About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Sunday, June 30, 2013

SANGA ONE AHUDHURIA KILELE CHA MASHINDANO YA ANSIGAR CUP PERAMIHO NA ANATARAJIA KUYAFUNGA LEO

 Viongozi mbalimbali wakiimba wimbo wa Taifa ulioimbwa katika Mashindano hayo, wakwanza kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa FARU, Golden Sanga, wa pili Mfadhiri wa mashindano hayo kwa niaba ya Dkt Ansigary Stuffe, na watatu ni Mwandishi Mahili wa Michezo katika Redio ya Jogoo Onesmo Emeran
 Miongoni mwa Timu shiriki ikiwajibika kuimba wimbo wa Taifa kabla ya kufunga mashindano hayo

 Mr Kolumbani Lugendo ambaye ni Msimamizi wa MECHI aliyeonyesha mkono akimpa maelekezo ya awali Mgeni Rasmi Mwenyekiti wa FARU Golden Sanga mwenye tai kabla hajazikagua timu shindani, wa kwanza kulia ni Katibu wa Mashindano Sixbert Komba, wa kwanza kulia ni Katibu wa SORUFA Iddfonsi Luoga, nyuma kabisa ni Ayubu Mvulla ambaye ni Mwenyekiti wa Mashindano hayo

Mwenyekiti wa Faru Golden Sanga akiendelea kuzisalimia na kuzikagua timu kabla hazijaanza mashindano hayo

Katika Fainali hiyo ya Ansigary Cup ambaye imefanyika mbele ya Mgeni Rasmi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma Golden Sanga (SANGA ONE) Timu mbili zilichezwa katika Uwanja wa Ansigary hapa PERAMIHO na kuhudhuriwa na mamia ya wapenzi na mashabiki wa timu hizo


Fainali hiyo iliwakutanisha Kilangano B 9 wenye pointi na Litisha yenye pointi 6

Mashindano hayo yalianza kwenye ngazi ya Tarafa April 21 mwaka huu na kuzinduliwa rasmi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimike na kuhitimishwa Juni 30 mwaka huu na Mwenyekiti Golden Sanga

Habari kamili za mashindano hayo zitaendelea kukujia kupitia Mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com

Monday, June 24, 2013

MBUNGENI WA CCM AHOFIA TANZANIA KUWA NA RAIS "SHOGA"


                                                      
               Ali Keissy (CCM), MBUNGE wa Nkasi Kaskazini

Na, Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy (CCM), amesema kuwa bila Watanzania kuwa makini na sheria mpya ya ndoa ijayo, huenda nchi ikapata rais, wabunge na madiwani wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja (mashoga).

Keissy alitoa kauli hiyo wakati akichangia mada katika mkutano wa siku tatu wa Chama cha Wabunge cha Kupambana na Ukimwi (TAPAC) uliomalizika jana mjini Dodoma.

Mbunge huyo aliwaomba viongozi wa dini kukemea kwa nguvu vitendo hivyo, pia alipinga hatua ya wazazi kuwapeleka watoto wao wadogo shule za bweni akidai kuwa huko ndiko wanakojifunza vitendo hivyo.

“Mnashindwa kulea watoto wenu, mnawapeleka shule za bweni wakiwa na miaka mitatu ili walelewe kizungu. Huko watapakwa mafuta ya KY na wataingiliwa,” alisema.

Keissy alitolea mfano mkutano mmoja uliofanyika jijini Dar es Salaam kuwa uliwashirikisha mashoga 400, jambo alilodai ni ishara kwamba wanaojihusisha na vitendo hivyo wanaongezeka, na hivyo kuitaka serikali kuwapiga marufuku.

Hata hivyo, baada ya mbunge huyo kuhitimisha mchango wake, mmoja wa vijana wanaojihusisha na mapenzi hayo ya jinsia moja, Abdilah Ally ambaye alikuwa amealikwa na TAPAC, alitetea kuwa jamii inapaswa kukubali kwamba matendo hayo yanafanyika.

“Tunatambua kuwa sheria haziruhusu vitendo hivi, lakini vipo na vinafanyika na tunapata maambukizi kwa kiwango kikubwa. Tunachokitaka tusinyanyapaliwe na jamii, bali tupewe huduma ya afya ya kujikinga na maambukizi.

“Mathalani mimi hapa nina wapenzi wanaume watatu ambao nashiriki nao mapenzi, sasa kama nimeathirika ina maana wote wale nao wamethirika,” alisema.

Akifunga mkutano huo, Naibu Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, aliwasihi wanasiasa wasiwabague makundi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya ushoga, usagaji na matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema kuwa makundi hayo yanakabiliwa na janga la maambukizi makubwa ya virusi vya ukimwi, hivyo wanahitaji kusaidiwa kuondoka katika makundi hayo badala ya kuwahukumu.

Mwalimu alifafanua kuwa miongoni mwa washiriki wa mkutano huo kutoka katika makundi hayo, alikuwa mtumiaji wa dawa za kulevya, lakini baada ya kupata msaada wa kiafya ameachana na vitendo hivyo na sasa anaendelea vizuri chini ya uangalizi.

Mkutano huo uliratibiwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), kama wadau wakuu waliotoa mada mbalimbali kuhusu jinsi wanavyopambana kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi.

Katika hilo, Mwalimu alisema kuwa serikali dhamira yake ni kufikia maambukizi asilimia sifuri, hasa kwa kutoa msukumo mkubwa kwa makundi ya wanawake, vijana na watoto ambayo yana maambukizi zaidi.

Mbunge wa Chambani visiwani Zanzibar, Yusuf Salam Hussein (CUF), alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kupunguza maambukizi hayo kwa wanandoa kutokana na sheria ya kuwataka wapime ukimwi kabla ya kufunga ndoa.

CHANZO: TANZANIA DAIMA

TGNP WAFUNGA MITAMBO YA KISASA MOROGORO

 Afisa Habari na Mawasiliano wa TGNP Lilian Kittunga akifundisha Program Maalum ya Kutumia mawasiliano miongoni mwa Vikundi vya Sauti ya Jamii Kituo cha Taarifa na Maarifa
Na, Mwandishi Wetu, Morogoro

MTANDAO wa Jinsia nchini (TGNP), umepanua mawasiliano kwa kutoa na kufunga mitambo ya kisasa ya mawasiliano kwenye vituo vya taarifa na maarifa ya jamii chini ya wanaharakati wa maendeleo katika mikoa mitano nchini.

Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki wilayani Morogoro na Ofisa Programu ya Utetezi na Mawasiliano na Habari TGNP, Deogratius Temba wakati akikabidhi mtambo wa aina hiyo kwenye kituo cha wanaharakati Mkabarani.

Alisema dhamira ya wananchi kuwezeshwa mtambo huo ni kuzinduliwa mradi wa ‘Sauti ya Jamii’ ambapo hapo utaitwa 'Sauti ya Jamii Mkambarani', ili kuongeza nguvu ya pamoja katika mapambano ya mabadiliko chanya ya maendeleo kwa kuhabarishana.

“Kuanzishwa kwa ‘Sauti ya Jamii’ na kutolewa kwa mtambo huu ni matokeo ya changamoto zilizojitokeza kwenye matamasha na mafunzo yaliyotolewa kwa jamii na TGNP hivi karibuni,” alisema Temba.

Alisema malengo ya kituo ni kumwezesha mwanawake na jamii kujikwamua kifikra, kiuchumi, kisiasa na kumharakishia maendeleo kutoka katika mfumo dume unaomzunguka.

Akitoa nasaha juu ya uanaharakati bora, Diwani wa Kata ya Mkambarani, Daniel Shawa, aliwataka wanaharakati kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizopo ili waheshimike na kuthaminiwa katika jamii wanayoitetea.

Mtambo huo ulioambatana na vifaa vya teknolojia ya kisasa ikiwemo kompyuta, ‘printer’ na chombo cha kuhifadhia vimetolewa Mkambarani wilayani Morogoro, Kisarawe mkoani Pwani, Kishapu mkoani Shinyanga, Songea na jijini Dar es Salaam.
MWISHO

Saturday, June 22, 2013

OFISI YA CCM YANUSURIKA KUCHOMWA MOTO KATIKA VURUGU ZA MADIWANI

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho

Na Stephano Mango, Songea.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma kimelazimika kusitisha uchaguzi wa kura za maoni wa kumpata Mgombea Uenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Mbinga baada ya baadhi ya Madiwani kuilalamikia Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Ruvuma ambayo inadaiwa kuwa ilishinikizwa na kigogo mmoja wa CCM kukata jina la mmoja kati ya Madiwani walioomba kugombea nafasi hiyo na kusababisha kuwepo vurugu kubwa za kisiasa ambazo zimesabibisha jengo la CCM la wilaya kunusurika kuchomwa moto na watu wasio fahamika.

Habari zilizopatikana jana mjini hapa kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambazo zimethibitishwa na Katibu wa Chama hicho Mkoa wa Ruvuma Velena Shumbusho zimesema kuwa uchaguzi wa kura za maoni wa kumpata Mgombea Uwenyekiti wa halmashauri hiyo umesitishwa mpaka hapo baadae tarehe itakapopangwa tena.

Shumbusho aliuambia Mtandao huu kwa njia ya simu kuwa uchaguzi huo umehairishwa mpaka CCM mkoa kupitia Kamati yake ya utendaji itakapopanga tena kwani hali ya kisiasa kwa sasa si shwari.

Alifafanua zaidi kuwa pamoja na kusitisha uchaguzi huo jengo la ofisi ya CCM la wilaya hiyo limenusurika kuchomwa moto na watu wasiofahamika jambo ambalo limesababisha wanachama wengi kushtushwa.

Aliwataja Madiwani wa CCM waliojitokeza kugombea nafasi ya hiyo kuwa ni Alanusi Ngahi ambaye ni Diwani wa Kata ya Kipapa, Alani Mahai Diwani wa Kata ya Maguu na Nathaniel Charles Diwani wa Kata ya Matili ambapo kamati ya siasa ya mkoa ilipokaa ilirudisha majina mawili ya Mahai na Charles jambo ambalo limeonekana kuwa na mtafaruku mkubwa baada ya baadhi ya Madiwani kuilalamikia Kamati ya Siasa kwa nini imekata jina la Diwani Alanusi Ngahi na kwamba majina ya nafasi ya Makamu mwenyekiti majina yote matatu ya madiwani walioomba yalirudishwa ambao ni Winfrid Kapinga diwani wa kata ya Ngima, Agnesi Mahangula na Prisca haule ambao wote ni Madiwani wa viti maalumu (CCM) .

Alibainisha kuwa Kamati ya Siasa ya Mkoa chini ya Mwenyekiti wake Oddo Mwisho ilikaa siku nne zilizopita na kupendekeza majina mawili ya wagombea ndio yaliyoletwa kwenye kikao cha Kamati ya Siasa ( CCM) Wilaya ya Mbinga ambayo ililidhia uchaguzi huo ufanyike lakini hakuna kigogo yeyote aliyeshinikiza kukata jina la mgombea bali ni kamati yenyewe ilifikia uwamuzi huo.

Baadhi ya Madiwani wa Halmshauri ya Wilaya ya Mbinga ambao hawakutaka majina yao yatajwe waliuambia Mtandao huu kwa nyakati tofauti walisema kuwa matukio hayo yanasababishwa na viongozi wenyewe wa CCM wa ngazi ya Wilaya na Mkoa kwani inaonyesha wazi kuwa jina la mgombea Ngahi limekatwa kwa shinikizo la kigogo mmoja ambaye ndiye kiongozi mmoja wa CCM vilevile ni kiongozi wa ngazi ya juu wa Halmshauri ya Wilaya mpya ya Nyasa ambayo inatarajia kugawanywa kuwa Halmashauri mbili tofauti

Walisema kuwa tukio hilo linahofiwa kuwa limetokana na Kamati ya Siasa ya Mkoa kutorudisha jina la mgombea jambo ambalo limewafanya baadhi ya Madiwani wagomee uchaguzi lakini swala la kutaka kuchoma jengo la CCM linahitaji Polisi waingie ndani zaidi kufanya upelelezi ili kuwabaini waarifu wenye tabia chafu za kutaka kukichafua Chama Cha Mapinduzi

Kwa upande wake Katibu wa CCM wa Wilaya ya Mbinga Anastasia Amasi alisema kuwa tukio la kutaka kuchoma ofisi yake limetokea Juni 20 mwaka huu majira ya saa za usiku ambapo alidai kuwa yeye akiwa nyumbani kwake juzi majira ya saa za asubuhi alipata taarifa za tukio hilo na alieleza kuwa alipofika kwenye eneo la tukio aliona uharibifu uliofanyika.

Alieleza zaidi kuwa baadaye alitoa taarifa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya ya Mbinga na Askari Polisi walipofika kwenye eneo la tukio walichukua maelezo ya awali kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kufafanua kuwa kwenye eneo la tukio yalikutwa masalia ya mafuta yanayodaiwa kuwa ni ya Petrol kwenye chupa yenye ujazo wa lita moja yaliyoletwa na waalifu waliotaka kufanya tukio hilo, lakini mlango mmoja na madirisha mawili pamoja na mapazia ya madirisha hayo yaliungua na moto.

Naye Mkuu wa kikosi cha Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Ruvuma Baraka Mvano alipohojiwa na www.stephanomango.blogspot.com kwa njia ya simu alikanusha kuwepo kwa tukio hilo na kudai kuwa ofisi yake haijapata taarifa ya aina yoyote ila anaendelea kufuatilia zaidi.

Hata hivyo Mtandao huu ulijitahidi kufanya mawasiliano ya kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeki ili atoe ufafanuzi juu ya tukio hilo ziligonga mwamba baada ya kumpigia simu zaidi ya mara tatu ambayo ilikuwa haipokelewi na baadaye Mtandao huu ulilazimika kuwasiliana na Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Ruvuma aliyejitambulisha kwa jina moja la Malimi ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo alidai kuwa lilitokea Juni 20 mwaka huu majira ya usiku lakini hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na Polisi inaendelea kufanya upelelezi zaidi ili kuwabaini watuhumiwa.

Friday, June 21, 2013

WATOTO WALILIA HAKI ZAO ZA KUISHI, KULINDWA NA KUHESHIMIWA



                              Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng, Stella Martin Manyanya ambaye pia ni Mbunge wa Vitimaalum Mkoa wa Ruvuma akizungumza na Watoto wa Wilaya ya Nyasa alipotembelea wilayani humo hivi karibuni

Na Gideon Mwakanosya ,Namtumbo

WATOTO wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kukomesha vitendo vya ubakaji vinavyofanywa kwa watoto wadogo wilayani humo kwani tatizo hilo limeonesha kuwa kubwa ambapo katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu jumla ya watoto 14 walibakwa na kesi zao kuripotiwa katika kituo kikubwa cha Polisi cha Wilaya hiyo.

Wakisoma Risala ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu jana iliyofanyika Kiwilaya katika kijiji cha Hanga wilayani Namtumbo walisema kuwa pamoja na jitihada za Serikali na wadau mbalimbali za kukomesha vitendo vya unyanyasaji kwa watoto wadogo bado tatizo hilo ni kubwa kwa Wilaya ya Namtumbo.

Walieleza kuwa katika takwimu za miaka miwili iliyopita zinaonesha kuwa mwaka 2012 wanafunzi 16 waliacha shule kutokana na mimba na wanafunzi 151 kati ya hao wavulana 88 na wasichana 63 waliacha shule kwa utoro na mwaka 2013 wanafunzi 12 wa kike walipata ujauzito na kuacha shule huku wanafunzi 34 walikuwa watoro mwaka 2012 na mwaka 2013 wanafunzi 18 ambao waliripotiwa kuwa watoro.

Walisema kuwa tatizo la watoto kutumikishwa kazi za majumbani kama vile kazi za ndani na mashambani,kutumiwa na watu wazima kufanya biashara ndogo ndogo hata kama wanatakiwa kuwepo mashuleni bado limekuwa ni tatizo hivyo ni vyema kila mzazi akatambua kuwa kila mtoto ni wake na anahitaji malezi bora hasa kuwapatia elimu iliyo bora na itasaidia kupunguza tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Kwa Upande wake mgeni rasmi wa maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alisema kuwa kila wananchi wakiwemo wazazi na walezi wanawajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wao hawatumikishwi kazi za hatari na kazi zinazowazidi umri ili kupunguza tatizo la watoto kukimbilia mitaani na kujiingiza katika mambo mabaya ikiwemo madawa ya kulevya.

Alisema kuwa kutowajibika kwa wazazi na walezi katika kulea familia kunasababisha mambo mengi yasiyofaa ndani ya jamii ikiwemo utoro,mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari hivyo ni wajibu wa kila mzazi katika kuwafichua waharifu wanaowapa mimba wanafunzi ili vitendo hivyo vikomeshwe kabisa ndani ya Mkoa huo.

Aidha alisema kuwa wazazi na walezi watambue kuwa watoto wanahaki ya kulindwa, kukua,kuendelea kuishi na kushiriki kutoa mawazo ndani ya jamii lakini kuna baadhi ya wazazi a walezi watoto wanapohitaji huduma hupewa karipio kali na wakati mwingine kipigo pasipo sababu.

MWISHO.

Monday, June 17, 2013

TGNP WAKABIDHI VIFAA SAUTI YA JAMII SONGEA


 
Afisa Habari na Mawasiliano wa Mtandao wa Jinsia Tanzani(TGNP) Lilian Kitunga akimkabidhi Vifaa vya mawasiliano Kompyuta, Printer, Moderm na muda wa wa Shilingi 500,000/= Mwenyekiti wa Kituo cha Sauti ya Jamii, cha Taarifa na Maarifa Songea Fatuma Missango
Mama Siwajibu Gama akisisitiza jambo kwenye kikao cha  Wanachama wa   Sauti ya Jamii, Kituo cha Taarifa na Maarifa Songea
Wa kwanza kushoto ni Mwandishi wa Habari wa IPP MEDIA, Nathan Mtega akiwa na Wanaharakati mbalimbali kwenye Ofisi za Sauti ya Jamii, Kituo cha Taarifa na Maarifa, juzi
  
Kutoka kushoto ni Wanaharakati Dada, na Mama Karimu wakisikiliza kwa makini makabidhiano ya Vifaa kutoka TGNP
                      

Sunday, June 16, 2013

KITUO CHA SAUTI YA JAMII SONGEA CHAPEWA MSAADA WA KOMPYUTA NA TGNP



Na, Stephano Mango, Songea

WANAWAKE waliopo pembezoni wametakiwa kukithamini na kukitumia Kituo cha taarifa na maarifa ili kuweza kupaza sauti zao kikamilifu katika changamoto zinazowakabili kwenye ujenzi wa tapo la ukombozi wa wanawake kimapinduzi

Wito huo umetolewa jana na Afisa Habari na Mawasiliano wa Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TGNP) Lilian Kitunga alipokuwa akikabidhi msaada wa Kompyuta,printer, moderm na muda wa maongezi vyenye thamani ya shilingi milioni 1.9 kweny Ofisi ya Sauti ya Jamii Kituo cha Taarifa na Maarifa Songea

Kitunga alisema kuwa msaada huo unapaswa kutumiwa kwa malengo kusudiwa ya mawasiliano kwa kuwafikia watu mbalimbali, kujenga nguvu ya pamoja katika kuleta mabadiliko chanya kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu (sms) kwa gharama za Tgnp ili kuweza kuunganisha nguvu katika kuhabarishana na kuchukua hatua za kuwajibisha mamlaka na kuleta mabadiliko chanya

“Sauti ya Jamii itatumia teknolojia ya bulk sms kwa kutuma ujumbe kwenye simu kwa kutumia Kompyuta kwa zaidi ya watu 10,000 kwa wakati mmoja kwa lengo la kupashana habari za ujenzi wa vuguvugu la kimapinduzi” alisema Kitunga

Alifafanua kuwa kwa zaidi ya miaka 18 sasa, Tgnp imejikita katika harakati za kupigania haki za binadamu hasa wanawake na makundi yaliyopo pembezoni, usawa wa kijinsia, pamoja na ujenzi wa vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika ngazi zote za kijamii

Alisema kuwa Tgnp kwa kushirikiana na wada wengine ilibaini kuwa mbinu za kupeana taarifa kwa wakati baina ya vikundi na asasi za kimataifa ni tatizo kubwa ambalo linakwamisha jitihada za ujenzi bora wa tapo la ukombozi wa wanawake wa kimapinduzi

Alieleza kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo moja ya mikakati iliyowekwa ni kuanzisha na kuviendeleza vituo vya Taarifa na Maarifa kwa kushirikiana na jamii ambavyo vitakuwa vitovu vya harakati katika ngazi ya jamii

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sauti ya Jamii Kituo cha Taarifa na Maarifa Songea Fatuma Misango alisema kuwa mradi huo ulibuniwa na Tgnp utaongeza chachu ya kuleta mabadiliko katika jamii na kuboresha mahusiano na mitandao ya kupashana habari kati ya Wanaharakati, Vikundi na Mitandao katika ngazi ya Jamii hadi Taifa ili kupunguza pengo kati ya wanao faidi taarifa muhimu na wale ambao hawapati taarifa hizo

Misango alisema kuwa kuanzishwa kwa Kituo hicho kutasaidia kunoa uelewa wa wanawake waliopo pembezoni wa uchambuzi wa masuala ya kimfumo, Kisera na kimuundo na kutumia chambuzi hizo katika kudai uwajibikaji na mabadiliko yenye mrengo wa ukombozi wa wanawake wa kimapinduzi

MWISHO

TGNP NA MPANGO WA UTAFITI SHIRIKISHI WA URAGHABISHI



Miongoni mwa Wanawake walipo Pembezoni wakipepeta pumba za Mchele ili waweze kupata punje za mchele ambazo zinawasaidia kwenda kutengeneza chakula chao au vitumbua ambavyo wanaviuza na kujikimu na maisha, hapo ni Songea
Bibi mkazi wa Bombambili Songea ambaye anakadiliwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 70, akitengeneza udongo ambao unapendwa sana na kina mama(Picha zote na Stephano Mango, Songea)

Na, Privatus Karugendo

KATIKA jitihada zake za kupambana na mfumo dume, uliberali mamboleo na mifumo yote kandamizi na kupambana ili rasilmali ziwanufaishe wanawake walioko pembezoni, TGNP imeanzisha mpango wa utafiti shirikishi wa uraghabishi.

TGNP, imeamua kuukumbatia mpango huu kwa vile unatoa nafasi pana ya ushirikishwaji hadi ngazi ya vijijini na kuchochea kuibua kero na changamoto nyingi ambazo zinahitaji majibu ya jamii nzima.

Mpango huu unatumika kama mbinu muhimu ya kujifunza, kutafakari, kuchambua na kutekeleza mikakati mbalimbali ya ujenzi wa Tapo la ukombozi wa wanawake kimapinduzi lililokita katika ngazi za msingi ya kijamii na lenye uwezo kwa kudai uwajibikaji katika kutoa huduma bora, kusimamia rasilimali za taifa ili ziwanufaishe makundi yaliyoko pembezoni hususan wanawake.



Lengo kuu na mpango huu wa utafiti shirikishi wa uraghabishi ni kuwezesha ushiriki wa wanawake, wanaume, makundi na mitandao katika ngazi ya jamii kufanya uchambuzi wa hali halisi kwa mrengo wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi; kuibua kero na changamoto zinazokabili makundi husika na za pamoja.

Mpango huu pia unalenga katika kukuza uwezo na uelewa wa uchambuzi wa kero zinazoikabili jamii.

Tamko la TGNP kwa vyombo vya habari lilitolewa tarehe 9. 6. 2013, ni la mpango huu ulioendeshwa kwenye wilaya tatu za Mbeya Vijijini, Kata ya Mshewe, Morogoro Vijijini Kisaki na Kishapu – Shinyanga. Katika makala hii tutajadili mrejesho wa utafiti huu ambao ni wa aina yake.

Changamoto za uwekezaji na mgawanyo mbaya wa ardhi kwa wananchi, ilijitokeza katika utafiti huu na mfano mzuri ni Kata ya Mshewe, Mbeya Vijijini. Katika kata hii utafiti ulibaini mgawanyo mbaya wa ardhi kwa wawekezaji; ardhi nzuri na yenye rutuba imetolewa kwa wawekezaji kiasi kwamba wenyeji hawana mashamba na wanalazimika kuwa vibarua kwenye mashamba ya wawekezaji.

Mbaya zaidi ni kwamba wawekezaji wenyewe wanawalipa kidogo. Mfano wanawake wanalipwa kati ya shilingi 2,500 hadi 3,000 kwa siku.

Pamoja na kulipwa kidogo, wanakumbana na rushwa ya ngono na manyanyaso mengine hali inayosababisha ongezeko la magonjwa ambukizi yakiwamo VVU na ukimwi.

Changamoto hii ya mgawanyo mbaya wa ardhi imejitokeza pia katika Kata ya Kisaki, Morogoro mjini, ambapo wakulima wadogo wadogo wanapambana na wafugaji.

Kwa vile wafugaji hawana maeneo ya kutosha kwa mifugo yao, wanaingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kuleta vita mbaya. Kwa upande mwingine wafugaji wanatumia fedha kuwahonga viongozi ili wasisumbuliwe wanapoingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.

Matumizi ya fedha ni kupokonya wanyonge haki zao, ni tatizo sugu kwa wananchi waishio pembezoni.

Suala jingine muhimu lililojitokeza kwenye utafiti huu wa TGNP kwenye wilaya tatu, ni upatikanaji wa maji safi na salama.

Pamoja na sera ya taifa kwamba maji yawe umbali wa mita 400 kutoka kwa makazi ya watu, bado maeneo mengi hapa Tanzania yana tatizo kubwa la kupata maji safi na salama. Watu wa Kishapu na Mshewe, ni miongoni mwa wananchi wa Tanzania ambao bado wana tatizo hili kubwa. Kijiji cha Ilota- Mshewe, wananchi wanalazimika kuchangia maji machafu na mifugo.

Tatizo hili la maji safi na salama ni kubwa sana katika vijiji vya Isoso na Lubaga katika Kata ya Kishapu, wanawake wanatembea mwendo mrefu na katika mazingira hatarishi kutafuta maji; mazingira haya yanasababisha mimba za utotoni, ubakaji na vipigo kwa wanawake wakichelewa kutoka kuchota maji.

Na nyongeza ni kwamba muda mwingi na rasilmali vinatumika kusaka maji kitu kinachoongeza hali ya umaskini katika jamii ya watu hawa wa Kishapu.

Ukosefu wa huduma bora za afya ni suala jingine lililoibuliwa na mpango wa utafiti shirikishi wa uraghabishi. Mfano kati ya wanawake 20 walihojiwa katika Kijiji cha Ilota, Mbeya Vijijini ni mwanamke mmoja tu ndiye aliyetaja kujifungulia hospitali.

Umbali wa hospitali na vituo vya afya unawalazimisha wanawake wengi kuzalia nyumbani kwa wakunga wa jadi.

Hii ni hatari kwa mama na mtoto na kuna ukweli wa wanawake wengi kupoteza maisha wakati wa kujifungua na watoto kutopata huduma muhimu za chanjo wakiwa na umri chini ya miaka mitano.

Kata ya Kisaki, Morogoro Vijijini, tatizo si hospitali wala kituo cha afya, tatizo ni dawa na wahudumu wa afya katika vijijini vya Gomero, Stesheni na Nyarutanga. Vijiji hivi vina majengo mazuri, lakini hakuna dawa na wahudumu.

Mbali na tatizo hilo, pia inapobidi wananchi wanachangia gari la wagonjwa shilingi 70,000, ili kumpeleka mama mja mzito kwenye Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Hali hii ni hatari, maana wanawake wengi wanaweza kupoteza maisha yao kwa kushindwa kulipia hizo shilingi 70,000.

Ukiachia masuala hayo yaliyotajwa hapo juu, utafiti huu wa TGNP, ulibaini kwamba lipo tatizo la msingi ni uongozi mbovu na rushwa. Hili lilitajwa kila sehemu iliyofanyiwa utafiti.

Kwamba uongozi mbovu na rushwa vinasababisha ukosefu wa huduma za msingi kwa wanawake na wanaume walioko pembezoni.

Na kwamba kuna usiri wa taarifa za mapato na matumizi, viongozi kutowashirikisha wananchi katika masuala ya maendeleo, viongozi ngazi za vijiji kuruhusu video za ngono na viongozi kutotekeleza ahadi zao kwa wananchi.

Ni mengi yaliyojitokeza kwenye utafiti huu, ila yametajwa machache ili kufikisha ujumbe kwa wahusika, ili wajaribu kutafuta majibu ya kuondoa unyanyasaji wa wanawake na wasichana katika wilaya hizi zilizotembelewa na watafiti wa TGNP pamoja na maeneo mengine ndani ya taifa letu.

Mfano tatizo la maji linasababisha vipigo kwa wanawake, ubakaji, elimu duni kwa wasichana, mimba za utotoni na ukosefu wa kipato.

Serikali kuu na serikali za mitaa zinaweza kuyatumia matokeo ya utafiti huu kurekebisha matatizo yaliyoorodheshwa hapo juu: Mfano serikali kuirejesha ardhi ya Kata ya Mshewe inayomilikiwa na wawekezaji wa nje na ndani ya nchi, kwa manufaa ya wananchi sasa na vizazi vijavyo.

Pia serikali itenge maeneo ya wafugaji katika Kata ya Kisaki, ili kuepusha mapigano kati ya wakulima na wafugaji.

Huduma ya kupatikana maji safi na salama ishughulikiwe katika vijiji vilivyotajwa na ambavyo havikutajwa.

Utafiti huu umeonesha wazi kwamba maji safi na salama ni muhimu kwa Watanzania wote. Huduma ya hospitali pia iboreshwe. Pia ni muhimu kuwapo na mfumo wa kuwawajibisha viongozi wote wanaokiuka maadili ya kazi zao ili kuondokana na aina zote za rushwa na ukatili wa kijinsia hasa ukatili kwa wanawake na wasichana.

Lakini pia viongozi wawakilishi hususan madiwani na wabunge wanaweza kutumia matokeo ya utafiti kudai uwajibikaji wa serikali kwa wananchi katika ngazi zote kupita bajeti, ripoti ya mkaguzi wa serikali, kudai sera ya haki ya uhuru wa wananchi na mikakati mbali mbali ya maendeleo.

Vyombo vya habari, taasisi za utafiti na makundi ya kiraia yanaweza pia kuutumia mpango huu wa utafiti shirikishi wa uraghabishi kuibua masuala ya wanajamii na kujenga uwezo wa wanajamii kuhoji na kudai uwajibikaji.

Hapana shaka kwamba mpango huu wa utafiti shirikishi na uraghabishi ndio unafaa kabisa kubainisha chanzo cha vurugu za Mtwara. Mpango huu unamruhusu kila mshiriki kuzungumza bila kuogopa na kwa njia hii ya uraghabishi, watu wanajifunua na kujiweka wazi.


+255 754 633122 www.karugendo.net

Thursday, June 13, 2013

CCM WANYUKANA HADHARANI



                       Mwenyekiti wa Ccm Taifa , Rais Jakaya Kikwete
• Jaji Bomani aungana na Warioba kutaka serikali tatu

Na Chalila Kibuda

SIKU moja baada ya Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushindwa kutoa msimamo juu ya mapendekezo ya rasimu ya katiba inayotaka uwepo wa serikali tatu, Jaji Mstaafu Mark Bomani amesema kuwa chama hicho tawala hakitaki serikali tatu.

Jaji Bomani ambaye ni mmoja wa majaji wenye ushawishi mkubwa nchini, alisema msimamo wa Kamati Kuu ya CCM iliyomaliza kikao chake mjini Dodoma juzi kuhusu pendekezo hilo, una mkanganyiko mkubwa na unaonyesha wazi kwamba chama hicho hakiko tayari kukubali muundo wa serikali tatu.

Alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), jijini Dar es Salaam.

Alisema uamuzi wa CCM kuamua kuipeleka rasimu hiyo kwa wanachama wake ngazi za matawi na kuunda mabaraza ya katiba ya chama, huku wakitaka elimu zaidi itolewe kabla ya kutoa maoni, kunaleta hisia kwamba hawataki muundo wa serikali tatu.

“Msimamo wa Kamati Kuu ya CCM kidogo umenikanganya kwa upande mmoja kuna hisia kuwa CCM haitaki serikali tatu, mara tunaambiwa kwamba wananchi waelimishwe vya kutosha kabla ya kutoa maoni yake,” alisema Jaji Bomani.

Akizungumzia msimamo wake, Jaji Bomani ambaye amepata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alisema anaunga mkono uwepo wa serikali tatu kwenye rasimu ya katiba.

Alisema kuwa suala la serikali tatu limekuwa likipendekezwa na tume nyingi, lakini kila lilipofika serikalini lilikataliwa bila kujua faida zake.

Alizitaja tume hizo kuwa ni pamoja na Tume ya Jaji Francis Nyalali, Jaji Robert Kisanga na sasa Kamati ya Jaji Joseph Warioba ambazo zote zilikuja na mapendekezo hayo.

“Kila tume zimeliangalia vilivyo mpaka kufikia uamuzi huo, muundo wa serikali mbili uliopo ulibuniwa haraka haraka na waasisi wa nchi hizo mbili (Tanganyika na Zanzubar), Mwalimu Nyerere na Sheikh Amani Abeid Karume kwa hiyo lazima tubadili muundo wa Serikali ya Muungano,” alisema Jaji Bomani.

Kwa mujibu wa Jaji Bomani, uwepo wa serikali tatu unaweza kupunguza au kumaliza migogoro inayojitokeza mara kwa mara hasa upande wa Zanzibar kuogopa kumezwa.

Alisema nchi nyingi zilizounda serikali za muungano, zimeweza kuendelea kutokana na kuweka mgawanyo wa madaraka kwa kila serikali kuwa na mipaka yake.

Bomani alisema serikali tatu sio mzigo katika nchi kutokana na kuweka mifumo ambayo itakuwa imara katika kutekeleza kwa wananchi.

Alisema endapo rasimu hiyo itapita, Tanzania itakuwa na serikali tatu, yaani Tanganyika, Zanzibar na ya Muungano ambazo zitakuwa na mipaka katika mgawanyo wa kimadaraka.

“Naamini serikali tatu inawezekana, woga wa gharama za uendeshaji hauna msingi na sio mzigo kutokana mfumo huo haujaanzia hapa kwetu,” alisema Bomani.

Alipendekeza kufanyika kwa kura za maoni hasa Zanzibar ili kujua kama wanautaka muundo wa serikali tatu na kama hawautaki, uwe muungano wa aina gani.

Jaji Bomani aliibua hoja nyingine ya majina ambapo alipendekeza kuwa endapo kutakuwa na serikali tatu, Serikali ya Tanzania Bara iitwe Tanganyika na ile ya Zanzibar ibaki kuwa Zanzibar.

CHADEMA wamtega Pinda


Katika hatua nyingine, CHADEMA imemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutimiza ahadi yake ya kuleta muswada wa marekebisho ya sheria iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya ili kuepusha mkanganyiko kwenye mjadala wa rasimu iliyotolewa.

Msimamo wa kambi hiyo, ulitolewa jana mjini hapa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akisema kuwa Pinda ameshindwa kusimamia maneno yake, hivyo kuruhusu Bunge kupoteza muda wa siku tano tangu Juni 7 hadi 12 pasipo kuleta muswada huo.

“Mtakumbuka Aprili 4 mwaka huu, Kiongozi wa kambi, Freeman Mbowe katika hotuba yake kwa ofisi ya Waziri Mkuu alitangaza mambo mawili akitaka yatekelezwe, vinginevyo CHADEMA ingejitoa kwenye mchakato wa katiba mpya,” alisema.

Mnyika aliyataja mambo hayo kuwa ni kufutwa kwa mabaraza ya katiba kutokana na uchaguzi wake kugubikwa na rushwa na hila, pili ni kuletwa kwa muswada wa marekebisho ya sheria iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alifafanua kuwa hata Msemaji Mkuu kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu kwenye hotuba yake Aprili 30 mwaka huu, alisema wanaipa muda serikali ilete muswada huo kabla ya rasimu kutolewa.

“Waziri Mkuu aliahidi kutimiza sharti la pili la kuleta muswada, lakini hadi rasimu inatolewa ameshindwa kusimama katika maneno yake. Rasimu imetoka, lakini imeibua mjadala na ubovu wa mchakato ukiachwa utaathiri upatikanaji wa katiba mpya,” alisema.

Aliongeza kuwa rasimu hiyo imezua mjadala kuhusu muundo wa muungano kwa wananchi kuhoji ni kwanini rasimu inaleta muundo huo pekee pasipo kueleza mustakabali wa katiba ya Tanganyika.

Mnyika alieleza kuwa ubovu huo waliubaini mapema ndiyo maana viongozi wa chama hicho walipokutana na Rais Kikwete Ikulu mwaka jana, walimweleza kuwa sheria iliyounda tume ya katiba ibadilishwe ili hatima ya Tanganyika iingizwe kwenye mchakato ili maoni yaguse vyote kwa pamoja.

Mnyika alisema kuwa CCM wanajipanga katika mabaraza kujadili rasimu kwa vile wanajua kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo mbovu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatambua kwamba maoni yote ya mabaraza yana uzito sawa, hivyo tume inaweza kuchakachua.

Alisema CHADEMA kwa sasa hawataki kutoa maoni ya jumla kuhusu rasimu hiyo bali waipitie kwanza neno kwa neno pamoja na wanachama wao nchi nzima wakilinganisha na waraka namba moja wa mapendekezo yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya.

“Baada ya hapo, Kamati Kuu itakutana mwanzoni mwa Julai na kutoa uamuzi. Hata Bunge likimaliza muda wake bila serikali kuleta muswada huo, sisi kama kambi tutalirudisha suala hilo kwa Kamati Kuu ili kulitolea uamuzi,” alisema.

Akigusia kwa uchache maeneo yenye kasoro kwenye sheria hiyo, Mnyika alisema mamlaka na madaraka ya wananchi kwenye kura ya maoni yataporwa ikiwa Tume ya Uchaguzi inayolalamikiwa itaendelea kusimamia mchakato huo.

Pia alitaja mamlaka ya uwakilishi wa wananchi kwenye Bunge la Katiba ambalo kwa mujibu wa sheria hiyo ukiacha wabunge wa sasa, rais ndiye atateua wajumbe wengine baada ya kupokea mapendekezo ya makundi mbalimbali akisema yanapokwa.

Mbowe aitisha Kamati Kuu

Katika hatua nyingine, CHADEMA imeitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu (CC), ili kujadili na kutoa msimamo wa chama hicho juu ya rasimu ya katiba mpya, iliyotolewa hivi karibuni, huku kikiwataka wananchi wote kuendelea kuichambua kwa makini na kutoa maoni yao kwa ajili ya kuiboresha.

Chama hicho kimesema kuwa kikao cha Kamati Kuu kitafanyika Jumamosi ya wiki ya kwanza, Julai mwaka huu, ambapo kwa muda wote uliobaki kimesema kitaendelea kuichambua rasimu hiyo 'neno kwa neno' kikisema kuwa ni muhimu kufanya hivyo kwani 'shetani hujificha kwenye maelezo'.

Mbali ya kuwataka wananchi kuisoma kwa makini rasimu hiyo, chama hicho pia kimewaagiza wanachama wote nchi nzima kupitia kwenye mfumo wake wa uongozi kuanzia ngazi ya chini ambayo ni misingi katika ngazi ya vitongoji, kuichambua rasimu kwa kuzingatia waraka namba moja wa chama hicho juu ya maudhui ya katiba mpya ya Tanzania, kisha wawasilishe maoni yao ili yazingatiwe kwenye maamuzi ya kikao hicho cha Kamati Kuu.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe juzi mjini Ifakara, kwenye mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Ifakara, alipokuwa akimnadi mgombea wa chama hicho, Peter Lijualikali.

Mbowe alisema kuwa tangu Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya itoe rasimu hiyo, chama hicho hakijatoa kauli yoyote, ili kupata muda wa kuisoma na kuichambua kwa makini 'neno kwa neno' nyaraka nzima, kisha kufanya mashauriano ya kitaalamu ndani ya chama, huku kikifanya maandalizi ya vikao kwa ajili ya maamuzi na hatimaye msimamo wao kwenye hatua hiyo ya mchakato wa katiba mpya.

“Ndugu zangu wananchi wenzangu wa Ifakara, katika mkutano huu wa kampeni za kumnadi mgombea wetu, naomba pia nitumie fursa ya kutoa tamko la kitaifa kuhusu suala muhimu sana na nyeti la katiba mpya. Tangu Tume imetoa rasimu ya katiba mpya, chama chenu kimekuwa kimya, kwa maana hakijazungumza, hii ni kwa sababu kadhaa.

“Kwanza kabisa tangu siku ya kwanza hadi leo, tumekuwa tukiipitia rasimu hiyo neno kwa neno, kipengele kwa kipengele, maana wanasema 'the devil lies in the details' yaani mzimu hujificha kwenye maelezo, sasa sisi kama mnavyojua tumekuwa chanzo na chachu kubwa ya mchakato huu hadi kufikia hapa ulipo, lazima tuwe makini katika msimamo wetu kama ambavyo imekuwa mara zote.

“Ilikuwa lazima pia tufanye mashauriano, wataalamu wetu waangalie mambo yote ya kitaalamu, neno kwa neno, kisha tukae vikao na kutoa msimamo wa chama chenu. Kama mnavyojua CHADEMA si Mbowe, si Slaa, wala si mtu mwingine yeyote, chama ni vikao. Hivyo tumeitisha kikao cha Kamati Kuu siku ya Jumamosi, wiki ya kwanza ya mwezi wa saba, kisha tutatoa tamko na msimamo wa CHADEMA katika rasimu hii ya katiba,” alisema Mbowe.

Aliongeza: “Wakati tunaendelea kuipitia rasimu hii hadi Kamati Kuu ikae, tunawataka Watanzania wote waendelee kuisoma kwa makini na kutoa maoni yao, lakini pia kwa msisitizo mkubwa kabisa, tunawaagiza wanachama wote wa CHADEMA katika ngazi ya msingi, kwenye vitongoji nchi nzima kukaa vikao, kuisoma na kuichambua rasimu kwa makini, kisha watuletee maoni yao kabla ya kikao hicho ili tuyazingatie kwenye maamuzi na utoaji wa msimamo wetu kama chama.

“Tunawakata wanachama wetu kuipitia rasimu yote kwa kurejea Waraka Namba Moja wa mwaka 2013 uliopitishwa na Baraza Kuu la chama mapema mwaka huu, hasa sehemu ya pili ambayo ilikuwa inaelezea maoni ya CHADEMA juu ya maudhui ya katiba mpya ya Tanzania.”

Mbowe akirejea kwa kutoa mifano namna chama hicho kilivyosukuma agenda ya katiba mpya kwa ajili ya mabadilio ya kimfumo na kiutawala kwa muda mrefu na kuweka msisitizo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, alisema kuwa watu wengi, hasa walioko madarakani leo, waliibeza CHADEMA, lakini leo wanakubali kuwa kiliona mbali.

Akitumia kaulimbiu maarufu ya chama hicho 'nguvu ya umma', Mbowe aliwataka Watanzania kuendelea kukiunga mkono katika kusimamia na kuhakikisha nchi inapata katiba mpya, huku akisema hawako tayari kuona wakuu wa wilaya na mikoa wakiendelea kuwemo kwenye katiba mpya.

Mwisho







Tuesday, June 11, 2013

CHADEMA YAIFYATUA CCM KWA KUPATA USHINDI WA KISHINDO MKOANI RUVUMA


 Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini ya Chadema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Ruvuma Joseph Fuime akiwahutubia mamia ya wananchi wa Kata ya Mkako kwenye mkutano wa Ufungaji wa kampeni ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kitongoji  cha Masangu kijiji cha Amani Makolo, Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma
 Mgombea aliyeshinda Uenyekiti wa Kitongoji cha Masangu kijiji cha Amani Makolo, Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Nestory Komba wakati akiomba kura
 Kutoka kushoni ni Diwani wa Viti Maalum wilaya ya Mbinga Anastasia Magubike, Diwani wa Vitimaalum Manispaa ya Songea Rhoda Komba, na watatu ni Katibu wa Kanda ya Kusini ya Chadema Edmund Nditi wakifuatilia kwa makini hotuba ya Ufungaji wa Kampeni hizo juzi kutoka kwa Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini ya Chadema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Ruvuma Joseph Fuime
 Katibu wa Kanda ya Kusini ya Chadema Edmund Nditi
akiwahutubia mamia ya wananchi wa Kata ya Mkako kwenye mkutano wa Ufungaji wa kampeni zilizofanyika Kitongoji cha Masangu
 Baadhi ya Viongozi wa Jimbo na Wilaya ya Mbinga wakifuatilia Kampeni hizo juzi
Na  Stephano Mango, Songea
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)  Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma kimepata ushindi mnono kabisa kwa kukibwaga Chama  cha Mapinduzi ( CCM ) kwenye uchaguzi mdogo wa Kitongoji  cha Masangu kijiji cha Amani Makolo,Kata ya Mkako
Akitangaza matokeo hayo jana Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi huo Bahati Liholile Haule alisema kuwa wapiga kura waliojiandikisha katika uchaguzi huo walikuwa ni 110, waliojitokeza kupiga kura walikuwa 103 ambapo hakuna kura zilizoharibika
Haule alisema kuwa katika uchaguzi huo Vyama viwili vya Siasa vilisimamisha wagombea ambapo kwa Chama cha Mapinduzi ( Ccm) kilimsimamisha Alto Ngonyani kugombea nafasi hiyo na kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( Chadema) kilimsimamisha Nestory Komba kugombea nafasi hiyo ya Kitongoji
Alifafanua kuwa katika uchaguzi huo ambao ulitawaliwa na amani kubwa matokeo  ya mgombea wa Ccm yalikuwa ni kura 45 na mgombea wa Chadema alipata kura 58
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini ya Chadema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( Chadema) Mkoa wa Ruvuma Joseph Fuime alisema kuwa ushindi ulikuwa mgumu , licha ya Serikali ya Ccm kutengeneza mazingira mfu ya kujipatia ushindi lakini walishindwa na nguvu ya umma ambayo ilijikita wazi katika kampeni ya kimkakati makini wa kujipatia ushindi wa kumpata kiongozi bora
Fuime alisema kuwa ushindi huo ni salamu tosha kwa watawala wa Ccm kuwa wananchi hawaitaji maneno yenye kutia matumaini bali wanachoitaji sera stahiki za kuwaondoa katika minyororo ya maumivu ya maisha kutoka na gharama za uendeshaji wa maisha yao kupanda
Alifafanua kuwa Mkoa wa Ruvuma umejaliwa kuwa na Rasilimali nyingi sana ikiwemo Makaa ya Mawe yaliyopo mita chache kutoka ambapo uchaguzi umefanyika lakini Rasilimali hizo zimekuwa hazitumiki kuwanufaisha wananchi wake
Alisema kuwa wanaonufaika na Rasilimali hizo ni Viongozi wa kifisadi wanaotokana na Ccm akiwamo Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mashariki Gaudence Kayombo na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga na ushahidi upo wazi ukifika katika Ofisi ya Mwenyekiti wa Kijiji,Mwenyekiti wa Kitongoji au Kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Mkako
Alifafanua kuwa ukifika kwenye ofisi hizo utakutana na saini zao hapo na ujumbe wao ambao una malengo yenye utata dhiti ya maeneo ambayo yana Rasilimali muhimu ambazo zingetumika vizuri zingeweza kusababisha wananchi waishi maisha ambayo Mungu anayapenda
“Ukifika katika Ofisi hizo utakuta Viongozi hao wametembelea Ofisi hizo mara nyingi kuliko maeneo mengine ambayo yana kabiliwa na changamoto nyingi na wananchi wanawahitaji kwa ajili ya kuwaongoza katika kutatua shida  zao lakini cha ajabu huwa awatembelei maeneo hayo mpaka muda wao wa Uongozi unakwisha
Mwenyekiti huyo alimalizia kwa kusema kwa nafasi hiyo anawashukuru wananchi kwa kutambua sera nzuri ambazo zinapaswa kutekelezwa na Kiongozi mzuri na pia kwa kupuuza ghiriba zilizo zeeka za Ccm na kutoa ujumbe kwa watawala katika chaguzi za kuelekea mwaka 2014 na 2015 ili kuleta matumaini na mustakabari mpya wa Taifa salama
MWISHO
 

