Na Joseph Mwambije,Songea
VIJANA wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) Mkoani Ruvuma wamekitaka Chama hicho kurejesha nguvu iliyokuwa nayo miaka ya 70 enzi ya Mwalimu Nyerere ya kuwachukulia hatua Viongozi wa Serikali wanaojihusisha na ufisadi vinginevyo watakihama na kwenda Upinzani.
Walitishia kukihama Chama hicho hivi karibuni kwenye Mkutano ulioitishwa kwa ajili ya kupata maoni yao ya namna ya kurejesha heshima yake na kujua kwa nini Vijana wanakichukia Chama hicho kilichoshika dola.
Walitoa kauli za kukitahadharisha Chama hicho mbele ya wajumbe wawili wa Baraza la vijana wa CCM Taifa ambao pia ni wajumbe wa kamati ya watu nane inayozunguka Nchi nzima kuchukua maoni ya vijana na kuyafanyia kazi kwa lengo la kurejesha heshima ya Chama hicho.
Mmoja wa Vijana hao ambaye anatoka kwenye kundi la vijana wasomi Razalo Komba alisema shida kubwa inayokipata Chama hicho inatokana namna ya watendaji wabovu wa Serikali ambao wanatumia vibaya madaraka yao ndani ya Serikali na kuwatendea vibaya wananchi.
Alisema kuwa wapinzani wameijengea chuki inayotokana na Viongozi wa juu wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wao na kufanya mambo kana kwamba hakuna utawala wa sheria hivyo wanajiona wao ni Miungu watu wanaoweza kufanya chochote bila kuguswa.
‘Kwa jinsi mambo yanavyokwenda inaonyesha dhahiri kwamba CCM haiwapendi wasomi na udhaifu huo wapinzani wameutumia na kuwateka wasomi na hivi sasa inaungwa mkono na wasomi wengi ambao wana uzalendo na Nchi yao ambao wanaona mambo yanakwenda ndivyo sivyo,kama mambo yatakwenda hivi yanavyokwenda hata mimi nitahamia Upinzani’alisema.
Kijana mwingine Amoni Mtega alisema Chama hicho kimepoteza mvuto mbele ya watu kwa kuwa kinashindwa kujibu hoja za Wapinzani hivyo akakitaka kujibu hoja hizo tena kwa wakati huku akisisitiza kwamba kwa kushindwa kuzijibu hoja hata kama ni za uongo wananchi wanayaaamini yanayosemwa.
Alisema kuwa vijana wamedharauliwa na kunyimwa fursa za maendeleo na ndio sababu wanakimbilia kwenye vyama vya upinzani ambavyo wanaviona kuwa mkombozi wao mpya badala ya Chama cha CCM.
Akizungumza mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo Joseph Mkilikiti alisema maoni hayo watayafikisha kwenye Baraza kuu Taifa ambalo litapeleka kwenye uongozi wa juu wa Chama hicho ili yaweze kufanyiwa kazi.
Mkutano huo ulitonosha vidonda vya makundi ya uchaguzi wa mwaka jana kati ya kambi za Oliver Mhaiki na ya Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emanuel Nchimbi baada ya Vijana wa kambi ya Nchimbi ambao walitokea upinzani kumsifia Mbunge huyo na kumponda Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa CCM Songea Mjini Vikta Ngonyani ambaye hakuwa kambi ya Mbunge huyo kwamba hajasoma,hafanyi ziara kuwatembelea vijana na kwamba hawezi kukabiliana na siasa za sasa.
Akifunga mkutano huo huku akionekana kujibu hoja za vijana hao Mwenyekiti huyo wa vijana wa CCM Songea mjini alisema kuwa inashangazwa na maneno ya vijana hao kuwa bado hawajui taratibu za chama hicho kwani waliingia na kukuta ziara zimeshafanyika hivyo amewataka watulie iliwajifunze na siku zijazo watapata uongozi ndani ya chama hicho.
Alisema vijana hao ndio waliosababishan CCM kupoteza Kata tano za Mjini kwa kuwa Mbunge alikuwa akiwatumia kufanya kampeni na badala ya kuomba kura wao walikuwa wakiwatukana wapiga kura hivyo wapiga kura waliwaadhibu kwa kuwachagua madiwani wa CHADEMA.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment