NA MWANDISHI WETU
 
MKURUGENZI wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama amesema kuwa baada ya kupata mafanikio kwenye Tamasha la Pasaka,anatarajia kutoa baiskeli 50 za walemavu  zenye thamani ya Sh. milioni 30.
 
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Msama alisema kuwa fedha hizo alizoamua kuzielekeza kwa walemavu, zimetokana na mauzo mazuri ya DVD na VCD za tamasha la Pasaka lililofanyika mwaka huu, ambalo pia lilihudhuriwa na rais Jakaya Kikwete.
 
Alisema kuwa ameamua kufanya hivyo kutokana na kuguswa na matatizo ya watanzania wenzake hasa walemavu ambao wamekuwa wakitaabika kutafuta ridhiki, kutokana na kushindwa kutembea.
 
“Nimeona kuna haja ya kuwajali walemavu,nilichoamua ni kuwa ni vema hiki kidogo nilichokipata nimeona ni vema kama nitagawana nao,”alisema Msama.
 
Alisema kuwa tayari ameshaanza kazi ya kununua baiskeli hizo, ambazo zitakuwa ni za kisasa.
 
Baiskeli hizo atazigawa kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara,Songea na Tabora, ambapo Tabora na Songea kila mkoa mmoja utapata baiskeli 10 huku Lindi na Mtwara kila mmoja utapata baiskeli 15.
 
Kwa upande mwingine aliongeza kuwa utaratibu huo utaendelea kila mwaka, kwani anaamini wapo watanzania wenye matatizo ambayo yanahitaji kusaidiwa na anaona kwa upande wake analojukumu la kuwasaidia.
 
Mwisho..