Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kanda ya Nyanda za juu kusini Monica Mbelle
Na Joseph Mwambije ,Songea
SERIKALI Mkoani Ruvuma imesema itatoa kipaumbele katika kutoa ajira kwenye mgodi wa madini ya Urani yanayotarajiwa kuanza kuchimbwa hivi karibuni kwa Wahitimu wa Chuo cha mafunzo ya ufundi stadi(VETA) cha Songea Mkoani Ruvuma baada ya utafiti wa madini hayo kukamilika.
Msimamo huo wa Serikali ulitolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu kwenye Mahafali ya 26 ya VETA Songea kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Saveli Maketa ambaye aliwataka Wazazi kuwapeleka watoto wao katika Chuo hicho na kusema kuwa ukisomea ufundi huwezi kukosa kazi.
‘Vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi vina umuhimu mkubwa katika kipindi hiki ambacho ajira zimekuwa zikitatiza lakini pamoja na kusumbua kwa ajira lakini ufundi umekuwa ukiwafanya watu wachomoze na kufanikiwa kimaisha’alisema.
Kutokana na umuhimu huo alisema Serikali imepanga kujenga Vyuo vya ufundi stadi kila Wilaya ili kutoa nafasi kwa vijana wengi zaidi kupata ujuzi na kujiajiri na kwa kujiunga na Vyuo hivyo alisema wanaweza kupambana na umaskini.
Aliwataka wahitimu 52 kati yao wavulana 42 na wasichana 10 wa fani za aina mbalimbali waliosoma kwa miaka mitatu Chuoni hapo kwenda kutumia ujuzi walioupata kulijenga Taifa na kujiunga kwenye Vikundi vya maendeleo na Vyama vya akiba vya kuweka na kukopa(SACCOS) ili waweze kupata mitaji ya kununulia vitendea kazi.
Alilisisitiza kuwa wahitimu wa VETA na Wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla watapatiwa kipaumbele kwenye ajira katika mgodi wa Urani uliopo Namtumbo Mkoani humo ambao utakuwa mmoja wa migodi mikubwa duniani na kwamba utafiti wa madini hayo umeshakamilika na yataanza kuchimbwa hivi karibuni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kanda ya Nyanda za juu kusini Monica Mbelle aliwataka wazazi kuachana na dhana potofu kwamba ufundi ni kwa wavulana tu na kuwapeleka watato wa kike Chuoni hapo.
Aliwataka wahitimu kwenda kufanya kazi ya kusaidia jamii na kwamba kwa kutokufanya hivyo watakuwa hawajalitendea haki taifa lao kwa kuwa Serikali imetumia gharama kubwa kutoa mafunzo hayo huku ikitoza pesa kidogo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment