Na Stphano Mango,Songea
HAKUNA sululu itakayoweza kukidhi mahitaji ya Taifa lolote Duniani kwa kuongeza kasi ya maendeleo na kukuza uchumi wa nchi kama Serikali husika itashindwa kuwekeza katika elimu ya sayansi na teknolojia kwa wananchi wake
Kwani ni ukweli ulio wazi kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia katika nchi nyingi duniani ni nguzo muhimu ya maendeleo kutokana na umuhimu wake katika kuvumbua maarifa mapya ambayo hutumika viwandani ili kuzalisha bidhaa mbalimbali
Dhana ya sayansi kinadharia ni chachu katika kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa nchi na kubadili mfumo wa maisha kutoka kwenye lindi la umaskini hadi kwenye ustawi stahiki wa maisha ya binadamu kwa kuweza kuwa na huduma bora za kijamii
Tafsiri sahihi ya dhana ya sayansi kama ilivyotafsiriwa na kamusi ya Kiswahili sanifu toleo la 2004, inaeleza kuwa ni elimu inayotokana na uchunguzi,majaribio,vipimo na kuthibitishwa kwa muda uliopo,utafiti huo unaleta jawabu sahihi la matumizi yake kwa wakati uliopo
Kamusi hiyo inaendelea kufafanua kuwa teknolojia ni maarifa ya sayansi yaliyowekwa katikamatumizi ya vitu mbalimbali kama zana au mitambo katika viwanda,mawasiliano,ufundi na kilimo
Kulingana na tafsiri hiyo ni wazi kuwa sayansi ndio baba wa teknolojia inayopandwa kwa binadamu ili kumwezesha kutumia maarifa hayo katika kuleta mapinduzi ya maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla
Nchi za Magharibi kama Marekani,Kanada,Uingereza,Ujerumani,Ufaransa na zile za Mashariki kama Urusi,China,Japan Na India ni miongoni mwa nchi zilizojikita katika kupanua wigo wa taaluma ya sayansi
Ambapo mafanikio ya teknolojia ya sayansi katika nchi hizo yamesaidia kufanikisha malengo ya tafiti mbalimbali ambazo nyingi kati ya hizo zinatokana na uzalishaji katika sekta ya viwanda
Mfano wa uzalishaji huo upo wazi kama vile simu za mkononi,modemu za intaneti,flash disk,Cd,memori card ambapo uzalishaji huo umewezesha kufanyika kwa biashara za kimataifa katika muda mfupi
Idadi kubwa ya wafanyabiashara wamekuwa wakijihusisha na biashara hizo kutoka nchi za Mashariki ya mbali kwa kuagiza kupitia teknologia ya mtandao na kuziingiza kwenye nchi zao ikiwemo na wafanyabiashara wa Tanzania na kusifia ubora wa bidhaa hizo kupitia matangazo mbalimbali utafikiri huko kiwandani wakati bidhaa hiyo inatengenezwa alikuwepo
Tumekuwa mabingwa wa kusifia bidhaa za wenzetu bila nasi kushiriki katika ugunduzi wa teknolojia iliyozalisha bidhaa hiyo,hivyo sasa ni muda muafaka wa kujiuliza vitu tunavyotumia leo katika maendeleo ya sayansi na teknolojia watanzania tumechangia nini?
Tunafurahia kama mazuzu kuruka kwa ndege kutoka sehemu ya mkoa hadi mwingine,nchi mpaka nchi nyingine kwa haraka,je mchango wetu kwenye kifaa hicho uko wapi? Vifaa kama vile kompyuta,luninga ambavyo tunavitumia kuangalia mambo mbalimbali duniani mchango wetu upo?
Sayansi ndiyo iliyovumbua matumizi ya kompyuta,utengenezaji wa mitambo,ndege,meli,magari,roketi,rada,zana za kivita,ujenzi wa majengo na barabara vyote ni kutokana na dhana ya sayansi
Jambo la kujiuliza ni njia zipi zinazofanikisha teknolojia hiyo kufanikiwa katika nchi husika? Hapo sasa ni wajibu wa serikali kujipanga katika elimu elekezi na thabiti ambayo itafanikisha teknolojia hiyo kupatikana mashuleni
Tunahitaji elimu ya ubunifu ambayo imesheheni vitendo kuliko nadharia kwani elimu ya uvumbuzi ndio ambayo imesaidia nchi nyingi duniani kuwa na maendeleo endelevu na kuachana na maendeleo bandi ambayo sisi tumekuwa tunajivunia huku tukisubiri kila kitu kulishwa kutoka kwenye mataifa mengine kana kwamba siye tumekuwa mazuzu
Nchi zilizoendelea zilitumia muda mwingi kutoa kipaumbele cha elimu kwa wananchi wake katika Nyanja ya sayansi pamoja na ugumu wake na ukubwa wa gharama za kuisomea kuliko masomo mengine lakini faida yake ni kubwa sana
Kuendelea kuogopa kuwekeza elimu ya sayansi nchini ni kushindwa kuwapata wanasayansi halisi kwa kipindi chote toka nchi ipate uhuru wake mwaka 1961 kwani elimu ya chuo kikuu ilinayoendelea kutolewa leo nchini inamahusiano ya masomo ya jamii pekee yake
Kutolewa kwa elimu ya sayansi kunahitaji mitambo ambayo itamwezesha mwanafunzi kufanya majaribio ya vitendo na kubaini majibu ya nadharia aliyojifunza darasani,uwepo wa na miundombinu stahiki yatakuwa yanamsaidia mwanafunzi kuunda,kuvumbua vitu
Elimu hiyo ndio ya kujivunia kwani ndiyo wanayoitumia wenzetu kuitawala dunia yetu leo hii hivyo katika suala hili ni lazima masomo ya sayansi yapewe msukumo zaidi kwa kufundishwa na walimu waliobobea ili kuweza kuleta zao stahiki
Hapo Mitaala ya sayansi ni lazima ziwe na maabara nzuri zilizojitosheleza kwa vifaa vinginevyo wanafunzi wa shule hizo wataishia katika masomo ya nadharia na Taifa litaendelea kukodisha teknolojia kutoka katika nchi zilizoendelea kisayansia
Somo kama fizikia ni lazima wanafunzi wapatiwe vitabu vya kutosha ambapo somo hilo linapaswa lifundishwe kwa kina hasa kwa vitendo hivyo somo hilo halipaswi kufundishwa kwa ajili ya kuwasaidia kufanya mtihani tuu
Wafundishwe somo hilo kuibua ubunifu wa wanafunzi ,tuachane na tabia ya kuwafundisha kufaulu mitihani kwani dunia ya sasa inahitaji watu ambao ni wabunifu hata masomo ya kemia na bayolojia yanatakiwa yawajengee uwezo wa kisayansi wanafunzi hao
Teknolojia ni nguzo muhimu ya kuanzisha viwanda vya mitambo ya juu,kati na midogo ambapo mitambo mikubwa ni pamoja na ile ya kutengeneza magari,matrekta,mashine za kufuma nguo,ya kutengenezea barabara ,madaraja na inayotumika kuchimbia madini migodini
Elimu ya sayansi huwawezesha wataalam kubuni mambo mbalimbali ya vyombo vya mawasiliano,utengenezaji wa silaha na ufundi wa zana mbalimbali
Watafiti mbalimbali wa kisayansi wanafafanua kuwa ukosefu wa teknolojia unaongeza umasikini katika jamii na taifa kwa ujumla hivyo uwekezaji katika elimu ya sayansi ungesaidia kufanya tafiti mbalimbali za mafuta,makaa yam awe na mali asili zingine
Ukosefu wa elimu ya sayansi ndio chanzo cha ukodishaji wa maliasili za nchi kwa makampuni ya kigeni kwa makampuni ya kigeni kwa kuwa taifa husika halina uwezo wa kufanya tafiti hizo hata kwa upande wa viwandani utafiti wa dawa za binadamu na mifugo unahitajika ili kuboresha huduma zinazotolewa na sekta ya afya
Wakati umefika sasa tuwe na wataalam ambao wanaweza kutengeneza vifaa tulivyoviainisha hapo juu mfano upo wazi Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) waliweza kutengeneza gari aina ya Nyumbu hiyo ni ishara njema kwa taifa letu hivyo tuwekeze huko
Ni lazima tujiulize kuwa Japan inayozalisha utitiri wa magari ya aina ya Toyota ambayo yamesambaa dunia nzima wao wana nini zaidi yetu au India inayozalisha magari aina ya Tata wana nini zaidi yetu
Jibu ni rahisi,uwekezaji kwenye elimu ya sayansi ambayo italeta uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali kwani wenzetu wameweza kuwekeza huko na kuchukua muda mwingi kufikiria ubunifu wa kitu furani ambacho kitakuja kukuza uchumi wa nchi yao
Kama tutashindwa kuchukua hatua stahiki leo basi nchi za Marekani ,Korea,China,Urusi,India na mataifa mengine yataendelea kugeuza nchi za afrika maeneo ya kuuzia bidhaa zao kwa sababu sisi hatuna mchango katika uzalishaji
Hatari yake nyingine licha ya kwamba nchi yetu itageuzwa jalala la bidhaa nyingine hata watu wetu watageuzwa watumwa wa kuuza bidhaa za nchi hizo kwa sababu elimu ya uvumbuzi tumeishiwa hivyo tuzinduke kama kweli tunataka kuwa sehemu ya maendeleo yaliyopo duniani
Ni aibu kuendelea kuimba kuwa sisi tuna maendeleo ya sayansi na teknolojia wakati kila tunachotumia kinatoka nchi za wengine nasi kazi yetu kusifia tuu uzuri wa kitu hicho utafikiri tulikuwepo wakati kinatengenezwa
Mwandishi wa Makala
Anapatikana 0755-335051
No comments:
Post a Comment