetu na kuona kama tunaweza kuyaangalia na kutolea mapendekezo bora zaidi.
Hivyo ni jukumu lako kutoa mapendekezo ya maboresho kuhusu Katiba mpya katika maeneo hayo tuliyoyapitia. Lakini pia ufungwi kupanua wigo wako wa uelewa wa Katiba kwa kutoa maoni eneo lingine zaidi.
No comments:
Post a Comment