Stephano Theofrida Mango 
 P.O.BOX 835, SONGEA, RUVUMA- TANZANIA.
SIMU: 0755-335051, 0715-335051, 0784-335051, 0778-335051,
 E-MAIL;stephano12mango@yahoo.com  www.stephanomango.blogspot.com

Thursday, June 6, 2013

MFEREJI WATAFUNA MAMILIONI YA FEDHA NA BADO HAUJAKAMILIKA


Na Mwandishi Wetu, Namtumbo
MFEREJI  wa maji uliojengwa kwa  fedha za Serikali kwa  ajili  ya  kilimo  cha  umwagiliaji katika  Kijiji cha Namahoka Kata  ya  Ligera Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma wadaiwa umesombwa  na  maji ya  mvua iliyonyesha  hivi karibuni.
Mwenyekiti wa kikundi  cha Songambele kinachojengewa mradi  huo, Gaudens  Komba amesema kuwa mfereji huo umesombwa  na  maji kutokana na tuta lililowekwa na Mkandarasi kukinga mfereji  huo lilikuwa dogo na baadhi  ya  sehemu  ya  mfereji  huo zilititia.
Komba alisema kuwa hiyo ni  mara  ya pili sasa  kwa  mfereji huo  kutokea  dosari kwani mwaka 2007 mwezi mei  Serikali  ilitumia shilingi milioni 67 kujenga mfereji  huo chini  ya  kampuni ya Legele civil works iliyokuwa  ikimilikiwa na Dastan  Mtembele ambapo kabla ya kukamilika kwake mfereji  huo ulititia na  kushindwa kupitisha maji kwenda  mashambani.
Aliongeza kuwa pamoja na  hayo Serikali ilitenga tena fedha kiasi cha milioni 297 kwa  ajili  ya kufanya marekebisho ya  mfereji huo kwa kuipatia  tenda kampuni ya Modspan chini ya usimamizi  wa Ernest  Mbawa kufanya kazi ya  kuurekebisha mfereji  huo ambapo mpaka  sasa kampuni  hiyo imelipwa milioni 83 na baadhi ya sehemu iliyofanyiwa marekebisho imesombwa na  maji na zingine kutitia.
Fundi mkuu msaidizi anayejenga mfereji huo Shafii  Magoto alisema  kuwa sehemu iliyosombwa  na  maji imetokana na mkandarasi kuweka tuta dogo la  kukinga mfereji huo na kuruhusu maji ya mvua kusomba tuta hilo kiurahisi na kuufanya mfereji huo kuvunjika.
 Hata hivyo Magoto alisema  kuwa ujenzi wa mfereji huo umesimama kwa muda wa miezi sita sasa kutokana na wao kutolipwa fedha yao kutoka kwa mwajiri wao Ernest Mbawa na wanaishi katika mazingira magumu na wanashindwa kurudi kwao kutokana na kukosa  fedha za  kurudia na  hivi sasa wanajikita katika kufanya  kazi binafsi  ili kujipatia fedha  ya kula .
 Mkandarasi Mbawa kwa  upande wake anawalalamikia viongozi wa kikundi cha Songambele  kwa kumcheleweshea kumwizinishia kuchukua fedha kwa wakati ili aendelee kujenga mfereji  huo na badala  yake viongozi hao hupenda  kuendeleza malumbano na kuingiza  migogoro isiyokuwa ya lazima na kutumia muda mwingi kushughulikia migogoro inayoibuka kila  kukicha ndani ya kamati.
Mbawa aliwataka viongozi wa kamati kumwizinishia fedha ili arekebishe sehemu iliyosombwa na maji ya mvua na kuwalipa mafundi wake na waendelee na kazi.
Baadhi ya wanakikundi wakiwemo Mohamedi Mangambila  na Mohamedi Akida waliuambia mtandao huu kuwa wamechoshwa na utendaji kazi wa Mkandarasi huyo walidai kuwa wataandika barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri  ya Wilaya ya Namtumbo kuomba kusimamisha mkataba wake kwa hoja ya kushindwa kujenga mradi huo kwa wakati kuendelea kujenga mradi huo nje ya mkataba na pia mkandarasi  kutokuwa na mahusiano mazuri na kamati.
Mhandisi wa halmashauri  ya wilaya ya Namtumbo Izakiel Nyirenda amethibitisha kuwepo na mgogoro katika mradi huo na kusema kuwa sababu kubwa inayofanya mradi huo kuyumba ni viongozi wa kikundi kuiona fedha katika mradi huo ni  kubwa na kwa namna fulani wanataka nao wapate mgao hali inayopelekea kuwepo na migogoro katika mradi  huo kila kukicha na mkandarasi kulazimika kutofanya kazi kwa muda mrefu na kutotaka  kumwizinishia fedha iliaendelee kujenga mradi  huo.
Nyirenda alidai kuwa sehemu ilisombwa  na maji inarekebishika kwa haraka na kuruhusu maji kupita kama kawaida licha ya wanakikundi hao kutomtaka Mkandarasi huyo kwani  wanakikundi wenyewe ndio waliopendekeza jina la Kampuni ya MODSPAN Inayosimamiwa na Ernesti Mbawa kujenga mradi huona kuziacha kampuni zingine nne zilizoomba kujenga  mradi  huo alisema  nyirenda.

Kampuni ya MODSPAN ilisaini mkataba wa miezi sita toka tarehe30 mwezi  novemba mwaka 2011 wa kurekebisha mfereji huo ambapo mpaka mei 2012 mkataba wake uliisha na wanakikundi inaonesha wazi hawakuridhika na utendaji kazi wa mkandarasi huyo na walifia uwamuzi wa kumwandika barua mkurugenziwa halmashauri  ya wilaya hiyo ya kutaka kumsimamisha mkandarasi huyo na ndipo mgogoro ulipoanzia na mradi huo  ukasimama  mpaka hivi sasa. Mradi wa ujenzi wa mfereji huo umesimamisha kilimo cha umwagiliaji katika eneo hilo na kuwaacha wananchi kuziba mito kienyeji na kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa kujichimbia mifereji  yao   wenyewe  na   kuendesha  shughuliza  kilimo cha umwagiliaji.
Hata hivyo mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Steven  Nana alipohojiwa na Mtandao huu kuhusiana na mgogoro  wa mradi huo wa kilimo cha umwagiliaji alikili kuwa matatizo yapo lakini hawezi kuelezea lolote mpaka awepo ofisini kwake ambako angedai kuwa angeweza kupata ufafanuzi mzuri kutoka kwa maafisa wake wa kilimo  na si vinginevyo.
MWISHO