WANAWAKE NA UFANYAJIKAZI ZISIZO TIMILIFU MIAKA 50 YA UHURU
Na,Stephano Mango,Songea
WANAWAKE wengi nchini wamekuwa wakifanya kazi ama za kuajiriwa au za kujiajiri wenyewe ambazo hazina staha au sio timilifu kutokana na mifumo mibovu ya ufanyaji kazi hizo kwa sababu ya ugumu wa maisha unaowakabili
Wakina mama hao wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mbalimbali na kushindwa kumudu gharama za maisha
kama vile matibabu,ukosefu wa makazi,elimu na huduma nyinginezo muhimu za kijamii
Hali hiyo hupelekea wanawake wengi kutafuta kazi ili waweze kuzifanya licha ya kuwa sio timilifu na hazina staha ili waweze kujipatia fedha za kujikimu na kupunguza ukali wa maisha unaowakabili katika maeneo
yao
Licha ya kufanya kazi hizo
kama vile kufagia barabarani,kutengeneza bustani katika maeneo ya miji,kupika mama lishe,kupita kwenye majumba ya watu na kuomba kusafisha vyombo au kufua nguo na kazi zinginezo wamekuwa wakidhurumiwa kupata ujira wao
Aisha Abdalah mwenye umri wa miaka 55 mkazi wa kata ya Ruvuma Halmashauri ya Manispaa ya Songea anasema kuwa mme wake alifariki mwaka 1997 na kumuachia watoto wawili wa kike ambapo kwa sasa anawajukuu 6 kutoka kwa watoto wake hao ambao wanamtegemea
Abdalah anasema kuwa watoto wake wameshindwa kumletea huduma muhimu kwa mahitaji yake na ya wajukuu zake ambao amepewa jukumu la kuwalea bila kuwa na kipato chochote kile hali ambayo inamuongezea ukali wa maisha zaidi
Alisema kuwa wajukuu hao wanne wanasoma katika shule ya msingi Mburani iliyoko katika kata hiyo ya
Ruvuma lakini mara nyingi watoto hao wamekuwa wakishindwa kuendelea na masomo kutokana na ukosefu wa michango mbalimbali katika shule hiyo ukiwemo mchango wa ulinzi
“Watoto hao mara nyingi wamekuwa wakila mara moja kwa siku tena chakula ambacho kwa kweli kinakatisha tamaa hata kukiangalia lakini tunalazimika kula kwa sababu hamna njia nyingine ya kusogeza siku za kuishi duniani”alisema Abdalah kwa uchungu mkubwa
Kutokana na ugumu huo wa maisha aliradhimika kutafuta kazi katika mashine za kukoboa mpunga wa wafanyabiashara mbalimbali na kubahatika kupata kazi hiyo na kupangiwa siku maalum ya kuanika mpunga,kutandaza,kuanua na kuupeleka mashine kwa ajili ya kuukoboa
Alisema kuwa katika kazi hiyo licha ya kuwa sio timilifu amekuwa akiifanya kwa zamu kutokana na wanawake wengi kuifanya kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili katika familia zao
Alieleza zaidi kuwa kazi hiyo wakati mwingine inakuwa mara moja kwa wiki kutokana na kuwekeana zamu ya kufanya shughuli hiyo kwani wakina mama wengi wamekuwa wakiifanya kutokana na ukosefu wa ajira timilifu
Alifafanua zaidi kuwa ujira wanaoupata katika kazi hiyo ni kuzoa pumba za mpunga na kuweka kwenye mifuko kwa ajili ya kwenda kuzipepeta ambapo wanapata chenga za mchele ndizo zinakuwa
kama mshahara wao
“Maisha tunayoishi yanakatisha tama kabisa lakini hatuna jinsi……tunaanika mpunga wakati mwingi siku mbili ili ukauke kulingana na uwepo wa jua,tunauanua na kuupeleka mashine halafu tajiri anatupa ujira wa kuzoa pumba ili tuweze kupata chenga za kwenda kupika”alisema Abdalah
Alisema kuwa wanapopepeta pumba hizo bila kuwa na vikinga fumbi hulazimika kupata mafua na kukohoa kila mara kutokana na kuvuta hewa iliyochanganyika na pumba laini hali inayopelekea mara nyingi kuugua na kupona bila kupata tiba
Alieleza zaidi kuwa akibahatika kuzoa angalau gunia tatu za pumba na kuzibebelea huku akiwa na njaa kali kuzipeleka eneo la bonde la Bombambili ambako ndio kunakofanyika shughuli hiyo ya kupepeta hupata walau robo tatu kilo ya chenga hizo
Alieleza kuwa kiasi hicho huenda nacho nyumbani kukipika na kula na wajukuu wake kwa milo mitatu ya siku tatu kwa kipimo cha robo kwa mlo wa siku ya kwanza.siku ya pili tena robo na siku ya tatu robo
Alisema kuwa endapo siku nyingine anapopata kilo moja au mbili za chenga hulazimika kiasi kingine kuuza kwa wapikaji wa vitumbua ambapo hujipatia fedha za kununua mafuta ya taa,kupaka,mboga na sabuni
Alifafanua analazimika kupunguza mlo ili aweze kufanikisha pia mambo mengine ya kifamilia kwani wakati mwingine wajukuu wake wanaumwa homa ambazo haziwezi kupona bila kupata angalau nusu dozi ya dawa za hospitali
“Namshukuru mungu kwani mara nyingi nimekuwa nikipata homa ndogo ndogo ambazo kutokana na ugumu wa maisha zimekuwa zikipona zenyewe bila kupata matibabu yoyote yale lakini wajukuu wangu wamekuwa wakinyemelewa na magonjwa mbalimbali ambayo mengine wanapona kutokana na dawa za asili na mengine kwa dawa za hospital”alisema Abdalah
Wanawake wengi wamekuwa wakiishi kwa kuhurumiwa na wasamaria wema na wengine wamekuwa wakipambana hivyo hivyo na ugumu wa maisha bila mfumo waliouchagua na kuwaahidi ahadi za maisha bora
Wakati taifa linaelekea kuadhimisha sherehe za miaka 50 ya uhuru tunapaswa kujiuliza ni nani atakayewapa au kuwatengenezea nguvu wanawake waweze kuikabili serikali
yao kuanzia ile ya kijiji hadi taifa katika kuweka mizania sawa ya matumizi ya rasilimali za nchi ili ziweze kuwanufaisha watu wote
Ili waweze kupata huduma muhimu za afya,maji,elimu,miundombinu na huduma nyingine stahiki za kijamii kwani jambo hilo kwa kushirikiana na mashirika ya kutetea haki za kijinsia TGNP,FemACT inawezekana kufikia hatua stahiki kwa ustawi wa makundi yaliyo pembezoni
Nilazima kuwe na mfumo mzuri wa kuyafikia makundi hayo kwa kutumia rasilimali za taifa ili kujua kila kinachowatatiza ili kuweza kuwajengea uwezo wa kimaamuzi,kufahamu haki zao na kuweka nguvu ya pamoja ya kiukombozi
Kwa lengo la kujitetea,kudai haki,kujilinda dhidi ya mifumo onevu katika itikadi,dini,kabila na jinsia ili kujenga agenda ya kimaisha kulingana na mazingira ya eneo ambalo mtu anaishi na mahitaji yake kwa ujumla
Wakati taifa likiadhimisha miaka hiyo ya uhuru na Mtandao wa Jinsia
Tanzania kuadhimisha Tamasha la Jinsia 2011 tunapaswa tutafakari kwa umakini changamoto zinazowakabili wanawake na makundi yaliyopo pembezono ili tuweze kujenga suluhisho la kitaifa
Kwasababu miaka 50 ya uhuru inatukumbusha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika kurekebisha sheria,sera,mifumo,mienendo na utekelezaji wa mambo mbalimbali ya maendeleo ili kureta mabadiliko chanya huko tuendako
Ili kuweza kuweka jitihada hizo kwenye mizania sawa na kuleta mabadiliko chanya katika sekta zote na makundi yote kufaidi rasilimali za taifa hili kongwe kiumri lenye umaskini mkubwa licha ya rasilimali kuzagaa kila eneo kuna hitaji nguvu za pamoja ambapo tumeamua kuthubutu,tunaweza na tuzidi kusonga mbele
Mwandishi wa Makala haya
Anapatika simu 0755-335051
Baruapepe;stephano12mango@yahoo.com