About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Monday, September 24, 2012

WANANCHI WILAYANI TUNDURU WAHOFIA MAISHA YAO

Na Steven Augustino,Tunduru IMEELEZWA kuwa Serikali isipochukua hatua za makusudi kuzuia na kutuliza vitendo vya uchomaji wa mabanda ya Nguruwe,kuharibu mali za watu pamoja na kuchoma moto nyumba vinavyo endelea kwa siku tano mfululizo huenda wimbo wa amani na utulivu ambao umekuwa ukiimbwa kila pembe ya nchi yetu ukatoweka hususani maeneo ya Wilayani hapa. Minong'ono na kauli za baadhi ya Wananchi kuanza kukosa uvumilivu imeanza kujitokeza kufuatia matukio hayo yanayo onesha kuhatarisha amani yanayo jitokeza mjini hapa huku vikundi vinavyo daiwa kutumia mwamvuli wa madhehebu ya Waislamu wenye msimamo mkali kuendelea kuvamia na kuchoma moto makazi ya watu na mazizi ya nguruwe. Kwa mjibu wa matukio hayo katika kipindi hicho Jumla ya mazizi 24 yamelipotiwa kuteketezwa na moto ambao jumla ya nguruwe 61 wameuawa pamoja na kuunguza nyumba za makazi ya watu vyote vikakadiliwa kuwa na thamani kiasi cha zaidi ya milioni 11 vimehalibiwa na kuziacha familia husika zikirudi katika lindi la umasikini uliopindukia. Wakiongea kwa nyakati tofauti, waathirika wa matukio hayo ambao wanaishi mitaa wa Nakayaya,Tuleane na Xtended mjini hapa, Luka Victor na Casian Asenga walisema kuwa kikundi hicho ambacho kimekuwa kikifanya matukio hayo majira ya usiku wa manane na kuharibu mali kwa kuchoma mazizi na nyumba zao na kuua nguruwe wameharibu na kuvuluga mifumo ya maendeleo yao. Nae Douglas Mwasimba alisema kuwa wahalibifu hao wa mali zake walivamia katika nyumba yake majira ya saa nane usiku wakati amelala na kwamba alisikia nguruwe wanalia kwa pamoja kilio kilichoashiria tukio lisilo la kawaida na alipoamka na kuelekea kwenye mazizi aliona moto mkubwa na tayari nguruwe wake 38 walikuwa wameteketea na moto huo huku nguruwe 51 wakiwa wamejeruhiwa kwa kuunguzwa na moto huo. Akielezea kwa masikitiko makubwa Thomas Mumba muuzaji maarufu wa nyama ya nguruwe mjini hapa, alisema kuwa kikundi hicho usiku huohuo kilifika kwake mnamo saa tisa na kilifanikiwa kuchoma zizi na kuua nguruwe 3 na kuwajeruhi wengine 5. Nako kwa Godfrey Mgao nguruwe 4 wameuawa na 5 wamejeruhiwa. Aidha Kikundi hicho hakikuishia hapo kwani siku ya pili kiliendelea na kampeni yao hiyo hadi katika Mtaa wa Tuleane na kuchoma moto Mazizi ya Mradi wa Kanisa Angarikana wanaofugiwa katika nyumba ya mchungaji wa Kanisa Mch. Edwin Nakajumo pamoja na mazizi ya Afisa maendeleo ya Jamii Mary Ding'oi ambako walifanikiwa kuchoma mazizi na moto huo kudhibitiwa mapema. Walisema inaonesha wazi walengwa wa matukio hayo ni Waumini wa madhehebu ya kikristo Siku ya tatu kikundi hicho kilirudi tena mtaa wa Nakayaya hadi kwa Mchungaji wa Kanisa La Biblia Mch. Yakobo Milanzi na -kufanikiwa kuchoma mazizi na kujeruhi nguruwe 8 Haikutosha kikundi hicho kilifika mbali zaidi kwa kutaka kuua watu usiku wa siku iliyofuata kikudi hicho kilifika na kuunganisha umeme (to shorten) kwa makusudi na kuiunguza nyumba na Mashine ya kusaga mali ya Godfrey Christopher pia walifanikiwa kuteketeza kwa kuchoma moto nyumba ya Jastene Severin Magwinda Walifanikiwa na nyumba hiyo iliwaka moto. Haikuleta madhara kwa binadamu kwani wote waliolala humo walinusulika kifo kutokana na tukio hilo. Akizungumzia matukio hayo Mweyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Wilaya hiyo Chande Nalicho mbali nakukiri kuwepo kwa matukio hayo aliwahakikishia wananchi wa mji waTunduru na Wilaya kwa ujumla kuwa serikali imejipanga kuhakikisha kuwa hali ya usalama inarejea katika hali ya kawaida Aidha Dc,Nalicho aliendelea kubainisha taarifa yake kuwa tayari serikali imeandaa mikakati mbalimbali ya kuhakiksiha kuwa watuhumiwa wa matukio hayo wana kamatwa ili sheria iweze kufuata mkondo wake na akatumia nafasi hiyo kuwaomba Wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa kwa kuwataja watuhumiwa kwa siri katika ofisi yake. mwisho

Thursday, September 20, 2012

AMRI HALALI INAYOTUMIWA NA JESHI LA POLISI KUSABABISHA MAAFA KWA RAIA, INAMAANA GANI? TUTAFAKARI KATIKA MAKALA HAYA

MOJAWAPO ya majibu ambayo yamekuwa yakitolewa katika kuhalalisha matumizi ya nguvu dhidi ya raia, ni kuwa ‘raia wanapaswa kutii amri halali’. Jibu hili wakati mwingine hutolewa likisisitiza kuwa serikali au vyombo vya dola vinapotoa amri, basi wale wanaoamrishwa wanatakiwa kutii tu “bila shurti”. Kwamba wakati mwingine polisi inawapasa watumie nguvu dhidi ya raia kwa sababu raia wamekataa kutii amri halali. Jibu hili limekuwa likitolewa hasa na wale ambao ni wapinzani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na watetezi wa serikali hii. Wanasema kuwa CHADEMA ni chama cha vurugu na kuwa matukio mbalimbali ya mauaji na watu kuumizwa ambako kumefanywa na vyombo vya dola kwa kweli ni makosa ya CHADEMA kwa sababu “kama wangesikiliza na kutii amri wanazopewa na serikali matatizo hayo yasingewakuta.” Kuna hisia kwamba askari au mtumishi wa serikali akiamuru kitu basi raia hapaswi kuhoji bali anapaswa kutii kwa vile amri lililotolewa ‘kihalali.’ Uhalali wa amri unatoka wapi? Kabla sijaangalia kama mtu anapaswa kutii amri anayopewa na ofisa wa serikali naomba nioneshe kwanza kitu kimoja muhimu sana. Amri haiwi halali kwa sababu imetolewa na mtu halali tu. Narudia tena hiyo kauli: Amri haiwi halali kwa sababu imetolewa na mtu halali. Uhalali wa amri unatakiwa ukidhi vigezo kadha wa kadha hicho cha kutolewa na mtu au chombo halali ni moja tu na peke yake hakitoshi kumlazimisha mtu kutii. Ile amri iwe halali, basi pamoja na kutolewa na mtu halali ni lazima itolewe kihalali. Mfano mzuri ni mtu ambaye ana kesi yake katika mahakama na baada ya upande wa mashtaka kumaliza mashtaka yake basi Jaji anaamua kutoa hukumu. Jaji ni mtu halali wa kutoa hukumu mahakamani lakini bila kutoa nafasi kwa utetezi basi mazingira ya kutolewa “kihalali” yanakosekana. Jaji hawezi baada ya kusikiliza upande wa mashtaka tu akaamua kumhukumu mtuhumiwa kifungo jela au kumwachilia. Katika taratibu za kawaida za kimahakama yule mtuhumiwa anatakiwa apewe haki yake ya kujitetea na kuonesha ushahidi au kuita mashahidi wote ambao wanaweza kumsadia asionekane mwenye hatia. Pamoja na kufanya hivyo, bado kuna taratibu za mahakama za kupima uzito wa ushahidi (law of evidence) ambapo baada ya kusikiliza pande zote mbili na kuangalia ushahidi unaotolewa na pande zote mbili Jaji hatimaye anaamua kutoa hukumu kwa masuala yale tu ambayo yanahusiana na kesi au zaidi yale ambayo yanabishaniwa. Lakini, licha ya kutolewa katika mazingira halali msingi mkubwa wa amri yoyote inayotolewa ni lazima itolewe ikiwa inaendana na ukweli. Amri ambayo inatolewa kwa uongo inaweza isisimame baadaye hasa ukweli ukijulikana. Hii ndio sababu amri yoyote halali ikiwa inazingatia vigezo vingine vyote inatolewa bona fide (in good faith), yaani kwa kuamini kuwa anayeitoea anaitoa akiwa anaamini ni kweli. Kwa mfano, kama baadhi ya vitu ambavyo viliongoza amri kutolewa vinapokuja kugundulika kuwa havikuwa vya kweli, basi aliyetoa hukumu hawezi kulaumiwa kwa sababu yeye alipotoa hukumu au agizo aliamini kuwa anafanya kwa haki na kwa usawa kabisa. Ni kutokana na hilo basi, yeyote anayetoa hukumu au amri yoyote ambayo anataka itekelezwe ni lazima yeye mwenyewe ajiridhishe kuwa yuko sahihi. Mfano mzuri ni wa mauaji ya Daudi Mwangosi. Kwa wale ambao walipata nafasi ya kuangalia mchakato mzima wa matukio hadi mwisho wake wataona kuwa sababu ya polisi kuingilia mkutano wa CHADEMA pale Nyololo ilikuwa ni kutokana na kuamini kuwa mkutano ule ulikuwa siyo wa “ndani” (internal meeting). Waandishi walijitahidi sana na kwa kweli wanastahili pongezi kumhoji kamanda Kamuhanda maana hasa ya “internal meeting”. Kamuhanda ambaye alinukuliwa kuwa ndiye alikuwa anatafsiri sheria zote pale alifanya kosa kubwa sana la kutopata ushauri kutoka kwa wenzake ili kujua kama maana ya “internal meeting” ni sawa na “inside meeting”. Kwamba je, mkutano wa “ndani” unaweza kufanyika “nje” au kuwa na watu wengine “nje”. Kwa vile alikosa hekima ya kutafuta ushauri alijikuta anatoa amri ambayo kama nitakavyoonesha hapa chini haiikupaswa kutiiwa na yeyote kwa sababu ilikuwa imetolewa kwa makosa. Dhamiri ya mwanadamu iko juu ya amri Kitu ambacho ningependa kukiandika kwa kina kidogo ni kile ambacho naweza kukiita ni “ukuu wa dhamira ya mwanadamu”, yaani the supremacy of human conscious. Kati ya vifaa vyote ambavyo Mwenyezi Mungu ametujalia wanadamu hakuna kilicho cha juu zaidi na ambacho kinatafsiri uanadamu wetu kama dhamiri. Yaani, ile sehemu ya utu wa mwanadamu ambayo inamuamuria wema na uovu, na ambayo inamsukuma kukubali au kukataa. Dhamiri ya mwanadamu ndio dira pekee ya maisha yake na kama dira hii imetengezwa vizuri (well formed), basi humuongoza katika maisha salama licha ya mikwaruzo ya hapa na pale. Dhamiri hufunzwa tangu utotoni kwa mtoto kufundishwa mema na mabaya na kwa kadiri anavyozidi kukua hufundishwa kwa vitendo vya wema na kuepushwa kwa vitendo viovu. Lakini, dhamiri isipoongozwa vyema toka utoto na katika maisha basi mwanadamu huenda akisukumwa kama mnyama akiongozwa na hisia na matukio. Lakini dhamiri hii ikiwa imefundishwa vizuri na kujizoeasha katika kufuata mema basi inajikuta ikitambua uovu na kuukataa. Sasa dhamiri ambayo imefundishwa vizuri kufuata mema haiwezi kulazimishwa kukubali uovu kwa gharama yoyote. Huu ndio ukuu wa dhamira. Watu wameenda katika vifo vyao na wengine katika vifungo vyao vya muda mrefu kwa sababu hawakuwa tayari kusaliti dhamiri zao. Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa unaweza kuwafunga watu gerezani au unaweza kuwatendea watu vibaya ukiamini kuwa kwa kufanya hivyo utawanyamazisha lakini ukweli ni kuwa utawanyamazisha tu kama utaua dhamiri zao. Lakini kama watu hao wanaamini katika ukweli wa dhamiri zao basi hakuna mateso, hakuna jela, hakuna vitendo ambavyo vinaweza kuwafanya wakubali uongo kuwa ukweli, uovu kuwa ni wema na uadui kuwa ni urafiki. Sasa dhamiri ya mwanadamu imeumbwa kutii ukweli, wema na uzuri. Na iko tayari kukataa kutii amri isiyo halali au ambayo inamfanya asiwe kama mwanadamu. Historia ina mifano mingi ya watu ambao walikataa kukubali uovu ili waoneakena vizuri. Kuanzia kwenye maandiko na katika historia wapo watu walioishi na kukataa kuishi pale ambapo dhamiri zao ziliwakataliwa. Mifano ya marafiki wa Nabii Daniel (Meshak, Shedrack na Abednego) iko wazi. Wangeweza kuiabudia sanamu ya mfalme Nebukadneza na wangeishi kwa raha mustarehe. Lakini dhamiri zao ziliwakataliwa. Kina Nelson Mandela na wenzake walikuwa na uwezo wa kukubali makosa madogo na kuomba radhi na kuahidi kuwa hawatafanya tena siasa ili kuepuka kifungo cha maisha. Lakini wote wakitii dhamiri zao (huku wakilipia gharama kubwa kwa familia zao) walikataa uongo na wakawa tayari kwenda jela. Miaka 27! Katika taifa letu bado hatujapata watu ambao wako tayari kutii dhamiri zao kuliko kutii uongo. Tunachokiona sasa hivi wapo watu ambao wameanza kuamka na kudai kutii dhamiri zao kutokana na ukweli uliopo. Kwa mfano CHADEMA wanapoamua kufanya mikutano ya ndani ambayo wanaamini wako sahihi hakuna amri yoyote ambayo inaweza kuwalazimisha kuacha kufanya hivyo hasa kama amri hiyo inatolewa ikiwa na mushkeli. Kifo cha Mwangosi, binafsi ninakiona pia ni ushahidi wa ukuu wa dhamiri ya wanadamu. Mwangosi hakuwa na sababu ya kwenda kuwahoji polisi kwanini wanamshikilia mwandishi wa Nipashe. Angeweza kukaa pembeni na kusubiri wamalizane ili baadaye aulize. Lakini dhamiri yake ilimkatalia. Ilimkatalia kwa sababu aliamini kuwa polisi hawapaswi kukamata waandishi wa habari na hawapaswi kutumia nguvu mahali ambapo hakuna tishio lolote la amani. Kwangu mimi kinyume na wale ambao wanaona mwandishi wa habari aliuawa – ni kuwa uhuru wa dhamiri ya mwanadamu ulikataliwa na watawala. Badala ya kumpa nafasi ya kumsikiliza walianza kumpiga na badala ya kumtuliza kwa kumwelewesha alilipuliwa. Alikuwa anasumbua watawala kwa maswali yake. Alitakiwa kutii tu bila ‘shurti’! Hatupaswi kutii amri ambazo zina hatari kwetu au ni kinyume yetu Hili ni kweli sana, tena sana. Mtu kwa vile ni polisi anavaa nyota nyota na anakuja na kimulimuli, hawezi kuja nyumbani kwako na kukuambia usilale na mwenza wako na wewe ukiwa na akili timamu ukaitikia “ndio afande!” Rais Kikwete pamoja na vyeo vyote alivyonavyo hawezi akaamka asubuhi na kusema simpendi sana Dk. Slaa mkamateni na mumfunge maisha! HAWEZI! Jaji Mkuu hawezi kuamua tu kuwa kwa vile Tundu Lissu amedai wapo majaji vilaza, basi ahukumiwe kwenda jela! Hawawezi kwa sababu hata wakijaribu dhamiri za wanadamu zinapaswa kuwakatalia! Amri uliyo na shaka nayo ihoji Ninachosema ni kuwa usikubali kutii amri ambayo una shaka nayo. Kwa mfano, polisi wa usalama barabarani akikusimamisha kwenye gari lako na kukuambia kuwa uteremke na urudi nyumbani ukitembea kwa vile gari lako amelichukua kwa jina la serikali, ni lazima uhoji. Utakuwa mtu mvivu wa kufikiri kama utaamua kuteremka na kukusanya vitu vyako na kumpatia ufunguo. Hili ni kweli kwa wanasiasa wetu na hasa watu wa CHADEMA. Viongozi wa serikali wakitoa amri ambazo wanaziona zina matatizo kwao na hazina haki ni wajibu wao kukataa kuzitii. Lakini, wasikatae kwa sababu hawazipendi. Kama amri imetolewa kihalali na katika mazingira halali basi ni wajibu wa wale wanaopewa amri hiyo kuitii. Lakini kutii amri halali yenye mazingira halali nako kunakikomo chake hasa kama mfululizo wa amri hizo unalenga kunyima haki za watu. Kwa mfano, kama kila wakati CHADEMA wanaomba kibali kufanya mkutano wanaambbiwa “intelligentsia inaonesha kutakuwa na vurugu” au wanakataliwa wakati watu wengine wanapewa basi ni jukumu la CHADEMA kukataa kutii amri hiyo. Huo ndio ukuu wa dhamiri ya mwanadamu.

KIFO CHA DAUD MWANGOSI CHA MUHUZUNISHA MBUNGE WA IRINGA

Mbunge wa Jimbo la Iringa mjini kupitia CHADEMA mh Peter Msigwa akutana na waandishi wa habari nakuzungumzia kifo cha mwandishi wa habari wa channel ten na mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Iringa Daudi Mwangosi. Mbunge wa Jimbo la Iringa mjini kupitia CHADEMA mh Peter Msigwa akiongea na waandishi wa habari mkoani iringa jana. --- Mbunge wa Jimbo la Iringa mjini kupitia CHADEMA mh Peter Msigwa amesikitishwa kuona viongozi wakuu wa serikali kukaa kimya kutokana na kifo cha mwandishi wa habari wa channel ten na mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Iringa Daudi Mwangosi. Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Msigwa amesema amesikitishwa sana na kifo cha Mwandishi mwangosi kwani hata kilipotokea yeye alikuwa safarini kuelekea Ujerumani lakini kwa kuufahamu mchango mkubwa aliokuwa nao Mwangosi katika kutetea haki kwa wananchi wa Iringa na tasnia ya habari ilimbidi ahairishe ili kuweza kutoa pole kwa familia ya marehemu. Ameeeleza kuwa yeye kama mbunge amesikitishwa sana na kuona viongozi wakuu wanchi kama rais kutozungumzia suala hili na haswa kwa viongozi wa ngazi ya mkoa na wilaya ambao marehemu alikuwa akifanya nao kazi kwa karibu sana. “Nimesikitishwa sana kuona kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa kuzidi kuwepo ofisini kwa lile lilitotokea, mikono ya kamuhanda na mikono ya Said Mwema imejaa damu, na mimi naungana na wanahabari kuugomea uongozi wa RPC Iringa” alisema. Ameongeza kuwa anasikitiswa sana Meya wa manispaa wa Iringa Amani Mamwindi kuhusika katika utoaji wa amri ya kuvunjwa kwa vijiwe vya wananchama wa CHADEMA.“Meya ametoa amri ya kubomoa vijiwe vya chadema akieeza kuwa ni amri ya jiji na kuacha jukumu lake kubwa la kuhakikisha kuwa takataka za mji zinatolewa na kuhakikisha uchumi unaendelea na badala yake kuhusika kubomoa vijiwe vya wanachama pamoja na kutoa bendera na hatutaruhusu hali hii iendelee” aliongeza msigwa. Kuhusu yeye kutoonekana kuwajibika jimboni na kuwa na ziara nyingi za nje Msigwa amesema haendi huko tuu kwa maslahi yake binafsi ila anafanya ili kujifunza mambo mengi ambayo yatakuja kuwasaidia wananchi baadae nahii inatokana na yeye kuwepo katika uongozi wa katika wizara mbalimbali ambapo ziara hizo zina maslahi kwa jamii nzima. Kutokana na hali hiyo mbunge huyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika mkutano utakaofanyika katika eneo la soko kuu kuanzia saa nane kamili na kuongea na wananchi kuhusiana na mambo mengi yanayohusiana na maendeleo ya jimbo

