About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Tuesday, January 31, 2012

WAKULIMA SONGEA WATAKIWA KULIMA KWA WINGI NA KWA KUZINGATIA KANUNI BORA ZA KILIMO


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu akiongea na watendaji wa vijiji vya Magagula.Muungano Zomba na Lugagara wilaya ya Songea jana alipotembelea kuhamasisha wakulima kuzalisha mahindi kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo.Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Sabaya(kulia) na mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea Rajab Mtiula(Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma)




Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu (mwenye kaunda suti nyeusi) akisikiliza maelezo ya kilimo kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Songea Thomas Sabaya (kulia) wakati wa ziara ya kukagua usambazaji wa pembejeo kijiji cha Lugagara wilaya ya Songea


Wakulima wa kijiji cha Magagula wilaya ya Songea wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu (hayupo pichani) jana alipofanya ziara ya kukagua shughuli za kilimo
Na Revocatus A.Kassimba,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
SERIKALI imewataka wakulima  mkoani Ruvuma kulima kwa wingi mahindi katika msimu huu kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo licha ya changamoto za soko lililowakabiri msimu wa kilimo uliopita.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu wakati wa ziara yake katika vijiji vya Magagula, Lugagala na Muungano Zomba vilivyopo wilaya ya Songea .
Mwambungu aliwaeleza wananchi kuwa serikali inatambua kero ya ununuzi wa mahindi iliyotokea msimu wa 2011/2012 ambapo wakulima wengi walichelewa kupokea fedha zao kutoka Wakala wa Hifadhi za Chakula (NFRA).
Aliongeza kusema kuwa changamoto ya fedha za wakulima hazitajitokeza tena msimu ujao kwani tayari serikali imejiandaa kwa kutengwa fedha katika bajeti ili kuhakikisha mahindi yote yatanunuliwa kwa wakati.
“Limeni kuliko mwaka jana kwani serikali imejipanga kununua kwa wakati na kuhakikisha kuwa hakuna mkulima atakayecheleweshewa malipo na serikali” alisema Mwambungu na kuongeza kuwa hakuna mkulima sasa anayeidai serikali wote wamelipwa.
Mkuu wa mkoa Mwambungu alisisitiza kuwa serikali inafanya kila linalowezekana kuondoa kero ya kukopa mahindi ya wakulima hivyo ni vema wakulima wakaendelea kuunga mkono juhudi hizi za serikali kwa kuongeza uzalishaji.
Katika msimu 2011/2012 wa kilimo kwa mujibu wa taarifa za Wakala wa Hifadhi ya Chakula jumla ya tani 50,018 za mahindi zimenunuliwa kutoka kwa wakulima mkoani Ruvuma zenye thamani ya shilingi bilioni 17.5 ambapo kilo ilinunuliwa kwa shilingi 350.
Mkuu wa Mkoa alitumia fursa hiyo kuwapongeza wakulima wa vijiji hivyo alivyovitembelea kwa kutumia vema pembejeo za ruzuku kwa mfumo wa vocha kwani wameongeza uzalishaji wa mahindi na kuifanya wilaya ya Songea kuongoza katika kuzalisha mahindi mkoani.
Ziara ya Mkuu wa mkoa ilihusisha pia kukagua zoezi la ugawaji wa vocha za pembejeo ambapo kwa mujibu wa taarifa ya iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Songea Thomas Sabaya alisema wilaya imepata mgao wa vocha 64,417 ambazo zimesambazwa kwa wakulima.
Sabaya alisema vocha hizo zinahusisha mbegu bora za mahindi, mbolea ya kupandia na mbolea ya kukuzia ambapo bei ya mfuko wa mbolea ya kupandia (DAP) inauzwa shilingi 80,000/=huku mkulima akichangia shilingi 52,000/=.
Kuhusu mbolea ya kukuzia (UREA) mfuko unauzwa shilingi 72,000/= na mkulima anachangia shilingi 52,000/= huku serikali ikilipia zinazobaki na kwa mbegu bora mfuko unauzwa shilingi 40,000/= huku mkulima akichangia 20,000/= na serikali zinazobakia.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lugagara Bi Taifa Mahundi katika risala yake alisema wakulima wana changamoto kubwa ya upungufu wa vocha za ruzuku hivyo akaiomba serikali kuongeza mgao kwa kijiji.
Mkuu wa mkoa akijibu hoja hiyo aliwafahamisha wananchi kuwa vocha zinazotolewa ni vigumu kufanana na idadi ya wakulima kwani hiyo ni ruzuku itolewayo na serikali kuwasaidia wakulima kujenga uwezo wa kujitegemea.
Katika msimu huu wa kilimo mkoa wa Ruvuma umepatiwa vocha za ruzuku ya pembejeo za kilimo 192,000 ambapo kwa mwaka uliopita ulipatiwa vocha 204,000 hivyo kuwa na upungufu wa vocha 12,000/=.
Mkoa wa Ruvuma ni kati ya mikoa sita maarufu kwa uzalishaji wa mahindi nchini ambapo mikoa mingine ni Iringa, Mbeya, Rukwa, Kigoma na Morogoro.
…………………………………………………………………………………………………
Revocatus A.Kassimba
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma

No comments:

Post a Comment