Na Stephano Mango,Songea
KAMATI ya siasa ya Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma imeifuta adhabu iliyopendekezwa na kutolewa na Kamati ya siasa ya chama hicho Wilaya ya Songea Mjini ya kuwafukuza uanachama Madiwani wake wa tano kwa kile alichojiita ukosefu wa maadili walioufanya wakati wa uchaguzi wa kumpata Meya wa Manispaa ya Songea uliofanyika hivi karibuni
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za chama hicho mkoa wa Ruvuma Katibu wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma Emmanuel Mteming’ombe alisema kuwa kamati ya siasa ya mkoa baada ya kuyapitia maelezo yaliyotolewa na kamati ya siasa ya Wilaya ya kuwafukuza Madiwani hao na baada ya kupitia kwa umakini maelezo ya utetezi ya Madiwani waliofukuzwa uanachama na kamati ya siasa ya Wilaya kamati ya siasa ya mkoa imelitengua pendekezo la adhabu hiyo kutokana na kutokuwa na hatia
Mteming’ombe alisema kuwa Kamati ya siasa ya mkoa imewaruhusu madiwani wale watano kuendelea na uanachama na udiwani wao kama ilivyokuwa awali na kwamba chama hicho kimesikitishwa sana na vurugu zilizojitokeza katika mkutano wa Baraza la Madiwani wa kumchagua Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Septemba 23 mwaka huu
“Chama kinakemea na kulaani tabia hiyo ya kufanya vurugu katika vikao kwani tabia ya kufanya vurugu vikaoni ni kinyume kabisa na kanuni za vikao na kwamba sio tabia za viongozi wanaotokana na Ccm hivyo chama kimeamua kuandaa semina kwa Madiwani wote wanaotokana na Ccm ili kuwaelekeza na kuwaelimisha kwa lengo la kuwapatia weledi juu ya namna bora ya kusimamia na kufuatilia utekelezaji na utendaji mzuri wa kazi zao”alisema Mteming’ombe
Hivi karibuni Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Songea kilipendekeza kuwafukuza uanachama Madiwani wake watano kutokana na kuungana na Madiwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)kwa kumpigia mgombea pekee Diwani wa Kata ya Matogoro kura 14 za hapana na za ndiyo 12 katika uchaguzi wa Umeya wa Manispaa ya Songea
Hali hiyo ilisababisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambaye ndiye Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Songea Mjini Nachoa Zakaria kushindwa kuyatangaza matokeo hayo na kumpa Naibu Meya Mariam Dizumba ambaye naye alikuwa ni miongoni mwa wapiga kura kuyatangaza matokeo hayo kinyume kwa kusema kuwa Mhagama amepata kura 14 za ndiyo na za hapana 12 na kusababisha vurugu kubwa na mkutano kuvunjika kutokana na ukiukwaji huo wa kanuni wa makusudi
Kutokana na hali hiyo Ccm Wilaya ya Songea mjini ikapendekeza Madiwani watano akiwemo Faustine Mhagama wa Kata ya Mshangano,Kurabest Mgwasa wa Msamala,Christian Matembo wa Seed Farm,Victa Ngongi wa Ruvuma na Genifrida Haule wa Viti Maalum wafukuzwe uanachama kutokana na kukizalilisha chama kwa kumpigia kura za hapana Charles Mhagama
MWISHO
No comments:
Post a Comment