Sunday, September 16, 2012

WANANCHI WAONYESHWA VIWANJA VYAO VILIVYOPIMWA NA KAMPUNI YA ARDHI PLAN

Maafisa wa Kampuni ya Ardhi Plan wakiwa kwenye eneo la ugawaji wa viwanja katika mchoro namba 8 kwenye mtaa wa Namanyigu, wa kwanza kushoto ni Gordwin Pambila na George Kimwaga


Aliyevaa miwani na kofia ni Afisa wa Kampuni ya Ardhi Plan George Kimwaga akitoa maelekezo kwa kutumia ramani kwa wananchi ambao wamemzunguka ili kuweka sawa kumbukumbu za ardhi
Kijana wa Kampuni ya Ardhi Plan akiwa amevaa kizibao chenye nembo ya Kampuni hiyo

Baadhi ya wananchi wakiwa na viongozi wa kamati ya upimaji wakiangalia maeneo husika


Baadhi ya wananchi wakiwa na viongozi wa kamati ya upimaji wakiangalia maeneo husika


Na Stephano Mango, Songea

WANANCHI wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ambao wamepimiwa ardhi yao katika Kata ya Mshangano kwa kutumia Kampuni ya Ardhi Plan wamefurahishwa kukamilika kwa mradi huo wa viwanja elfu 18,000 ulioanza mwaka 2011 na kukamilika septemba mwaka huu

Akizungumza kwa niaba ya kamati ya ugawaji wa viwanja iliyochaguliwa na wananchi wenye maeneo katika Kata ya Mshangano kwenye eneo la ugawaji jana Telesia Komba alisema kuwa kitendo kilichofanywa na Kampuni hiyo ni cha kiungwana sana kwani wameheshimu makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa mwaka jana wakati mradi unaanza

Komba alisema kuwa makubaliano yaliyofikiwa wakati huo kwenye mkutano mkuu wa kata wa kata hiyo kati ya Kampuni, wananchi na viongozi wa Serikali yalikuwa ni kwamba gharama za mradi huo zinatolewa na wananchi wenyewe kwa kutoa ardhi badala ya kusubiri Serikali mpaka ipate uwezo wa kifedha ambapo kwa wale wenye maeneo madogo yaani kiwanja kimoja mpaka viwili wanatozwa gharama ya fedha shilingi laki moja (100,000/=) kwa kiwanja kimoja na laki mbili (200,000) kwa viwanja viwili kama gharama za upimaji na kwa wale wenye viwanja 5 basi viwili wanaipa Kampuni

Alisema kuwa kwa wale ambao wanachelewa kutimiza wajibu wao wa kulipia gharama za upimaji hawataonyeshwa mipaka ya maeneo ya ardhi yao na kukosa nyaraka zitakazowafanya wawe wamiliki halali wa viwanja hivyo mpaka pale watakapotekeleza makubaliano

Alifafanua kuwa wananchi ambao wametimiza makubaliano husika wanaendelea kuonyeshwa maeneo yao ili waweze kuyamiliki kisheria na kuyafanyia shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kadri ya mipango yao wenyewe

Akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Namanyigu Fidolin Malindisa alisema kuwa wananchi wanapaswa kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa ili Kampuni ipate haki yake kwa sababu tayari imeshatimiza wajibu wake wa msingi

Malindisa alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawapa fursa wananchi kuweza kuishi kwenye maeneo yaliyopimwa, pia watatumia maeneo hayo kwa kupata mkopo na kuendesha miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto

Naye Afisa kutoka Kampuni ya Ardhi Plan Gordwin Pambila alisema kuwa Kampuni imeanza kuwaonyesha wananchi viwanja katika mtaa wa Namanyigu ambako kuna madeni madogo ya fedha za gharama za upimaji ambazo zinadaiwa kutoka kwa wananchi

Pambila alisema kuwa wananchi wengi hawajatimiza makubaliano ya kulipia gharama za upimaji hivyo ndio wanaochelewesha ukamilishaji wa mradi huo na kuifanya Kampuni itumie muda mwingi na rasilimali nyingi kuwakumbusha kulipia maeneo hayo
MWISHO

Friday, September 14, 2012

HOFU YA KUTAKA KUMUUA MUFTI SIMBA YATANDA


• Waziri amng’oa kigogo NECTA kumlinda Ndalichako


na Waandishi wetu

WAKATI baadhi ya Waislam wakipanga kuandamana kuvamia ofisi ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Issa Bin Shaaban Simba, hofu ya kutaka kuuawa kwa kiongozi huyo wa dini imetanda nchini.

Kutokana na tishi hilo, Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kwa kundi lolote la Kiislamu lililopanga njama za kuvamia ofisi ya Mufti leo kwa lengo la kumdhuru na kumuondoa madarakani.

Habari zinasema kuwa kundi hilo limepanga kufanya maandamano bila kibali na kuibukia katika ofisi za Bakwata kwa lengo la kumng’oa Mufti Simba.

Akizungumzia tishio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema kuwa polisi wamechukua hatua mbalimbali kukabiliana na kundi linalotaka kuvamia ofisi za (BAKWATA) na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) na tayari washukiwa wawili kati ya kumi wamekamatwa kwa mahojiano.

Kamanda Kova alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kupokea malalamiko kutoka Bakwata na kufungua jalada la kesi dhidi ya kundi lenye lengo la kutumia nguvu na mabavu hali inayoashiria uvunjifu wa amani.

Kova alisema kuwa ni jukumu la serikali kupitia vyombo vya dola kuhakikisha uwepo wa usalama wa taasisi yoyote iliyosajiliwa kisheria.

“Ni wajibu wetu kuwalinda viongozi walioko madarakani mpaka pale taratibu za kiutawala na Kikatiba zitakapowaondoa madarakani,” alisema Kova.

Pia Kova aliwasihi wananchi na wafuasi wa makundi hayo kutofuata mkumbo katika kutekeleza azma hiyo na kueleza kuwa jeshi hilo haliwalindi Bakwata pekee, bali viongozi wote na yeyote anayetaka kumuondoa kiongozi madarakani aende mahakamani au afuate taratibu na kanuni za taasisi husika.

Hivi karibuni Mufti alinukuliwa na gazeti moja la kila siku akieleza kuwapo kwa kundi la wanaojiita Waislamu lenye lengo la kumuondoa madarakani na kusema kuwa yeye yupo kisheria na kwamba kundi hilo haliwezi kumuondoa kwani Waislamu si wa Dar es Salaam pekee.

Katika hatua nyingine, serikali imelazimika kumfukuza kazi Mkuu wa Idara ya Utafiti, Tathmini na Huduma za Kompyuta wa Baraza la Mtihani, Joseph Mbowe, kwa madai ya uzembe uliosababisha kurudiwa kwa mtihani wa Maarifa ya Kiislam.

Hatua hiyo imekuja takriban wiki moja imepita tangu maandamano ya Waislamu kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani kufanikisha kuachiwa huru kwa wenzao waliokamatwa kwa sababu ya kususia sensa ambapo pamoja na mambo mengine, wiki hii walitishia kufanya maandamano kwenda kumng’oa Ndalichako na Mufti Simba.

Akitangaza kusimamishwa kazi kwa Mbowe, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema jana kuwa hatua hiyo imetokana na mapendekezo ya kamati ya wataalamu mbalimbali waliochunguza chanzo cha malalamiko ya kufeli kwa wanafunzi wa Kiislam waliofanya mtihani huo mwaka jana.

Kwa mujibu wa Mulugo, kamati hiyo ilibaini pasi na shaka kwamba tatizo la usahihishaji wa mtihani huo lilitokana na kasoro za kiutendaji na kiufundi na si vinginevyo, hivyo kupendekeza kuwajibishwa kwa mkuu wa kitengo cha kompyuta.

Alisema kamati hiyo ilihusisha wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (kwa kuwa Necta ni taasisi ya Muungano) na Islamic Education Panel.

Wataalamu wengine walitoka Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislam, Idara ya Usalama wa Taifa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa).

“Kamati ilipewa hadidu nane za rejea ikiwemo kupitia orodha ya wasahihishaji wa somo la Maarifa ya Kiislam kubainisi sifa zao, kupitia maoni yao na sampuli za karatasi za majibu ya watahiniwa ili kujiridhisha na usahihishaji wake.

“Kamati hiyo iliyoteuliwa na Waziri wa Elimu iliwataka wajumbe hao kulinganisha mchakato wa usahihishaji wa mwaka 2012 na miaka iliyopita, kuwahoji baadhi ya watendaji wa Necta waliohusika na ukokotoaji wa mtihani huo na kupendekeza nini kifanyike,” alisema naibu waziri huyo.

Alisema kamati iligundua kwamba tatizo la usahihishaji wa mtihani kwa kutumia kompyuta ulihusisha karatasi tatu za majibu badala ya mbili, hivyo kusababisha watahiniwa wote kupata alama za chini.

Mulugo alisema kamati iliona kwamba mfumo wa usahihishaji kwa kutumia kompyuta haukufanyiwa majaribio ili kujiridhisha huku ikiridhishwa na utendaji bora wa Necta hasa kwa kuandaa na kusahihisha mitihani.

Awali aliwaomba radhi watahiniwa wote kwa usumbufu uliojitokeza huku akiahidi kutorudiwa tena kwa kasoro hizo na kusisitiza kwamba licha ya kusimamishwa kazi, Mbowe atachukuliwa hatua zaidi za kiutendaji.

Kabla ya kuchukuliwa kwa hatua hizo, wizara ilipokea malalamiko kutoka kwa wakuu wa shule za Kiislam, hivyo aliwaomba wote kukubaliana na hatua zilizochukuliwa.


Chanzo Tanzania Daima

Tuesday, September 11, 2012

VIONGOZI WA RUVUMA PRESS CLUB WAJIFICHA MAFICHONI KUTOKANA NA MAANDAMANO


KATIBU WA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA RUVUMA( RUVUMA PRESS CLUB) AMBAYE PIA NA KATIBU WA MBUNGE WA JIMBO LA SONGEA MJINI DKT EMMANUEL NCHIMBI) ANDREW CHATWANGA

Na Stephano Mango, Songea

MGOGORO mkubwa umeibika kwa waandishi wa habari mkoani Ruvuma baada ya Viongozi wa chama cha waandishi wa habari mkoani humo kutoitisha maandamano na kuingia mafichoni kwa muda ili kuepusha kufanyika maandamano ya kuunga mkono maombolezo ya kifo cha mwandishi wa habari na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Iringa Daud Mwangosi aliyefariki kwa kupigwa na mlipuko uliosababishwa na polisi katika kijiji cha Nyololo mkoani Iringa.

Mgogoro huo umewagawa waandishi wa habari na kuwafanya baadhi ya waandishi kutishia kujitoa nafasi zao za uongozi na uanachama katika umoja huo kwa sababu ya kutokuwa na imani na viongozi wao ambao wanaonekana kufanya kazi kutokana na maslahi ya kisiasa.

Waandishi wa habari mkoani Ruvuma walianza kwa kushangazwa na hatua ya viongozi wa ngazi ya juu ya chama hicho kutowajulisha muda na njia zitakazotumika kwa maandamano hayo hadi pale kwa njia ya simu na baadhi ya waandishi wa habari ambao walishapanga waandamane saa 10. Jioni baada ya kujihakikishia kuwa viongozi wao wamewatosa na hawana ajenda muhimu ya kupinga maandamano hayo kwa hula.

Awali baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari ambao ni wanachama wa chama cha waandishi wa habari mkoani humo (RPC) walijikusanya pamoja na kufuatilia matangazo ya vyombo mbali mbali vya habari yaliyokuwa yakiendelea huku wakiangalia baadhi ya picha zilizopigwa wakati na baada ya kifo cha mwandishi huyo wa habari ambaye alipatwa na mauti wakati akiwa kazini na walipanga wandamane saa 10 jioni muda ambao ndio Marehemu Mwangosi aliuawa kinyama kupigwa na bomu na Polisi.

Katibu Msaidizi wa Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Ruvuma , Julius Konala, alionyesha ushirikiano mkubwa kwa wanachama ambao muda wote walikuwa wanadai ratiba na hatua iliyofikiwa na viongozi wa chama hicho kwaajili ya maandamano na kuwajulisha kuwa viongozi wake hawajulikani waliko na wanapinga kufanyika kwa mnaandamano hayo.

“Jamani mimi mtanionea tuu, Mwenyekiti na katibu wamesema kuwa UTPC imeyasimamisha maandamano yetu bila kutaja sababu,” alisema Konala ambaye alichukua hatua ya kuwasiliana na viongozi wa Polisi mkoani hapa waliotaka kujua ni njia zipi zitakazotumika katika maandamano hayo ili walete askari wa kuyalinda maandamano hayo ya amani.

Tukio hilo limewakasirisha sana viongozi wa Chama hicho na kulazimika kuitisha mkutano wa dharura kwa baadhi ya wanachama wengi wao wakiwa ni mamluki na kusababisha viongozi hao kuomba radhi kwamba wamekosa mawasiliano nao na baadhi ya wanachama wametishia kujiuzulu akiwemo Katibu msaidizi Julius Konala kwa madai kwamba chama hicho kimeingiliwa na mikono ya wanasiasa.

“Naona mbele yangu kuna wingu kubwa na zito ambalo mwisho wake siujui, nafikiria kujiuzulu uongozi na kujitoa katika chama, “ alisema Konala.

Baadhi ya wadau wa habari mkoani humo wameonesha kushangazwa na ukimya wa wanahabari wa mkoa huo licha ya wanahabari wote nchini wakionekana kwenye runinga wakiandamana kupinga ukatili huo uliofanywa dhidi ya Mwandishi wa habari akiwa kazini.

Hata hivyo Mkurugenzi wa muungano wa Vyama vya waandishi wa habari nchini UTPC Abubakar Karsan akiongea na Tanzania Daima kwa njia ya Simu amekanusha vikali kuzuia maandamano bali wao waliyabariki na ndio maana walijumuika na waandishi wengine nchini na kutoa matamko mbalimbali katika viwanja vya Jangwani Jijini Dar es Salaam na kwamba wao walitoa maelekezo kwa Ruvuma Press Club kuungana na Press Club zingine nchi kufanikisha maandamano ya amani ambayo yameitishwa kiuhalali.
Mwisho

Sunday, September 9, 2012

TUME YA KATIBA YATOA WITO KWA WANAWAKE MKOANI RUVUMA


Mwenyekiti wa Tume ya kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba Jaji Joseph Walioba akizungumza jambo, wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa kundi la tano la Tume ya mabadiliko ya katiba Profesa Mwesiga Baregu

Na Stephano Mango, Songea

WANAWAKE mkoani Ruvuma wametakiwa kuhamasishana kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya Tume ya kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba ili waweze kutoa maoni yao kuhusu changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika jamii zao

Wito huo umetolewa jana na Mwenyekiti wa kundi la tano la Tume ya mabadiliko ya katiba Profesa Mwesiga Baregu kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa hotel ya Seedfarm Villa mjini Songea

Profesa Baregu alisema kuwa kumekuwepo na idadi isiyoridhisha ya wanawake wanaohudhuria katika mikutano ya Tume kulinganisha na idadi ya wanawake waliopo kwenye kata hizo kwani takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watu 8,915 waliojitokeza kuhudhuria mikutano ya Tume katika wilaya ya Namtumbo na Tunduru wanawake ni 1,949 tu ambao ni sawa na asilimia 21.9 ya mahudhuria

“ Hii ni idadi ndogo sana kwa akina mama kujitokeza kwenye mikutano hiyo muhimu kwa mustakabari wa wananchi na nchi kiujumla, hivyo Tume inawajibika kutoa wito ili waweze kujitokeza kwa wingi na kuchangia kutoa maoni yao kwa uwazi”alisema Profesa Baregu

Alifafanua kuwa pia kumekuwepo na idadi ndogo sana ya wanawake wanaojitokeza kutoa maoni katika mikutano ya Tume ukilinganisha na uwingi wao kwenye kata mbalimbali kwani takwimu tulizonazo katika Wilaya ya Tunduru na Namtumbo wananchi waliotoa maoni kwa njia mbalimbali ni 2,074 ambapo wanawake ni 198 tu idadi hiyo ni ndogo kulinanisha na wanawake 1,949 ambao wamehudhuria mikutano hiyo

Alieleza changamoto nyingine waliyokutana nayo ni idadi ndogo ya wananchi wanaochangia maoni ya mabadiliko ya katiba kwa njia ya kuongea au kwa kuandika kwani takwimu zinaonyesha kuwa katika wananchi 8,915 waliohudhuria mikutano mbalimbali waliochangia ni 2,074 sawa na asilimia 23.3 ya waliohudhuria

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba Jaji Joseph Walioba alisema kuwa wananchi wengi wanaojitokeza kwenye mikutano ya Tume wamekuwa wakilalamika kwamba hawaielewi katiba iliyopo hivyo itakuwa vigumu wao kuchangia na kutoa maoni yao lakini mwananchi huyo anapoanza kutoa maoni yake anaeleza mambo ya msingi yanayohusiana na katiba
Jaji Walioba alieleza kuwa katika mkoa wa Ruvuma Tume inatarajia kufanya mikutano 72 katika jumla ya kata 72 zilizopo kwenye wilaya tano za mkoa wa Ruvuma ikiwemo wilaya ya Nyasa, Namtumbo, Mbinga, Tunduru na Songea
MWISHO

Saturday, September 8, 2012

WAZIRI LWENGE AICHARUKIA KAMPUNI YA PROGRESSIVE


Na, Steven Augustino, Tunduru

SERIKALI imetoa nafasi ya mwisho ya matazamio kwa Mkandarasi anayejenga kwa kiwango cha Lami Barabara ya kutoka Namtumbo kwenda Tunduru yenye urefu wa zaidi ya Kilometa 188 zitakazo ghalimu zaidi ya shilingi Bilioni. 180.66 huku ikiahidi kuchukua hatua kali kwa mkandarasi huyo kampuni ya progressive Constraction

Kauli hiyo iliyo onesha kuwa mkuki mkali kwa viongozi wa kampuni hiyo ilitolewa na Naibu waziri wa Ujenzi Eng. Gerson Lwenge wakati akiongea katika majumuisho katika Ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Tunduru baada ya kukamilisha ziara yake ya kikazi Mkoani Ruvuma na kuongea na wakandarasi wa kamuni hiyo ambapo pamoja na mambo mengine alionesha kushangazwa na kusuasua kwa mradi hio.

,,Uvumilivu wa Serikali kwa kampuni yenu umefikia kikomo na hatuendelea kuwa wazembe wa kuzibeba kampuni za aina hiyo ambayo hadi sasa imetimiza miezi 18 kazini bila kuonesha uhai wowote,, alisema kwa ukali Eng. Lwenge na kuongeza kuwa hali hiyo imetokana na kujionea ubabaishaji huo na ajaridhika na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo na kwamba Serikali itachukua hatua dhidi ya Mkandarasi na Msimamizi wa Kampuni hiyo.

Aidha Eng. Lwenge baada ya kukerwa na hali hiyo aliwaahidi wanachi wa Wilaya ya Tunduru kuwa atapeleka kero iliyosababishwa na kampuni hiyo katika vikao vyenye maamuzi ili kuangalia utaratibu wa kukatisha mkataba wao.

Alisema kuwa kampuni ya Progressive Constraction ilisaini mkataba wa kukamirisha mradi huo katika kipindi cha miezi 27 iwe imekamilisha ujenzi wake lakini hadi sasa takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi chote hicho kazi zilizofanyika ni uwiano wa asilimia 4% tu za ujenzi wa Mradi huo hali inayo onesha kuwa ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati wa miezi 9 iliyobakia inahitajika kufanyika miujiza.

Alisema mradi huo uliogawanywa katika vipande vitatu na kuainisha thamani zake ni Tunduru Matemanga Kilometa 58.70 Shilingi Bilioni. 63.41 kilipangwa kukabidhiwa mwezi Julai 2013, Matemanga Kilimasera kilometa 68.20 chenye thamani ya Shilingi Bilioni. 64.02 kilipangwa kukabidhiwa mwezi Mei 2013 na Kilimasera Namtumbo Kilometa 60.70 Chenye thamani ya Shilingi Bilioni.53.23 kilipangwa kukamilika mwezi machi 2013.

Aidha Eng. Lwenge pia alitumia nafasi hiyo kuzipongeza Kampuni za SOGEA SATOM anaejenga Bara bara za Songea - Namtumbo kilometa 67.00 utakao ghalimu Shilingi Bilioni.62.88 na … inayojenga Barabara ya Peramiho - Mbinga kilometa 78.00 wenye thamani ya shilingi Bilioni.79.81 kuwa inaendelea vizuri na akaongeza kwa kuonesha mashaka ya mdororo wa ujenzi wa Barabara ya Tunduru - Namtumbo kuwa huenda mradi huo ukapitwa na miradi mipya ya Barabara za Tunduru Mtambaswala Kilometa 202.5, Shilingi Bilioni.240.858 na Mbinga - Mbambabey kilometa 66.00 utakao ghalimu shilingi Bilioni.2.90.

Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya Wilaya ya Tunduru kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Chande Nalicho, Afisa Tawala wa wilaya hiyo Martin Mulwafu pamoja na kueleza changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiikabili Wilaya hiyo wakati wa kutekeleza miradi ya Barabara na Ujenzi alisema kuwa halmashauri hiyo imepanga kutumia jumla ya shilingi 1,097,920,000/.

Alisema fedha hizo zilizopangwa kwa ajili ya kufanya matengenezo ya maeneo korofi katika barabara za Changarawe,vumbi na kilo meta 3 za Lami nyepesi, kujenga madaraja kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara za Tunduru mjini Tsh.675,780 Milioni zitatolewa na mfuko wa barabara, Tsh.428.000 Milioni zitatolewa na mpango wa kuzipatia ruzuku serikali za mitaa (LGCDG) na (CDG).

Akiongea kwa niaba ya wajumbe walioshirika katika mazungumzo hayo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mustafa Bora aliwataka Mawaziri kumsaidia Rais katika utekelezaji wa majukumu yao ili kukifanya chama chake kutimiza ahadi zilizopangwa kutekelezwa katika ilani yake ya mwaka 2010-2015 huku Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Ephraem Ole Nguyaine akimaliza kwa kuwa kumbusha na kuwa karibisha Viongozi wa Kitaifa kutembelea Tunduru iliyopo pembezoni ili kutoa msukumo na kuwaondoa wananchi dhana waliyo ijenga kuwa viongozi wao wamekuwa wakifika nyakati za kampeni tu.

Akiongea kwa niaba ya Kampuni hiyo, Meneja mshauri wa kampuni ya Progressive Constraction Marid Poli pamoja na kueleza changamoto lukuki zikiwemo za kampuni kutokuwa na wataalamu na watumishi wakutosha ndio kikwazo kwa kampuni kutekeleza wajibu wake. aliiomba Serikali kutokatisha mkataba huo na kuahidi kuwa kazi hiyo itaisha kwa wakati na kwamba tayali wamekwisha jipanga kuhakikisha kuwa shughuli zote zinakwisha katika kipindi cha miezi 9 iliyobakia.

Akiwa Ruvuma Eng, Lwenge alianza kwa kutembelea kivuko cha Mto Luhuhu mpakani mwa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na Ludewa iliyopo mkoa wa Njombe ambako alisema kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kuhakikisha inajenga Daraja na bwawa litakalosaidia kilimo cha katika mto huo.
Mwisho

SANGA ONE AWAOMBA WADAU KUMUOMBEA KATIKA KINYAN'GANYIRO


Mgombea nafasi ya Uwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Diwani Mstaafu wa Kata ya Bombambili Golden Sanga( Sanga One)Ni mdau mzuri wa mtandao huu na pia ni mdau muhimu wa masuala mbalimbali ya kimichezo na kisiasa hapa mkoani Ruvuma

Kwani amewahi kuwa Diwani na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Halmashauri ya Manispaa ya Songea ( SUFA) kwa muda usiozidi miaka 5

anawaombeni wadau wote wa mtandao huu kumuombea katika kinyanganyiro hicho cha kuwania Uwenyekiti wa ccm Songea Mjini

Dua zenu ndio mafanikio yake, Tumuombee na kumshauri pia

Kila la heri Sanga One, kila la heri

Thursday, September 6, 2012

TENDWA ANACHEZA NGOMA ASIYOIJUA

KAMA kawaida yake, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, jana aliibuka mbele ya waandishi wa habari akizungumzia mauaji ya mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi, aliyeuawa na Jeshi la Polisi juzi mkoani Iringa wakati akitimiza majukumu yake.

Tendwa ambaye ni mlezi wa vyama vya siasa mwenye jukumu la kuvisimamia, kuvishauri na kuhakikisha vinatendewa haki na kufanya shughuli zao katika mazingira sawa ya ushindani, alitumia muda mwingi kutupa lawama kwa chama cha CHADEMA kuhusu vurugu hizo.

Katika kuonesha kuwa Tendwa anacheza ngoma asiyoijua mdundo wake, alitumia muda mwingi kurejea hadithi zake za vitisho vya kuifutia usajili CHADEMA, akidai kushangazwa na operesheni zake mikoani wakati huu ambapo hakuna uchaguzi.

Kwanza, tunampongeza Tendwa kwa kujitokeza hadharani na kuzungumza hicho alichoona kinampendeza yeye na wale waliomteua, maana pamoja na kuchelewa kutoa maonyo hayo kwa polisi na CHADEMA, bado ameendelea kudhihirisha kuwa hatambui wajibu wake.

Tunasema hivyo kwa ushahidi kuwa kazi ya ofisi yake haionekani kuvisaidia vyama vya siasa, hasa vya upinzani na badala yake Tendwa amekuwa kinara wa kuvitisha na kutosikiliza malalamiko yao.

Mathalani katika vurugu zilizozushwa na polisi kwenye maandamano ya CHADEMA mkoani Arusha Januari 5, mwaka jana, kisha mkoani Mwanza, Msajili huyu hakuonekana kusema lolote hadi Rais Jakaya Kikwete alipohutubia taifa na kuwatisha CHADEMA ndipo kesho yake naye akaibuka na vitisho.

Kama hiyo haitoshi, katika uchaguzi mdogo wa Igunga ambao matokeo yake yametenguliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, miongoni mwa mambo yaliyomuengua Dk. Dalali Kafumu, yalilalamikiwa sana na wapinzani kwenye kampeni kuwa CCM inacheza rafu lakini Tenda alikaa kimya na matokeo yake yameonekana.

