HOTUBA YA UFUNGUZI WA SONGEA GLOBAL NETWORK (SGN) KWENYE UKUMBI WA AGOPAL – SONGEA TAREHE 21/04/2012.
Mh. Mwenyekiti,
Mh. Katibu
Mh. Mhasibu
Ndugu Wanamtandao,
Ndugu Wageni waalikwa,
Mabibi kwa Mabwana.
ASALAAM ALYEIKUM! TUMSIFU YESU KRISTO!
Kwanza, Nampenda nianze kwa Kumshukuru Mungu kwa Baraka na Neema zake alizotujalia na kuweza kutufikisha hapa kwa ajili ya kufanya tukio muhimu la uzinduzi wa mtandao wenu huku tukiwa na afya njema na furaha.
Pili, naomba niwashukuru sana kwa kunialika kuja kuungana nanyi katika siku hii muhimu ya kuzindua mtandao wenu (Songea Global Network). Mmenipa heshima na kunionyesha upendo kwa mwaliko wenu. Asanteni sana!
Tatu, naomba nitumie fursa hii kuwapongeza sana kwa ndoto yenu, juhudi, nia na dhamira ya kuanzisha na kuendeleza mtandao wenu huu wenye malengo mliyojipangia ninyi wenyewe. Leo kweli nashuhudia ndoto ikizaa jambo la uhalisia nayo ni Songea Global Network, hongereni sana!
Chama au kikundi chochote cha watu hujengwa na mambo makuu matatu. Kwanza ni mahudhurio ya watu au wanachama, katiba na michango ya wanachama (rasilimali, ushauri, muda, fedha na nguvu). Kama mwanzo wa chama chenu napenda niwaombe tokea mwanzo kuwa kama mnanuia kweli ustawi, mafanikio na maendeleo ya mtandao wenu basi jibidisheni nyote kuhudhuria vikao bila kuchoka wala kudharau kwani mtu mmoja una thamani kwa mtandao huu. Tena jitahidini kuunda na kuwa na katiba imara itakayokuwa dira na mwongozo wa kufikia mafanikio ya malengo mliyojiwekea. Na Zaidi jalini mtandao wenu na kujitoa sadaka nguvu, akili, utashi, rasilimali muda na michango yenu ya hali na mali katika kujenga, kukuza na kustawisha. Haya kwenu ni ya msingi na ya kuzingatia kati ya mengi kama mnataka kuwa na mtandao imara na wenye nguvu.
Mmeunda mtandao kwa malengo mliyoyataja kama kusaidiana, kufahamiana, kujengeana uwezo na kushauriana n.k. Mie natambua kuwa mtandao ili uendelee mbele kuwa wenye nguvu, wenye mafanikio na watu wengi inapaswa kuutangaza, kuulinda, kuukuza, kuustawisha, kujivunia na kuufurahia. Tumieni fursa hii kufanya yale yote mtakayoona yanausaidia mtandao wenu kustawi na zaidi epukeni yale yote yanaweza kuvunja na kudhoofisha mtandao kama ubinafsi, dharau, chuki, fitina na majungu. Haya ni sumu kwenu!
Ntatolea lugha ya picha ya mtandao wenu. Mfano mtandao wa simu wa Vodacom unawauunganisha watu wenye line za Vodacom na wengine. Promotion zikitoka zinawapata wote na mtandao ukikatika hasara ni kwa wote. Vivyo nanyi, muwe na nia ya kuleta faida ya wote na kuepa yanayowaletea hasara wote. Hili limo ndani ya uwezo wenu.
Leo mmeitangazia Songea, Ruvuma, Tanzania na dunia kuwa mna ndoto kubwa ya mafanikio. Kwa kawaida kuanzisha kazi ni rahisi kuliko kuiendeleza na kuimalizia. Mmeanza kwa kishindo, sasa msirudi nyuma. Daima kwenda mbele kwa kasi na viwango ili ndoto yeni itimie. Inawezekana, timizeni wajibu wenu.
Naomba tuendelee kuchangia mtandao huu sisi sote tuliopo ili uweze kuwa msaada wa ushauri, msaada wa kiuwezeshaji na msaada wa rasilimali watu wenye upeo na ndoto kwa mkoa wetu wa Ruvuma. Kufanikiwa kwa Songea Global Network ni kufanikiwa kwa mkoa wa Ruvuma. Katika maisha mafanikio yanapimwa kuanzia mtu mmoja mmoja. Kama kikundi endeleeni kuutanganza vyema mkoa wetu wa Ruvuma. Mti hauwezi kujifanya kinyago mpaka umechongwa. Basi chongeni vyema mtandao wenu ili uzae matunda mema na bora sana.
Mimi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa natoa au Mkuu wa Mkoa ametoa kiasi cha Tsh 300, 000/= kuachangia umoja na mtandao huu wa wanasongea wenye nia njema ya kuwa kisima cha ushauri, uwezeshaji na watu wanaopenda kuitangaza Ruvuma kwa mafanikio katika yale wanayoyafanya. Naomba na wengine tuliopo hapa ambao hatujauchangia mtandao huu kila mmoja agusike na ajitolee hapa ili kuuchangia mtandao wetu kwani “Peke yetu tunafanya machache, pamoja tunafanya mengi,” alisema Hellen Keller, Mwanafasihi wa Marekani.
Mwisho, naomba niwatakie kila jema katika makuzi ya mtoto mliyemzaa leo Songea Global Network. Kuzaa si kazi, kazi ni kulea. Leeni mtandao huu uwe taa ya kutoa giza la umasikini na uwe chumvi ya kuleta ladha kwa mafanikio yenu na mkoa wa Ruvuma. Kama wengine waliweza kwanini nyie mshindwe?Hapana, kataeni msamiati wa kushindwa na siku zote neno msamiati wa kwanza uwe ni USHINDI DAIMA. Heri na mafanikio kwenu na Hongereni sana. Sasa natamka rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Said Mwambungu kuwa nimeuzindua rasmi mtandao wenu wa “SONGEA GLOBAL NETWORK.”
Mungu Ibariki Ruvuma,
Mungu Ibariki Songea Global Network
Asanteni kwa kunisikiliza.
RISALA YA WANAMTANDAO KWENYE UFUNGUZI WA SONGEA GLOBAL NETWORK (SGN) KWENYE UKUMBI WA AGOPAL – SONGEA TAREHE 21/04/2012.
Mh. Mgeni Rasmi,
Mh. Mwenyekiti,
Mh. Viongozi,
Ndugu Wanamtandao,
Ndugu Wageni waalikwa,
Mabibi kwa Mabwana.
HABARI ZA JIONI NYOTE!
Wahenga walishanasihi kwamba, “Moyo usiokuwa na shukrani hukausha mema yote.” Tutakuwa wezi wa fadhila kama hatutamshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa fadhili, rehema na mapendo kwa kutujalia sote uhai na afya na kutujalia nafasi hii adimu na adhimu ya kushiriki tukio hili la kihistoria uzinduzi wa mtandao wetu wa “SONGEA GLOBAL NETWORK.”
Tena, tusheheneze shukrani zetu nyingi kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mh. Said Thabit Mwambungu ambaye amebariki tukio hili liwepo kwa kumtuma mwakilishi wake Kaimu Afisa Tawala wa Mkoa wa Ruvuma ndugu… Seligius Ngahi …….kuja kuwa Mgeni wetu Rasmi. Naye akakubali kwa hiari na utayari. Asante sana ndugu kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi.
Hali kadhalika, tunawashukuru wale wote waliojitolea kufanikisha uanzishwaji wa mtandao huu. Wanamtandao wenyewe na wadau wageni waalikwa mabibi kwa mabwana. Asanteni sana. Tujipogeze pia wanamtandao kwa kufanikisha ndoto yetu leo walau ya kupanda mbegu ya Songea Global Network. Tulitaka na tukataka sana, tumefanikiwa sana leo kuanza rasmi safari yetu ya kuifisha ndoto yetu mbali.
Kila asubuhi Tanzania, swala huamka. Anajua kwamba ni lazima akimbie kwa kasi kuliko simba anayekimbia kwa kasi sana ama sivyo atauawa. Aidha, kila asubuhi simba huamka. Anajua kwamba ni lazima kumkimbiza swala anayekimbia polepole ama sivyo atakufa kwa njaa. Haijalishi kama wewe ni simba au swala…jua linapochomoza, ni vema kukimbia!
Nasi Wanamtandao wa kila kada tunaitwa leo, sasa na hapa tulipo tukimbie kwa kasi katika kuunganisha mtandao na kujiendeleza ama sivyo tutakufa kwa njaa au kuangamiza taifa letu!
Mhe, Mgeni Rasmi na Wageni waalikwa mabibi kwa mabwana,
Awali kabisa, Mtandao wetu ulianza kama wazo la kukutana na kufanya hafla ya kuuaga mwaka 2011. Lakini baada ya kukaa tukasema hapana, tulitajirishe wazo letu kwa kuanzisha mtandao utaotuunganisha wote hata baada ya sherehe kama umoja wenye nia ya kusaidiana wakati na shida na raha, kushauriana na kujengeana uwezo ili sote tufanikiwe. Baada ya majadiliano mapana na ya kina, tulikubaliana sote tuanzishe mtandao au umoja huo tukaupa jina la SONGEA GLOBAL NETWORK (SGN). Leo ndio siku tuliyokubaliana ya kupanda mbegu imara na safi ya mtandao huu ili umee na kuwa faida kwetu sisi wanachama na kuutangaza mkoa wetu wa Ruvuma kupitia mtandao wetu huu.
Tulichagua jina hili SGN kwa sababu na dhima ya kuunganisha watu wa kada mbalimbali bila kubagua umri, kazi, kabila, jinsia, rangi, dini wala itikadi. Anayekubali malengo yetu na kuwajibika kuchangia dira yetu, huyo ni mwanachama mzuri kwetu. Tunatumia fursa hii kuwaomba wanachama wengi wajiunge zaidi ili kuupa nguvu mtandao wetu. Tena hata wewe Mgeni Rasmi tunakuomba leo ujiandikishe kama mwanamtandao ili tuufanikishe mtandao wetu. Karibu sana!
Sisi wanamtandao tupo watu wa fani mbalimbali: wajenzi, mainjinia, mafundi, wahasibu, wanafunzi,madaktari, wajasiriamali, wafanyakazi wengine wa serikali, n.k. Ni mseto ulioiva wa wanachama wenye nia ya kushikamana na kutimiza ndoto ya mafanikio, udugu, ushirikiano na utajiri!
Mhe, Mgeni Rasmi na Wageni waalikwa mabibi kwa mabwana,
Tumeamua kuanzisha mtandao huu kwa MALENGO yafuatayo
Kwanza, kusaidiana na kujaliana kwa shida mbalimbali mfano. Misiba, dharura. Hata Bill Gates ana shida zake. Shida ni sehemu ya ubinadamu.
Pili, kufahamiana na kupanua mtandao katika dunia hii ya utadawazi ambapo watu wanatafuta kuungana na kushirikiana katika maisha ya kila siku. Kujifungia ni umaskini wa mawazo na fikra.
Tatu, kuwezeshana na kujengana kimawazo, kiushauri na kiuchumi.
Nne, kufunguliana fursa za kusaidiana kadri ya utaalamu na kazi ya kila mmoja.
Tano, baadaye kuwa na SACCOS itakayotuwezesha kiuchumi: kuweka akiba, kukopa.
Mafanikio ya malengo haya yanawezekana kadri tutakavyoendelea kuisimamia ndoto yetu kwa dhati. Ipo hadithi ya siku moja ambapo:
Watu walimuona sungura kashika fimbo na anatembea kwa haraka sana. Wakamuuliza sungura unaenda wapi mbona hauko kawaida? Naye akajibu kuwa naenda kuumuua tembo. Utaweza sungura? Naye akajibu ndiyo, nitajaribu!
Tuchukue wajibu wa kutekeleza mipango yetu kikamilifu na kutibu matatizo yetu wenyewe kwa ujasiri kwamba tunaweza kumuua tembo wa matatizo yanayotukabili katika kujiendeleza na kuujenga mtandao wetu. Yupo Mshairi maarufu wa Uskochi Robert Louis Stevenson aliyewahi kusema, “Usipime siku yako kwa yale uliyoyavuna bali kwa yale uliyoyapanda.” Malengo hayo yametufanya tuamue kupanda mbegu ya Songea Global Network ili baadaye tuvune mbegu ya mafanikio na utajiri wa ndoto yetu kwa maslahi ya wanachama na ustawi wa mkoa wetu wa Ruvuma ambao sisi ni wakazi.
