Na Joseph Mwambije,Songea
MGODI wa Makaa ya mawe wa Ngaka uliopo katika kijiji cha Ruanda , wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma utaanza kuzalisha Umeme kiasi cha megawatts 120 katika kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa baada ya Kampuni ya TANCOAL Energy inayomiliki Mgodi huo kupata leseni ya biashara hiyo.
Shughuli za uchimbaji wa Makaa ya Mawe zilizozinduliwa rasmi hivi karibuni na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Cyril Chami aliyeambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa NDC Dkt.Chrisant Mzindakaya.
Mgodi huo wa Makaa ya mawe wa Ngaka, unamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania yenye asilimia 30, na kampuni ya Intra Energy ya Australia yenye hisa asilimia 70.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri huyo wa Viwanda na Biashara alisema mradi huo utaleta ukombozi mkubwa kwa Tanzania ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosekana kwa nishati ya umeme wa kutosha.
“Ukikosa umeme maana yake viwanda haviwezi kufanya kazi, ajira zinapungua, wafanyabiashara wanaathirika na shughuli zingine za uzalishaji mali zinakwama” Alisema Dkt Chami.
Aidha Waziri huyo aliongeza kuwa Wizara yake itaunga mkono juhudi za kufanikisha mradi huo kwa kuwa inaamini utakua mkombozi wa Taifa katika kipindi kifupi kijacho.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TANCOAL Energy Bw. Graeme Robertson alisema kwa sasa mradi huo unazalisha tani 30,000 za makaa ya mawe kwa mwezi sawa na tani 360,000 kwa mwaka ambazo huzisambaza katika viwanda vya hapa nchini ikiwemo viwanda vya saruji vya Mbeya na Tanga.
Bw. Robertson alisema kwa kuanzia TANCOAL Energy itazalisha megawatts 120 za umeme katika kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa, lakini uzalishaji huo utakua ukiongezeka hadi kufikia megawatts 2,000 kwa kuwa eneo hilo la Ngaka lina hifadhi kubwa ya makaa ya mawe inayozidi tani milioni 250 na kwamba utafiti unaoendelea unaonesha eneo hilo linaweza kuwa na hifadhi kubwa zaidi.
Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa Mradi huo kampuni hiyo licha ya kuinufaisha Tanzania kwa nishati ya kutosha ya umeme, pia itahakikisha inaisaidia jamii kwa kutoa ajira na kununua bidhaa za kilimo zinazozalishwa na wananchi
Naye Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa NDC Dkt. Mzindakaya aliwaondoa shaka watanzania, akisema mradi huo una manufaa makubwa zaidi kwa Tanzania kuliko kwa mwekezaji.
Alisema kuwa Tanzania pamoja na kunufaika na umiliki wa kampuni ya TANCOAL Energy kwa asilimia 30 pia itanufaika na matokeo ya kuwepo kwa umeme wa kutosha ambao utaihakikishia ustawi wa viwanda, biashara na kilimo.
Mzindakaya pia alisema haina sababu kwa Taifa kulaumiana kwa kuchelewa kuitumia rasilimali hiyo na badala yake viongozi wachukue hatua ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mbunge huyo Mstaafu aliongeza kuwa wapo baadhi ya wanasiasa ambao wamekua wakinung’unika na kulaumu wakati wao wenyewe hawachukui hatua zozote za kuwasaidia wananchi.
“Hata huu mradi sio watu wote watauunga mkono, wapo watakaoupinga lakini sisi NDC tutasonga mbele” Alitamba Dkt Mzindakaya na kuongeza kuwa NDC na bodi yake hawawezi kuingia mkataba wa kijinga.
Katika hatua nyingine Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Chami amekanusha vikali uvumi ulioenezwa kuwa Mradi wa Makaa ya mawe wa Ngaka unapanga kujenga mitambo ya kuzalisha umeme katika wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya badala ya Mbinga Mkoani Ruvuma.
Chami alisema uvumi huo hauna ukweli wowote na kwamba, mitambo hiyo itajengwa katika makutano ya Mto Ruhuhu na Mto Ngaka yaliyopo jirani na yanapochimbwa makaa hayo wilayani Mbinga.
Pamoja na kuzindua uchimbaji wa makaa hayo ya mawe alisema pia alikabidhi vyeti kwa wanafunzi wa shule ya msingi Mtunduwalo ambao wamefuzu majaribio ya kujifunza kazi za makaa ya mawe na pia amezindua madarasa matatu ya shule hiyo ya msingi ambayo yamejengwa kwa ufadhili wa kampuni ya TANCOAL Energy.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mbinga mashariki Bw. Gaudence Kayombo ambaye amekua chimbuko la Mradi huo alielezea furaha yake ya kuanzishwa kwa mradi huo na kutoa wito kwa wananchi wake kujipanga kuuza bidhaa za kilimo kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo pamoja na kuchangamkia fursa ya ajira
Mwisho
No comments:
Post a Comment