Ni Tendwa huyu aliyeibuka kwenye kampeni za uchaguzi mdogo Arumeru Mashariki na kuwatisha CHADEMA kuwa wasimtumie aliyekuwa mbunge wao wa Arusha Mjini, Godbless Lema, katika kampeni hizo akidai wazee wa jamii ya Kishiri walimwambia watamdhuru.

Tunachelea kuamini kuwa ikiwa Msajili mwenye jukumu la kusimamia amani na utulivu anapofikia hatua ya kuzua uongo kama huo, tena kipindi cha uchaguzi halafu akashindwa kuthibitisha madai ya kauli zake, leo tutamshaangaje akiibuka na kuwasingizia CHADEMA kwa lolote ilhali ukweli wa vurugu za kisiasa unajulikana?

Ofisi ya Tendwa imezuia vyama kufanya shughuli za kisiasa kama mikutano na maandamano wakati huu wa sensa na vyama vyote vimetii lakini CCM inaendelea na mchakato wa uchaguzi wake wa ndani kwa wagombea kuchukua na kurudisha fomu kwa maandamano bila kuonywa, ila CHADEMA wanaofungua tawi wanatishiwa kufutwa kuwa wanachochea vurugu.

Tangu kuanza tena kwa mfumo wa vyama vingi nchini, Ofisi ya Msajili imekuwa na kasoro nyingi sana katika ustawi wa demokrasia ya upinzani, maana hata mtangulizi wa Tendwa, Jaji George Lindi, naye alipwaya ingawa huyu wa sasa amezidisha ushabiki kiasi cha kujikuta akicheza ngoma asiyoijua.


Chanzo TAHARIRI, Tanzania Daima, Septemba 6,2012

Wednesday, September 5, 2012

WATOTO WANNE WA FAMILIA MOJA WATEKETEA KWA MOTO



Na Agustino Chindiye, Tunduru

MAJONZI na simanzi vyatawala katika mji wa Tunduru na viunga vyake vyake kutoka na msiba wa kusikitisha wa watoto wanne wa familia moja ambao wamefariki dunia baada ya miili yao kuteketea kwa kuunguzwa kwa moto uliozuka katika chumba walicho kuwa wanalala.

Kufuatia hali hiyo Mama yao Mzazi Asha Hamadi aliyedaiwa kuacha Mshumaa ukiwaka na kuwafungia watoto hao amelazwa katika Hospitali ya serikali ya Wilaya ya Tunduru akiwa hajitambui kutokana na kuugua ugonjwa wa moyo.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa chanzo cha moto huo ni mshumaa ambao uliachwa ukiwa unawaka huku wazazi wao wakiwa wamewafungia kwa nje na kulala chumbani kwao.

Watoto hao ambao ni marehemu kutoka katika familia ya Kipemba walitambuliwa kwa majina ya Harid Nasoro (7),Hamid Nasoro (5)Ally Nasoro(4) na Alkam Nasoro(3).

Akizungumzia tukio hilo Baba wa Marehemu hao Nasoro Hamadi alidai kuwa Watoto wake walipatwa na mkasa huo baada ya kufungiwa kwa nje na mama yao mzazi Asha Hamadi kutokana na kilichodaiwa kuwa walifanya hivyo ili kuwadhibiti wasitoke nje kutokana na utundu walio kuwa nao.

Alisema chanzo cha kuamua kulala na mshumaa huo kilitokana na watoto hao kuzowea kulala na mwanga huku siku hiyo umeme ulizima baada ya Luku yake kwisha huku kukiwa na zuio la wateja wa huduma hiyo kutoluhusiwa kununua Umene kupitia huduma za Simu, M-pesa, Nmb Mobile kama ilivyo kuwa imezoeleka.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeki amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo ambapo pia alisema kuwa Polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo

Kwa mujibu wa taarifa ya Mganga aliyezifanyia uchunguzi miili ya marehemu hao Dkt. Moses Nwahasunga amesema kuwa chanzo cha vifo hivyo kilitokana na miili yao kukosa hewa safi na kuungua vibaya baada ya moto huo kulipuka ndani ya chumba.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Chande Nalicho ametuma salamu za rambirambi na kuitaka familia hiyo kuwa na subira wakati huu wa majonzi makubwa yaliyowakuta.

Msiba huo ambao uliwasisimua watu wengi na kuzusha simanzi na vilio kila kona ya mji wa Tunduru Miili ya watoto hao imezikwa katika makabuli yalipo katika mtaa wa Mabatini mjini

Mwisho

Saturday, September 1, 2012

TANGAZO LA KULIPIA GHARAMA ZA UPIMAJI WA VIWANJA MSHANGANO

MKURUGENZI MTENDAJI WA KAMPUNI YA ARDHI PLAN GOMBO SAMANDITO ANAWATANGAZIA WANANCHI WOTE WALIOPIMIWA MASHAMBA( VIWANJA) KATIKA MITAA YA MSHANGANO, MITENDEWAWA NA NAMANYIGU KATIKA KATA YA MSHANGANO HALMASHAURI YA MANISPAA YA SONGEA KUWA WANATAKIWA KWENDA KULIPIA GHARAMA ZA UPIMAJI ILI HATUA ZA UMILIKISHAJI ZIFANYIKE KAMA MAKUBALIANAO YA AWALI WAKATI MRADI UNAANZA YALIVYOFIKIWA MWAKA 2011, SIKU AMBAZO ZILIKUBALIWA KUWA NI MWISHO WA ULIPAJI WAKATI WA MKUTANO WA HADHARA ULIOFANYIKA KATIKA MTAA WA NAMANYIGU NA MSHANGANO NA KUHUDHURIWA NA VIONGOZI MBALIMBALI AGOSTI 18 MWAKA HUU ZINAKARIBIA KWISHA KWANI ILIPENDEKEZWA KUWA SEPTEMBA 3 MWAKA HUU WALIOLIPIA GHARAMA KUSUDIWA NDIO WAONYESHWE HIVYO NI VEMA KWA WALE WASIOLIPIA WAKAJA KULIPIA HARAKA ILI KUONDOA MIGONGANO YA MAWAZO HUKO MBELE KWANI KAMPUNI HAITAHUSIKA NA USUMBUFU UTAKAOJITOKEZA KWA MAELEZO ZAIDI KUHUSU ULIPAJI PIGA SIMU 0756368522 AU 0654629090 AU FIKA KATIKA OFISI ZA KAMPUNI YA ARDHI PLAN ZILIZOPO VARONGO INTERNET CAFE ZILIZOPO JILANI NA BENK YA NMB KAMPUNI INAOMBA YOYOTE ATAKAYESOMA TANGAZO HILI AMJULISHE NA MWENZIE