Mhe, Mgeni Rasmi na Wageni waalikwa mabibi kwa mabwana,
Leo tunavyopanda rasmi mbegu ya mtandao wetu (SGN), tunatumia fursa hii kukumbushana wanamtandao masharti ya kufanikiwa ili tuendelee mbele zaidi kufikia malengo na ndoto yetu.
· Kujitoa kweli
· Kupenda kweli mtandao
· Kuwa na ndoto
· Kutoa michango ya dhati bila kuchoka
Ni kweli kuja pamoja ni mwanzo. Kufanya kazi pamoja ni umoja. Kudumu katika umoja ni maendeleo. Kuunganisha vipaji vyetu ni kuwa timu moja. Hatimaye kustahimili pamoja ni ushindi wa mtandao wetu huu.
Kuna Hadithi, Upendo, mafanikio na Utajiri : tukikaribisha upendo wa kweli tutafanikiwa katika malengo yetu na kutajirisha mtandao wetu kwa maendeleo ya mkoa wa Ruvuma. Tutafakari na tuchukue hatua.
Inapendeza, inakubalika, inawezekana na inahitajika kuwa na mtandao imara usiokatika network na kufanikiwa kweli. Ni kweli wahenga wa Ghana walishatuasa kwa methali yao kuwa, “Unaweza kumlaumu mtu kwa kukuangusha chini lakini ujilaumu mwenyewe kwa kukataa kunyanyuka.” Naomba wanamtandao tulioamua kuanzisha kwa hiari mtandao huu tusikalie kumlaumu mtu au kujilaumu wenyewe na badala yake tudhamirie na kuwa na bidii ya kunyanyuka leo na kuendeleza ndoto na mtandao wetu. Bila shaka linaloonekana haliwezekani litawezekana, milima isiyokweeka itakweeka na miti isiyopandika itapandika.
Tumuombe Mungu ili idumu, iote na ifanikiwe mbegu ya SGN ambapo sote tuchangie maendeleo yetu na ya taifa letu la Tanzania. Karibuni sote tufurahie jambo hili adhimu na tuchangie kila mmoja kwa nafasi na uwezo wake, kiushauri na kirasilimali aliyonayo kwa mafanikio ya SGN. Tushikane mikono tuanze safari yetu kwa hatua ya kwanza leo, kwani hata Waswahili wanasema, “Safari ya maili elfu huanzia na hatua moja.” Na hakika ni kweli. Tumethubutu kubuni na kuanzisha mtandao, tumeweza kuanzisha mtandao huu na sasa tunanuia kusonga mbele na mtandao tuliouanzisha.
SGN safi, safi sana, SGN juu, juu sana!
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Atubariki sote.
Asanteni sana kwa usikivu wenu wa makini!
Naomba kuwasilisha!
KWA NIABA YA WANAMTANDAO WA SONGEA GLOBAL NETWORK. Imeandaliwa na Kusomwa na JOHN M. KASEMBO: 0755 417 074 / 0712 120 775: jmkasembo@gmail.com
Mgeni rasmi aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, Seligius Ngahi akiteta jambo na Mwenyekiti wa Mtandao wa Songea Global Network Sakina Jamal wakati wa hafla ya uzinduzi wa mtandao huo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Agopal
Katibu Mtendaji wa Songea Global Network John Kasembo akitafakari jambo wakati wa hafla hiyo
Mhasibu wa Mtandao wa Songea Global Network Rehema Nasibu akiendelea na utaratibu stahiki katika hafla hiyo
Wanakamati ambao pia ni wanachama wa Mtandao wa Songea Global Network wakiwa na Mwenyekiti wa Mtandao huo Sakina Jamal katika viwanja vya Agopal
Wanachama wa Mtandao wa Songea Global Network wakijadiliana jambo wakati wa hafla hiyo
Wanachama wa Mtandao wa Songea Global Network wakijadiliana jambo wakati wa hafla hiyo
Wanachama wa Mtandao wa Songea Global Network wakijadiliana jambo wakati wa hafla hiyo
Wanachama wa Mtandao wa Songea Global Network wakijadiliana jambo wakati wa hafla hiyo