Na Steven Agustino, Tunduru
WATU wawili wakazi wa kitongoji cha Chipweteka katika kata ya Mlingoti Mashariki Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma Mussa Zubery (36) na Chuma Ramji(25) wamelazwa wakiwa hoi bini taabani katika Hospitali ya Serikali ya Wilaya hiyo baada ya kujeruhiwa vibaya na kundi laTembo lililovamia kijiji chao.
Mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa majeruhi hao walipatwa na mkasa huo baada ya kuvamiwa na kundi la Tembo hao ambao wamekuwa wakizagaa hovyo katika eneo la kitongoji hicho na vijiji jirani wakati wakienda mashambani.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Goerge Chiwango alisema kuwa hali za wagonjwa ni mbaya na kwamba Hospitali yake inatarajia kuwapeleka katika Hospitali ya Missioni ya Ndanda kwa matibabu zaidi.
Dkt. Chiwangu aliendelea kueleza kuwa majeruhi Mussa Zubery aliumizwa vibaya katika Mguu wa kushoto ambao pamoja na kuvunjwa mara mbili na Tembo huyo pia nyama za paja lake ziliondolewa kabisa katika tukio hilo pamoja na kuvunjwa mkono wake wa kushoto.
Kuhusu hali ya majeruhi Chuma Ramji Dkt. Chiwango alisema kuwa hali yake ni mbaya pia kutokana na kuvunjwa mguu wa kulia na tembo hao hali inayo wasukuma kuwahamisha majeruhi hao wote na kuwapeleka katika Hospitali ya Missioni baada ya wataalamu wa Hospitali yake kushindwa kuwahudumia.
Akizungumzia tukio hilo Kaimu wa kaimu Afisa maliasili wa Wilaya ya Tunduru Abdalah Mbanganike mbali na kukiri kuwepo kwake alisema kuwa tayari amekwisha peleka askari wenye silaha kwa ajili ya kuwasaka Tembo hao ili kuepusha matukio ya aina hiyo kwa wananchi wengine.
Aidha Mbanganike alitumia nafasi hiyo kuwaomba Wananchi wa Wilaya hiyo kutoa taarifa za matukio ya uharibifu wowote ambao umekuwa ukisababishwa na Wanyama ili waweze kupatiwa msaada kabla ya kupatwa na madhara.
Alisema idara yake inazo Bunduki na Risasi za kutosha pamoja na askari wenye ujuzi wa kutosha katika matumizi ya Silaha hizo wakati wa mapambano dhidi ya wanyama hao waharibifu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amedhibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa Jeshi la Polisi lipo tayali kwenda kutoa msaada katika idara hiyo endapo wataombwa kufanya hivyo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment