About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Tuesday, January 31, 2012

VIONGOZI WA UWT WATAKIWA KUWASHIRIKISHA WANACHAMA KATIKA CHAGUZI ZAKE

                        KATIBU WA UWT MKOA WA RUVUMA MARIAM YUSSUF
Na Stephano Mango,Songea
WATENDAJI na viongozi wa Jumuiya ya Wanawake ya Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma wametakiwa kuwahamasisha na kuwashirikisha kikamilifu wanachama wa Jumuiya hiyo iliwaweze kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama
Wito huo umetolewa jana na Katibu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania(Uwt) Mkoa wa Ruvuma Mariam Yussuf wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake kuhusu mchakato wa uchaguzi wa Jumuiya za Chama cha Mapinduzi
Yussuf alisema kuwa viongozi wa Uwt  kupitia vikao halali vya Jumuiya wanapaswa kuwahamasisha wanachama kushiriki katika uchaguzi kwa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwani wanawake wanaweza hata bila kuwezeshwa
Alisema kuwa wanachama wanatakiwa waendelee kuhudhuria vikao na mikutano inayowahusu ili kuweza kutumia haki stahiki ya kidemokrasia kwa kuomba kuchaguliwa au kuchagua viongozi bora watakaotuvusha wakati huu mgumu
Alieleza kuwa Jumuiya ya Uwt tayari imeshawatangazia wanachama wake utaratibu wa uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi za uongozi kuanzia ngazi za matawi,kata,wilaya,mkoa na Taifa ili wale wenye sifa za uongozi waweze kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi
Alieleza zaidi kuwa wanaotaka uongozi ni vema wasifanye kampeni kabla ya wakati kwa kuanza kurushiana maneno machafu,kwa kutoa rushwa kwani kwa kufanya hivyo kutasababisha kuleta uadui na ustawi wa jamii na jumuiya ya Uwt na Ccm kwa ujumla hivyo tuepukane na vitendo hivyo
MWISHO

WAKULIMA SONGEA WATAKIWA KULIMA KWA WINGI NA KWA KUZINGATIA KANUNI BORA ZA KILIMO


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu akiongea na watendaji wa vijiji vya Magagula.Muungano Zomba na Lugagara wilaya ya Songea jana alipotembelea kuhamasisha wakulima kuzalisha mahindi kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo.Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Sabaya(kulia) na mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea Rajab Mtiula(Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma)




Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu (mwenye kaunda suti nyeusi) akisikiliza maelezo ya kilimo kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Songea Thomas Sabaya (kulia) wakati wa ziara ya kukagua usambazaji wa pembejeo kijiji cha Lugagara wilaya ya Songea


Wakulima wa kijiji cha Magagula wilaya ya Songea wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu (hayupo pichani) jana alipofanya ziara ya kukagua shughuli za kilimo
Na Revocatus A.Kassimba,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
SERIKALI imewataka wakulima  mkoani Ruvuma kulima kwa wingi mahindi katika msimu huu kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo licha ya changamoto za soko lililowakabiri msimu wa kilimo uliopita.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu wakati wa ziara yake katika vijiji vya Magagula, Lugagala na Muungano Zomba vilivyopo wilaya ya Songea .
Mwambungu aliwaeleza wananchi kuwa serikali inatambua kero ya ununuzi wa mahindi iliyotokea msimu wa 2011/2012 ambapo wakulima wengi walichelewa kupokea fedha zao kutoka Wakala wa Hifadhi za Chakula (NFRA).
Aliongeza kusema kuwa changamoto ya fedha za wakulima hazitajitokeza tena msimu ujao kwani tayari serikali imejiandaa kwa kutengwa fedha katika bajeti ili kuhakikisha mahindi yote yatanunuliwa kwa wakati.
“Limeni kuliko mwaka jana kwani serikali imejipanga kununua kwa wakati na kuhakikisha kuwa hakuna mkulima atakayecheleweshewa malipo na serikali” alisema Mwambungu na kuongeza kuwa hakuna mkulima sasa anayeidai serikali wote wamelipwa.
Mkuu wa mkoa Mwambungu alisisitiza kuwa serikali inafanya kila linalowezekana kuondoa kero ya kukopa mahindi ya wakulima hivyo ni vema wakulima wakaendelea kuunga mkono juhudi hizi za serikali kwa kuongeza uzalishaji.
Katika msimu 2011/2012 wa kilimo kwa mujibu wa taarifa za Wakala wa Hifadhi ya Chakula jumla ya tani 50,018 za mahindi zimenunuliwa kutoka kwa wakulima mkoani Ruvuma zenye thamani ya shilingi bilioni 17.5 ambapo kilo ilinunuliwa kwa shilingi 350.
Mkuu wa Mkoa alitumia fursa hiyo kuwapongeza wakulima wa vijiji hivyo alivyovitembelea kwa kutumia vema pembejeo za ruzuku kwa mfumo wa vocha kwani wameongeza uzalishaji wa mahindi na kuifanya wilaya ya Songea kuongoza katika kuzalisha mahindi mkoani.
Ziara ya Mkuu wa mkoa ilihusisha pia kukagua zoezi la ugawaji wa vocha za pembejeo ambapo kwa mujibu wa taarifa ya iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Songea Thomas Sabaya alisema wilaya imepata mgao wa vocha 64,417 ambazo zimesambazwa kwa wakulima.
Sabaya alisema vocha hizo zinahusisha mbegu bora za mahindi, mbolea ya kupandia na mbolea ya kukuzia ambapo bei ya mfuko wa mbolea ya kupandia (DAP) inauzwa shilingi 80,000/=huku mkulima akichangia shilingi 52,000/=.
Kuhusu mbolea ya kukuzia (UREA) mfuko unauzwa shilingi 72,000/= na mkulima anachangia shilingi 52,000/= huku serikali ikilipia zinazobaki na kwa mbegu bora mfuko unauzwa shilingi 40,000/= huku mkulima akichangia 20,000/= na serikali zinazobakia.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lugagara Bi Taifa Mahundi katika risala yake alisema wakulima wana changamoto kubwa ya upungufu wa vocha za ruzuku hivyo akaiomba serikali kuongeza mgao kwa kijiji.
Mkuu wa mkoa akijibu hoja hiyo aliwafahamisha wananchi kuwa vocha zinazotolewa ni vigumu kufanana na idadi ya wakulima kwani hiyo ni ruzuku itolewayo na serikali kuwasaidia wakulima kujenga uwezo wa kujitegemea.
Katika msimu huu wa kilimo mkoa wa Ruvuma umepatiwa vocha za ruzuku ya pembejeo za kilimo 192,000 ambapo kwa mwaka uliopita ulipatiwa vocha 204,000 hivyo kuwa na upungufu wa vocha 12,000/=.
Mkoa wa Ruvuma ni kati ya mikoa sita maarufu kwa uzalishaji wa mahindi nchini ambapo mikoa mingine ni Iringa, Mbeya, Rukwa, Kigoma na Morogoro.
…………………………………………………………………………………………………
Revocatus A.Kassimba
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma

WAKAMATWA NA KILO 350 ZA BANGI NA KILO 112 ZA MBEGU ZA ZAO HILO

KAMANDA WA POLISI MKOA WA RUVUMA MICHAEL KAMUHANDA

Na, Mwandishi Wetu,Tunduru

KIKOSI maalumu cha Oparesheni zuia uharifu cha Polisi Wilayani
Tunduru Mkoani Ruvuma kimewakama watu watatu kwa tuhuma za kukutwa na kilo 350 za bangi zikiwa tayari kwa ajili yakusafilishwa na kusambazwa sehemu mbalimbali za masoko ya walaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa
tukio hilo limefanikiwa kufuatia taarifa zilizotolewa na raia wema na kufanikisha kuwanasa watu hao ambao miongoni mwao yumo mtuhumiwa wa usambazaji wa madawa hayo katika sehemu mbali mbali za vijiji vilivyopo Wilayani humo.

Kamuhanda alisema kuwa Sambamba na tukio hilo pia watuhumiwa hao walikutwa na kilo 112 za mbegu za bangi ambazo zinadaiwa pia zilikuwa katika harakati za kusafirishwa zikiwa ni juhudi za wakulima wa zao hilo kujidhatiti hasa kipindi hiki
cha kilimo ili kukidhi mahitaji ya soko lao.

Kamanda Kamuhanda aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Adam Mkwanda
(33), Mkwanda Said (29) wakulima wakazi wa Kijiji cha Mpanji Wilayani humo pamoja na Mfaume Alli Mpwanda mnunuzi na msambazaji wa Bangi mkazi wa Kijiji cha Mchoteka Wilayani hapa.

Kamuhanda alifafanua kuwa katika tukio hilo watuhumiwa hao walikutwa wakiwa wamehifadhi shehene hiyo ya bangi katika maghala ya kuhifadhia chakula kukiwa na viroba 6 vilivyo kuwa vimejazwa madawa hayo vikiwa tayari kwa ajili ya kusafirishwa.

Kufuatia hali hiyo kamanda kamuhanda akatumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi kulisaidia jeshi hilo kutoa taarifa za matukio ya uhalifu na kwamba hivi sasa wamejipanga kuhakikisha watoa taarifa wanalindwa zikiwa ni juhudi za kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya elimu ya ulinzi shirikishi yanayotolewa na jeshi hilo.

Alisema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakama baada ya kukamilika kwa tatratibu za upelelezi ili sheria
iweze kufuata mkondo wake.

Wakati hayo yakijiri uchunguzi unaonesha kuwa wakulima wengi Wilayani humo wamekuwa wakishawishika kulima zao hilo kutokana na kivutio cha bei ambayo hutolewa na wafanyabiashara wake huku kukiwa na wimbi kubwa la ongezeko la watumiaji wa madawa hayo ambayo hudaiwa kuwapatia stimu.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo Debe moja la bangi linauzwa kati ya Tsh.20,000/= na 30,000/=  ikiwa ni tofauti na Bei ya mahindi ambayo debe moja hivi sasa linauzwa kwa bei ya 7,000/=.

Mwisho

WAKULIMA WA KOROSHO WATAKIWA KUWA NA SUBIRA WAKATI SOKO LA MAZAO YAO LINATAFUTWA

   MKUU WA MKOA WA RUVUMA SAID MWAMBUNGU

Na Augustino Chindiye,Tunduru

WAKULIMA wa Korosho Nchini wametakiwa kuwa na subira wakati serikali ikiendelea kutafuta suluhisho la kudumu la upatikanaji wa soko la uhakika wa zao

Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said
Mwambunmgu wakati akiongea na Madiwanai wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mkoani humo na kuongeza kuwa hali hiyo imetokana na Serikali kubaini tatizo la ubabaishaji wa Soko la Mazao hayo katika msimu wa Mwaka 2011/2012 hali inayo tishia wakulima kupata malipo ya pili.

Sambamba na ahadi hiyo pia Mkuu huyo wa Mkoa wa Ruvuma amewaahidi wakulima wa mazo hayo kuwa kauli ya serikali juu ya Suluhisho la kupatikana kwa Soko la uhakika litatolewa katika kikao kitakachoketi February 2 Mwaka huuu Mjini Dodoma  na kuwahushisha Wakuu wa Mikoa Mitano inayao lima Korosho nchini.

Akifafanua taarifa hiyo Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa kikao hicho ambacho Mgeni Rasmi atakuwa Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Prof.Jumanne Maghembe, Pia kitawahusiha Maafisa Kilimo wa Mikoa na Wilaya husika, wadau na viongozi wa vyama vya Ushirika katika Wilaya na Mikoa hiyo.

Mwambungu aliitaja Mikoa itayaohusika katika Mkutano huo kuwa ni
Ruvuma, Mtwara, Lindi,Pwani na Morogoro ambayo alidai kuwa pamoja nautekelezaji wa majukumu yao ya kawaida pia kwa pamoja wameapa kutolifumbia macho suala la ubabaishaji wa soko la mazao hayo kutoka kwa wakulima zikiwa ni juhudi za kuwarudishia ari wakulima baada ya kuhakikishiwa upatikanaji wa soko la mazao yao.

Kufuatia kuyumba kwa soko la zao hilo Mkuu wa Mkoa huyo akatumia
nafasi hiyo kuwataka viongozi wa Wilaya ya Tunduru kubuni mikakati mbalimbali ya kuwainua wananachi kwa kuwahimiza Wakulima kulima kwa wingi za la Mpunga na kulitumia kwa chakula na Biashara likiwa ni mbadala wa zao la Korosho.

Alisema Wilaya ya Tunduru ambayo ni kati ya Wilaya tano zilipo Mkoa Ruvuma ni tajiri wa rasilimali ardhi ambayo imesheheni Mito na mabonde yanayo tiririsha maji kipindi cha mwaka mzima na kwamba endapo viongozi watajipanga vyema katika kuwawezesha wakulima kwa kuwawekea miundombinu ya uhakika wataweza kuwaondoa katika mawazo mgando ya utumwa wa kutegema zao moja tu ambalo linaonekana kubezwa na walaji wakati huo wakiwa na mahitaji nalo.

Nao Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Madaha na Mkurugenzi mtendaji
wa Halmashauri hiyo Efraemm Ole Nguyaine walisema kuwa pamoja na
maandalizi ya miundombinu inayoendelea kutekelezwa pia Wilaya hiyo imekwisha jenga Skim 4 za umwagiliaji imenunua matrekta madogo zaidi ya 200 na kuyasambaza katika vikundi vijijini zikiwa ni juhudi za dhati katika utekelezaji wa kauli mbiu ya Kilimo kwanza.

Kwa upande wao baadhi ya Madiwani ambao walitaka majina yao yasitajwe gazetini ambao mbali na kukiomba kikao hicho kutoa kauli yenye maslahi kwa Wakulima walionesha mashaka
makubwa kuwa kikao hicho si lolote kwa madai ya kuwepo kwa fufunu za wanunuzi “kuiweka” kiganjani Serikali hali inayo wafanya kuwa na kiburi cha kuiyumbisha watakavyo huku viongozi wake wakishindwa kutoa kauli.
Mwisho

Saturday, January 28, 2012

MADIWANI MKOANI RUVUMA WAMETAKIWA KUSIMAMIA KIKAMILIFU MGAO WA PEMBEJEO ZA RUZUKU

                           Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu
Na Revocatus Kassimba ,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma
MADIWANI mkoani Ruvuma wametakiwa kutumia madaraka waliyonayo kuhakikisha wananchi walengwa wananufaika na mgao wa pembejeo za ruzuku  kwa njia ya vocha znzazotolewa na serikali zinafika kwa wakati na hakutokei udanganyifu.
Rai hiyo imetolewa jana  na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la madiwani katika Halmashauri hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Klasta Mlingoti wilayani Tunduru
Mwambungu aliwaambia madiwani kuwa wao ndio wenyeviti wa kamati za maendeleo za kata hivyo ni muhimu wakashirikiana na serikali katika kuhakikisha walengwa wa kunufaika na pembejero za ruzuku za kilimo wanapata kupitia taratibu zilizowekwa.
“Nawaombeni sana madiwani tumieni nafasi zenu kuhakikisha vocha zinagawiwa kwa walengwa’ alisema mkuu wa mkoa na kuongeza kuwa lengo kuu la serikali ni kuwajengea uwezo wakulima kuzalisha kwa wingi na kwa ubora mazao yao.
Alisema kuwa serikali haitamwachia yeyote yule atakayekwenda kinyume na zoezi la vocha za pembejeo kwani hizi ni fedha za umma hivyo ni budi wananchi wakapatiwa ili zisaidie kuongeza uzalishaji wa mazao na kujihakikishia uhakika wa chakula.
Mwambungu alisisitiza juu ya mtendaji au wakala wa pembejeo za ruzuku atakayebainika kuchakachua vocha kuwa hatua za kisheria za kuwafikisha katika vyombo vya sheria zitachukuliwa mara moja
Katika msimu huu wa kilimo zaidi ya wakulima laki moja na tisini watanufaika na pembejeo za ruzuku za kilimo zikiwemo mbegu bora za mahindi,mpunga, mbolea ya kupandia na kukuzia katika mkoa wa Ruvuma.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka madiwani wa halmashauri ya Tunduru kuhamasisha wakulima kuzalisha zao la mpunga ambalo linastawi kwa wingi wilayani humo ili liwe zao mbadala la biashara badala ya kutegemea korosho pekee.
Alisema hivyo kutokana na suala la soko la korosho za wakulima kuendelea kuzorota na kusababisha kero hivyo akawaasa kutumia skimu za umwagiliaji maji zilizopo wilayani humo kuzalisha mpunga huku serikali ikiendelea kutafutia suluhu ya soko la korosho hapa nchini.
“Tunaweza kutumia mpunga miaka ijayo kama zao la biashara hivyo tuwahamasishe wakulima kulima sambamba na korosho” alisisitiza Mwambungu

Na Revocatus Kassimba
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma

KIKAO CHA MAANDALIZI YA MASHINDANO YA SANGA ONE CUP KIMEANZA MCHANA HUU

Kutoka kushoto ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Sufa Mshamu Mkuruma,Adimu Rader
Kutoka kushoto ni Katibu Msaidizi wa Chama cha Mpira wa miguu Manispaa ya Songea Godfrey Mvula,wa pili ni Katibu wa Kamati ya Ufundi SUFA Francis Kasembe,Kumburu Laukila,Shaibu Mambo
Katibu wa Chama cha Mpira wa miguu Manispaa ya Songea Ajaba Chitete


KAMATI MASHINDANO YA SANGA ONE CUP KUZINDULIWA MCHANA HUUUUUUUUUUU

Na Stephano Mango,Songea
KAMATI ya kuandaa na kusimamia Mashindano  ya Sanga One Cup kuzinduliwa mchana huu katika viwanja vya Sanga One Bombambili
Akizungumza na Mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com, Diwani Mstaafu wa Kata ya Bombambili na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu ambaye pia ni mdhamini wa mashindao hayo Golden Sanga (Sanga One) alisema kuwa tayari wajumbe hao wamepatikana ambao watafanya uchaguzi mdogo ili kuweza kuwapata viongozi wake
Sanga alisema kuwa kazi yao kubwa itakuwa ni kuandaa mashindao hayo na kusimamia mashindano hayo kwa haki na usawa ili waweze kupatikana washindi stahiki na wachezaji bora watakaoweza kuibuliwa na mashindano hayo
Alisema kuwa anategemea kuwa wajumbe hao watawapata viongozi wenye busara na uzalendo katika kusimamia mashindano hayo,kuibua wachezaji chipukizi watakao chukuliwa kuchezea timu zingine za Wilaya,Mkoa na Taifa na kuleta ushindani mkubwa katika soka
Alieleza kuwa wajumbe wa kamati hiyo tayari wameanza kuwasili katika viwanja vya mkutano ili kuweza kutimiza lengo la kikao na kwamba anaamini kuwa kamati hiyo itafanya kazi yake vizuri kama ilivyokusudiwa
MWISHO

Friday, January 27, 2012

TIMU YA MLALE JKT YASAJIRI KINDA KUTOKA KAHAMA UNITED

Na Stephano Mango, Songea
 
TIMU ya soka ya Mlale JKT ya Songea imesajili kinda  kutoka Kahama United ya Shinyanga katika nafasi ya kiungo katika usajili wa dirisha dogo kabla ya kuanza kwa ligi ya Daraja la kwanza mzunguko wa pili, ligi hiyo ambayo inatarajiwa kuanza Februari, 4 mwaka huu.
 
Akizungumza mjini hapa jana kocha msaidizi wa Maafande hao, Edger Msabaila alimtaja kinda hilo kuwa Dotto Mrisho ambaye alikuwa akichezea nafasi ya kiungo katika timu yake ya Kahama United na kuwa tishio kwa timu nyingine za mkoa huo.
 
Alisema wamechukua uhamuzi huo wa kusajili nafasi hiyo moja ya kiungo baada ya kukaa chini na kamati ya ufundi wa timu hiyo na kuweza kubaini kulikuwepo na pengo katika mechi zake za mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kutokana na mchezaji anayechezea nafasi hiyo, Patrick Batweri kusumbuliwa  na maumivu ya mara kwa mara ya kifundo cha mguu.
 
Alieleza usajili huo wa kinda hilo umepelekea timu yao kukamilika kila idara zake na kuwataka wapenzi wa soka wa mkoa wa Ruvuma wawe na matumaini ya kuvuka ungwe hiyo na kucheza tisa bora na hatimaye kucheza ligi kuu ya Bara msimu ujao
 
Alisema moyo wa matumaini hayo yamekuja kufuatia uwezo mkubwa aliouonyesha kinda huyo wa kuweza kumiliki nafasi hiyo ya kiungo ambao anauonyesha katika mazoezi na kuwa kivutio kwa watazamaji wanaofurika kushuhudia mazoezi yao yanaendelea kwenye uwanja wa Majimaji mjini hapa.
 
Mlale JKT katika mchezo wake wa kwanza duru la mzunguko wa pili wamepangwa kukutana na ndugu zao Majimaji kabla ya kucheza na Small Boys ya Rukwa na mchezo wake wa tatu itasafiri na kwenda  kukutana na Maafande a Polisi Iringa, kabla ya kurudi nyumbani na kuzisubili timu za Mbeya City na Prisons ya Mbeya.
 
MWISHO.

MDAHALO JIMBO LA SONGEA MJINI WAMALIZIKA MCHANA HUU KATIKA UKUMBI WA CHUO CHA UALIMU CHA MATOGORO SONGEA

 Washiriki wa Mdahalo huo wakiendelea kusikiliza hoja mbalimbali
 Dereva wa Sonngo Shilingi kushoto akiwa na Mjumbe wa Roa Venas Komba
 Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini akijibu hoja mbalimbali zilizoelekezwa kwenye ofisi ya Mbunge
 Mratibu wa MVIWATA mkoa wa Ruvuma Bigambo Ladslaus akieleza jambo wakati wa mdahalo
 Mtoa Mada Oddo Hekela akiwasilisha mada kwenye mdahalo huo
 Katibu wa Sonngo Mathew Ngarimanayo akifafanua jambo wakati wa Mdahalo huo
Mtoa Mada Bashiru Mgwasa akiwasilisha mada ya umuhimu wa viongozi na wajibu wa wananchi

MDAHALO JIMBO LA SONGEA MJINI WAENDELEA CHUO CHA UALIMU SONGEA

 Kushoto ni Mwandishi wa Radio Maria Songea,Julius Konala,Mwandishi wa Gazeti la Majira Crecensia Kapinga
 Mtaalamu wa ICT wa Asasi ya Sonngo Boniface Bundala akifuatilia Mdahalo wa wananchi wa Jimbo la Songea unaofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Songea
 Washiriki wakiendelea kufuatilia Mdahalo huo
Wa kwanza kutoka kushoto Dereva wa Sonngo Bucard Mkuwa (Maarufu kwa jina la SHILINGI) wa pili ni Mtoa huduma wa watoto HBC wa Asasi ya Roa na Mwanaharakati na Mtaalamu wa Zana za Kilimo Wilaya ya Songea Venas Komba,wa tatu ni Mkurugenzi wa Asasi Rumed David Kakoyo
Wa kwanza kutoka kulia ni Katibu Muhtasi (Msaidizi wa Ofisi) wa Sonngo Sophia Limbuya akizungumza jambo na Mtaalum wa ICT wa Asasi ya Sonngo Boniface Bundala

WANANCHI JIMBO LA SONGEA MJINI WAANZA MDAHALO WA WAZI WENYE LENGO LA KUPATA TASWIRA YA UWAJIBIKAJI WA VIONGOZI KWA WANANCHI WAO

Mwenyekiti wa Mtandao wa SONNGO Siwajibu Gama akifungua Mdahalo,wa kwanza kutoka kulia Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Andrew Chatwanga,wa pili Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria,wa kwanza kutoka kushoto Katibu wa Sonngo Mathew Ngarimanayo,wa pili ni Meya wa Manispaa ya Songea Charles Mhagama

Kutoka kushoto Afisa Kazi Ruvuma Oddo Hekela,Diwani wa Kata ya Matarawe James Makane,Diwani wa Viti maalum Genfrida Haule

Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakifuatilia Mdahalo

ABAKWA NA WATU WATANO NA KUMSABABISHIA KIFO

Na Gideon Mwakanosya,Songea
JESHI la Polisi mkoani  Ruvuma linawasaka watu watano wasiofahamika wakazi wa eneo la Lilambo Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kuvamia  na kuingia ndani ya nyumba  kisha kumbaka Mwanamke  mwenye umri wa miaka 20  kwa kupokezana wakati akiwa amelala  na kumsababishia Kifo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma Michael Kamuhanda  alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi  majira ya saa nne usiku  kata ya Lilambo nje kidogo ya mji wa Songea.
Amesema,Inadaiwa siku ya tukio  majira ya saa nne usiku watuhumiwa hao walifanya kitendo hicho cha kinyama  na kumsababishia maumivu makali  sehemu nyeti  marehemu  ambaye hata hivyo jina lake limehifadhiwa .
Ameeleza zaidi  kuwa  watuhumiwa hao  inadaiwa baada ya kumfanyia kitendo cha unyama mwanamke huyo walimchukua  toka nyumbani kwake na kwenda kumtupa nje ya nyumba kwenye shamba la migomba  ambapo watu waliokuwa wakipita kwenye eneo hilo walishituka kuona mwili wa marehemu ukiwa umelazwa  katika shamba hilo.
Amefafanua zaidi kuwa mara baada ya wananchi wa kata hiyo kuona mwili huo walitoa taarifa kwa viongozi wa  serikali ya kata  ambao ndio waliotoa taarifa kwenye kituo kikuu cha polisi cha Songea , na kuwa askari polisi wakiwa wameongozana na daktari walifika katika eneo la tukio na kuuchukua kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambapo waligundua kuwa sehemu zake za siri zinamchubuko.
Kamanda Kamuhand amesema kuwa wakati Polisi wanaendelea kuwasaka watuhumiwa  bado  inaendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Mwisho.
 

Wednesday, January 25, 2012

WAZAZI WAKIWA KUFUATILIA MAENDELEO YA ELIMU YA MTOTO WA KIKE

                   Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Madaha

Na Augustino Chindiye,Tunduru

SERIKALI imewataka Wazazi na Walezi kusimamia na kufuatilia kwa karibu maendeleo ya Watoto wao hasa wa kike zikiwa ni juhudi za kuhakikisha kuwa watoto hao wanafanya vizuri katika masomo yao na kujiletea maendeleo yao.

Wito huo umetolewa kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma
Madaha na kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Manfred Hyera wakati akiongea na Wadau wa elimu waliohudhuria katika mafunzo
ya uzinduzi wa Mradi wa Usimamizi na Utetezi wa Haki ya Mtoto wa kike kupata elimu yaliyofanyika katika ukumbi wa Skyway mjini hapa.

Alisema ili kufanikisha hali hiyo serikali imejipanga kutoa elimu kwa kuwaomba wazazi na walezi kuchangia chakula ili kufanikisha watoto wao kuanza kupata chakula mashuleni kama kivutio kwa wanafunzi kupenda masomo.

Akizungumzia mila na destuli za makabila ya Wayao alisema kuwa tayari serikali imeunda kikosi kazi cha kuonana na viongozi wa mila, makungwi na manyakanga kuwaelimisha juu ya utoaji wa elimu kwa watoto wa kike kupenda masomo tofauti na sasa ambapo kundi hilo limekuwa likifundishwa kukabiliana na maisha ya ndoa hali iliyo sababisha kuwepo kwa matukio mengi ya ndoa za utotoni wakiwa shuleni.

Wakiongea kwa nyakaka tofauti baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Hadija Hasan na Amina Mwajesa katika maoni yao juu ya kinachosababisha elimu kushuka Wilayani humo walidai kuwa Kipato duni cha akina mama ambao mara nyingi ndio wamekuwa wakiachiwa jukumu la kutunza Watoto wa kike .

Kuhusu mila na desturi za makabila hayo washiriki hao waliiomba
Serikali kuchukua hatua za makusudi kusimamia na kutokomeza  mila hizo hasa mafunzo mabaya ambayo hutolewa wakati wa jando na unyago pamoja na kuwataka akina mama kuacha tabia za kutunza siri za watoto wao wa kike.

Akisoma risala ya mafunzo hayo Mwakilishi kutoka shirika lisilokuwa la kiserikali la TUFAE Educcation Aids Trust linalo ratibu mafunzo hayo Hakimu Kilowa alisema kuwa mafunzo hayo yamefuatia majibu mabaya baada ya utafiti uliofanywa na shirika hilo mwaka 2007 hadi 2010 juu ya maendeleo ya elimu kwa mtoto wa kike wilayani humo.

Kilowa alisema katika utafiti huo uliofanyika katika Tarafa za
Muhuwesi,Namasakata,Ligoma,Nandembo,Mlingoti Mashariki na Mlingoti Magharibi zilibainisha kuwapo kwa kundi kubwa la watoto wa kike waliopata mimba pamoja na kikwazo cha uelewa mdogo wa jamii juu ya SERA ya Elimu,Haki ya mtoto wa kike kupata Elimu,Mila zilizopitwa na wakati.

Alisema Takwimu hizo zilifafanua kuwa katika kipindi cha Mwaka
2007-2010 jumla ya waliotarajiwa kuandikishwa shule ni watoto wa kike 17,386, walioandikishwa ni 14,692 ambao ni Sawa na asilimia 85.49%  na waliosajiliwa ni 13,411,waliofanya mitihani wa kumaliza darasa la saba walikuwa 13,097 ambao ni sawa na asilimia 97.65%, huku kukiwa na anguko la watoto 314 ambao waliacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo kupata mimba wakiwa shuleni pamoja na utoro.

Awali akitoa ufafanuzi wa mafunzo hayo Meneje wa Mradi wa shirika hilo John Nginga katika maelezo yake alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anapata elimu kuanzia darasa la awali, elimu ya msingi, sekondari hadi Chuo Kikuu.

Mafunzo hayo ya siku 15 yanayofadhiliwa na Shirika la The Foundation for Civi Society (FCS) la Jijini Dar Es Salaam  yatahusisha wadau 180 kutoka katika makundi ya Walemavu,walimu, wazee,Viongozi wa Vyama vya Siasa, Dini,Watendaji Kata na Vijiji kutoka katika Kata Sita hizo kwa ajili ya kupeana mbinu na kubainisha changamoto zinazotokana na vikwazo vya Mtoto wa kike kupata Elimu badala ya kuwa ozesha wakiwa
wadogo.

Mwisho.

Tuesday, January 24, 2012

WASAFIRISHAJI WA MIZIGO WAULALAMIKIA UONGOZI WA MANISPAA SONGEA

Na Stephano Mango,Songea
WASAFIRISHAJI wa mizigo wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameulalamikia uongozi wa Manispaa hiyo kwa kitendo cha kuwazuia  kuingia na magari ya mizigo katikati ya mji wafanyabiashara wachache huku wengine wakiingia na magari ya mizigo bila kuchukuliwa hatua yoyote
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari jana mjini hapa,wasafirishaji hao ambao waliomba majina yao yahifadhiwe,walisema kuwa kitendo kinachofanywa na Uongozi wa Manispaa  ni cha uonevu kwa sababu wamewazuia kuingia na magari katikati ya mji bila kuwatengea maeneo mengine yenye miundombinu mizuri ya maji,choo,ofisi na umeme
Walisema kuwa wasafirishaji wengi wana ofisi zao katikati ya mji ambazo zinahuduma zote muhimu ambapo uwepo wake unawasaidia wateja wao kuweza kuchukua mizigo yao kwa urahisi na kwa bei ndogo hivyo uwepo wa ofisi mbali kinawaletea usumbufu wananchi ambao ni wateja muhimu kwao
Walieleza kuwa pamoja na kupokea maelekezo ya Viongozi wa Manispaa kuwa magari yanayotakiwa kuingia mjini yasizidi tani 10 lakini kuna baadhi ya magari yanaingia na hayachukuliwi hatua yoyote na maagizo ya Viongozi hao yanabadilika kila wanavyoamua bila kujali usumbufu unaojitokeza kwani awali walituambia gari za tani 10 ndizo zinazopaswa kuingia mjini lakini baada ya wiki moja kwisha wanatuambia gari za 9 ndizo zinapaswa kuingia mjini
Walisema kuwa kutokana na usumbufu huo Wasafirishaji wanalazimika kupandisha bei ya kusafirisha mizigo na kusababisha wananchi kupandishiwa bei ya bidhaa kwani kila inachokifanya Serikali dhidi ya wafanyabiasha mwisho wa siku gharama hizo zote zinapaswa kulipwa na mwananchi mnyonge na kusababisha gharama za maisha kupanda sana
Walieleza zaidi kuwa miji mingine yote  nchini gari zinaingia mwisho gari za tani 10 ili kuweza kulinda barabara za ndani ya mji na kupunguza msongamano katikati ya mji lakini hapa tunashangaa kuambiwa kuwa gari zinazotakiwa kuingia mjini mwisho za tani 9 tena ziingie usiku wakati gari hizo hazipo
Walifafanua kuwa wameelekezwa kuanzia disemba 31 mwaka 2011 walitakiwa kutoingia kwenye barabara za mjini badala yake waishie na kushusha mizigo kwenye uwanja wa nanenane na sio vinginevyo wakati eneo hilo ni uwanja uwezi kujenga choo,hakuna huduma ya umeme,ofisi za wasafirishaji ,maji,chakula hivyo wametupatia wakati mgumu sana wa kuitunza mizigo ya watu na utunzaji wa mazingira
Walisema kuwa maagizo ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea yamejaa utata hata wanaopaswa kusimamia maagizo yake wamekuwa wakishindwa kuyazuia magari yote kuingia katikati ya mji na ndio maana magari mengine yamekuwa yakipita bila maelezo yoyote kutokana na udhaifu wa viongozi hao
Awali kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Nachoa Zakaria,Afisa Biashara wa Manispaa hiyo  Kelvin Challe aliwaandikia barua tarehe 12 Disemba,2011 wasafirishaji yenye kumb,na,SO/MC/T.10/14/11 kuhusu kusitisha kuingia magari ya mizigo yanayozidi tani 10 ndani ya barabara za Manispaa kuanzia Disemba 31,2011
Baada ya agizo hilo kuhojiwa na Wasafirishaji kutokana na kugubikwa na utata Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea   tarehe 9 Januari 2011, iliwaandikia tena wasafirishaji barua na kusaini na Kelvin Challe yenye Kumb.Na.SO/MC/T.10/14/11/17 yenye kichwa cha habari Ufafanuzi wa kina juu ya zoezi la kusitisha kuingiza magari ya mizigo kuanzia tani 10 ndani ya barabara za Manispaa Songea Kuanzia tarehe 31/12/2011
Sehemu ya barua hiyo inasema…..magari  yanayoruhusiwa  ni magari yenye uzito wa kuanzia tani 9 tu.Magari yenye  uzito zaidi ya tani 9 yanatakiwa kushusha mizigo katika uwanja wa nanenane,hivyo unatakiwa kuzingatia na kutekeleza maamuzi hayo
Jitihada za kumpata Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea aweze kujibu malalamiko ya wasafirishaji  Nachoa Zakaria ziligonga mwamba baada ya kuambiwa na mhudumu wa Ofisi yake kuwa yupo kwenye vikao ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na alipotafutwa kwenye simu yake ya kiganjani,simu iliita bila kupokelewa
MWISHO

Monday, January 23, 2012

WASHAURIWA KUTOJITOA KWENYE TAASISI ZA FEDHA WAKATI WA MTIKISIKO WA KIUCHUMI WA VYAMA HIVYO

Na Stephano Mango,Songea
WANACHAMA wa Chama  Cha  ushirika cha Akiba na Mikopo  cha walimu Songea Manispaaa wameshauriwa kuacha tabia ya kujitoa  uanachama kutokana na kukosa uvumilivu baada ya mikopo yao kuchelewa kutolewa kwa wakati  au wanapokosa mikopo  na badala yake  wametakiwa kuwa wavumilivu.
Wito huo umetolewa jana na Meneja mikopo wa benki ya NMB tawi la Songea Derick Fidelis wakati akifungua mkutano mkuu  wa  14 wa wanachama  wa chama hicho uliofanyika kwenye ukumbi wa Songea Club.
Amesema,Wanachama wanapaswa kuwa wavumilivu na si kukimbilia kujitoa pindi mikopo waliyoomba  kutoipata kwa wakati  na badala yake wajue kuwa matatizo hayo ni ya kawaida  hivyo wasikate tamaa wala kukimbia matatizo.
“Walimu tunapaswa kuwa  wavumilivu tuache tabia ya kujitoa uanachama pindi tunapokosa mikopo au kucheleweshewa mikopo , tuwe wavumilivu matatizo ni jambo la kawaida ,nyinyi  ni wadau wa kubwa wa NMB ili benki iendelee tunawategemea sana kwani mapato mengi ambayo yanaingia benki yanatokana na michango ya walimu,na mikopo mingi tunawakopesha walimu,”alisema Derick.
Aidha, Meneja mikopo ameahidi kuwa  benki hiyo itaendelea kuboresha huduma zaidi ili kufanikisha malengo ambayo  wateja wao wakiwemo walimu wanahitaji , ameishauri bodi ya chama hicho kukaa na kuomba mkopo ili kuweza kumalizia jengo lao ili kuinua uchumi wa chama hicho.
Akitoa  salamu wakati wa mkutano huo Mwenyekiti wa chama hicho  Martin  Challe amewataka wanachama hao kuendelea kuwa wajasili na kutokubali kuyumbishwa au kushawishiwa  kujitoa uanachama na watu ambao wasiopenda  na ustawi na maendeleo ya chama hicho.
“Tayari kunawachama ambao wamejitoa ukiuliza wanadai kuwa  kwa sababu uchumi wa chama siyo mzuri na kuchelewa kupata  mikopo  waliporudi kuomba  tena uanachama  nasi tumewakataa kwani walikimbia baada ya kuona tumeyumba,”alisema.
Mwisho.

Sunday, January 22, 2012

WATAKIWA KUWAPIMA WABUNGE WAO KWA USHIRIKISHAJI WA WANANCHI


                                  Afisa Kazi Ruvuma Oddo Hekela

Na Stephano Mango,Songea

WANANCHI wametakiwa kuwapima Wabunge na Madiwani wao ili kuweza kubaini ubora wao katika ushirikishaji wa wananchi katika eneo lake la uongozi katika kuleta maendeleo ya nchi kwa kutumia dhana shirikishi
Wito huo umetolewa jana na Afisa Kazi Ruvuma Oddo Hekela kwenye mdahalo  wa wazi wenye lengo la kupata taswira ya uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi wao ulioitishwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Songea(Sonngo)kwa ufadhiri wa Shirika la The Foundation For Civil Society
Hekela alisema kuwa Mbunge na Diwani wote ni wawakilishi katika eneo lao la kazi ambao wamebeba jukumu la kuhamasisha wananchi katika kutekeleza majukumu ya maendeleo hivyo ushirikishwaji bora ndio maendeleo bora
Alisema kuwa ili kupima ubora wa Mbunge na Diwani lazima upime uwezo wa ushirikishwaji wa wananchi katika eneo lake ili kuweza kuleta maendeleo ya nchi kwani wote ni wawakilishi wa wananchi katika Serikali ya watu hivyo wajibu wao unafanana
Alieleza kuwa miongoni mwa majukumu ya Mbunge akiwa jimboni ni kukaa ofisini na kuhudumia wananchi kwa kusikiliza hoja zao ili aweze kuzitatua au kuzipeleka sehemu husika kwa hatua zaidi,kufanya ziara kwa wananchi ili kuweza kujua mikakati ya maendeleo,kufuatilia utekelezaji wa miradi ya kitaifa jimboni kwake inayotekelezwa na Serikali kuu kusikiliza maoni ya wananchi kuhusiana na utekelezaji wa miradi hiyo
Alieleza zaidi kuwa majukumu yake mingine akiwa jimboni ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera mbalimbali kwa kutoa tafsiri ya sera zenyewe ili wananchi wazielewe,kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi ushiriki wao katika miradi ya maendeleo
Kwa upande wake Katibu wa Mtandao wa Sonngo Mathew Ngarimanayo alisema kuwa Viongozi wanapaswa kutimiza wajibu wao kikamilifu katika kuhakikisha Sera mbalimbali zinawanufaisha wananchi ili kuweza kupunguza umaskini wa kipato unaowakabili na kuweza kuchangia pato la Taifa
Ngarimanayo alieleza kuwa ni jambo la aibu kuona Mbunge anazunguka mjini huku wapiga kura wake wanahangaika kutokana na sera mbalimbali kutokuwa wazi na wakati mwingine kushindwa kumnufaisha mwananchi kutokana na kuwa katika mazingira magumu ya upatikanaji wake na zimewekwa katika lugha ambayo mwananchi mnyonge hawawezi kuielewa
MWISHO

WAZIRI MAGHEMBE ATAKIWA KUTEMBELEA MIKOA INAYOZALISHA MAZAO YA CHAKULA

Ukiwaona kwa mara ya kwanza unaweza kusema ni vijana wa familia moja(Baba mmoja) lakini hawa sio ndugu ila ni Wanaharakati wakubwa wa Haki za Binadamu katika Mkoa wa Ruvuma

Picha hii walipiga nje ya ukumbi wa mdahalo uliofanyika katika Wilaya ya Songea,Jimbo la Peramiho,Kata ya Mtyangimbole mara baada ya kumalizika kwa mdahalo huo ikiwa ni furaha ya kumalizika kwa mdahalo huo kwa upendo na amani

Hawa vijana wana vyeo vingi sana katika jamii,lakini kwa eneo hili na madhumuni ya picha hii kila mmoja atakuwa na cheo kimoja kilichowakutanisha hapo

Kutoka kushoto ni Katibu wa Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Songea (Sonngo) Mathew Ngarimanayo,wa kwanza kulia na Afisa Habari wa Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Songea(Sonngo) Andrew Chatwanga


Mmiliki wa Mtandao huu,Stephano Mango akiendelea kuhabarisha umma katika mdahalo huo,wa pili toka kulia ni  Mwanafunzi wa Chuo cha Ustawi na maendeleo ya Jamii Rungemba Mariana Nyoni,wa tatu ni Msaidizi wa Ofisi ya Sonngo Sophia Limbuya

Na Stephano Mango,Songea
WANANCHI wa kata ya Mtyangimbole wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wamemtaka Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika Profesa Jumanne Maghembe kuona umuhimu wa kutembelea mikoa inayozalisha mazao ya chakula ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili katika msimu huu wa kilimo ili kuweza kupunguza uhaba wa chakula nchini
Wito huo umetolewa jana na Diwani wa Kata ya Mtyangimbole Meckezedeck Mwella  kwenye mdahalo  wa wazi wenye lengo la kupata taswira ya uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi wao ulioitishwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Songea(SONNGO kwa ufadhiri wa Shirika la The Foundation For Civil Society
Mwella alisema kuwa Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kama mahindi,mihogo lakini wananchi wake wamekuwa wakiendelea kukwamisha na mipango mbalimbali ya Serikali yenye malengo ya kuinua kilimo
Alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia mfumo mbovu wa ugawaji wa pembejeo za ruzuku zinazotolewa na Serikali kwa lengo la kuwainua wakulima kutokana na urasimu mkubwa unaojitokeza kuanzia ngazi ya mtaa hadi Wilaya na kusababisha kero kubwa kwa wakulima hao
Alieleza kuwa siku zote mkulima hana likizo kwani kwa kipindi chote cha mwaka yeye anahangaika na shughuli za kilimo lakini amekuwa ni maskini wa kutupwa kutokana na uzembe toka kwa viongozi wa Serikali ambao wamekosa huruma dhidi ya wakulima kwa kuwanyonya haki zao mbalimbali
Alieleza zaidi kuwa kitendo cha Serikali kushindwa kununua mahindi toka kwa mkulima msimu wa 2011/2012 na kusababisha mahindi hayo kuanza kuota yakiwa kwenye magunia maeneo mbalimbali ya maghala ni cha uonevu mkubwa kwani wakulima wengi wamekata tamaa kutokana na madeni mbalimbali yanayowakabili kutokana na uzalishaji walioufanya katika msimu uliopita
“Wakulima walitegemea kuwa msimu wa uuzaji wa mahindi wangeweza kupata fedha kwa ajili ya kuandaa msimu mwingine wa kilimo,kulipia karo za watoto,kupata mahitaji muhimu ya kibinadamu,na kulipia huduma mbalimbali za kijamii lakini imeshindikana kutokana na mipango mibovu ya Serikali kuhusu kumkomboa mkulima kwenye upatikanaji wa masoko ya uhakika wa mazao hayo”alisema Mwella
Akizungumza kwenye Mdahalo huo Katibu wa Sonngo Mathew Ngarimanayo alisema kuwa Viongozi wanapaswa kutimiza wajibu wao kikamilifu katika kuhakikisha Sera za kilimo,ushirika na masoko zinawanufaisha wakulima ili kuweza kupunguza umaskini wa kipato unaowakabili na kuweza kuchangia pato la Taifa
Ngarimanayo alisema kuwa katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika, maafisa kilimo wa ngazi zote wanapaswa wawatembelea wakulima kwenye maeneo yao ili kuweza kubaini vikwazo mbalimbali wanavyokutana navyo wakulima  katika msimu wa kilimo badala ya kukaa ofisini wakisubiri taarifa potofu toka kwa wasaidizi wao
Alieleza kuwa ni jambo la aibu kuona Mbunge anazunguka mjini huku wapiga kura wake wanahangaika na kilimo kwa kutumia dhana duni zisizokidhi viwango vya uzalishaji wa mazao kwa wengi  bila kusaidiwa na wataalamu wa kilimo na kusababisha uzalishaji kupungua kutokana na kutumia pembejeo duni
Awali Mwenyekiti wa mtandao wa Asasi zisizokuwa za Kiserikali Wilaya ya Songea (Sonngo)Siwajibu Gama akifungua mdahalo huo alisema kuwa lengo la mdahalo huo ni kuwawezesha wananchi kutambua wajibu wao na kuelewa wajibu wa viongozi wao ili waweze kukaa pamoja,kupanga na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa pamoja
MWISHO

MDAHALO WA WAZI KUHUSU KUIMARISHA MAHUSIANO KATI YA WABUNGE NA WANANCHI WAO WAMALIZIKA

 Viongozi wa Asasi ya Sonngo na Viongozi wa Serikali wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea wakiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mdahalo huo mara baada ya kumalizika

Saturday, January 21, 2012

SONNGO WAWAKUTANISHA WANANCHI WA MTYANGIMBOLE KWENYE MDAHALO WA WAZI KUHUSU KUIMARISHA MAHUSIANO KATI YA WABUNGE NA WANANCHI WAO

 Kutoka kulia ni Afisa Maendeleo ya Jamii,Halmashauri ya Wilaya ya Songea Bashiru Mgwassa,Diwani wa Kata ya Mtyangimbole Meckezedeck Mwella, Mwenyekiti wa Sonngo Siwajibu Gama,Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mwl,Mwingira,Makamu Mwenyekiti wa Sonngo Ifigenia Mbawala,wa kwanza kutoka kushoni ni Katibu wa Sonngo Mathew Ngarimanayo
 Washiriki wa mdahalo huo wakisikiliza kwa makini mada zilizokuwa zinatolewa na wataalamu wa masuala ya uwajibikaji wa wa viongozi kwa wananchi wake

 Waandishi wa Habari wakiendelea kunasa matukio mbalimbali kwenye mdahalo huo,kutoka kushoto ni Mpiga picha Mpenda Mvula,Fundi Mitambo Boniface Bundala,Mwandishi wa Star Tv na Radio Free Africa Adam Nindi
 Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Sonngo Jongo Haule
 Mwendesha ratiba katika Mdahalo huo MC Juma Nyumayo akitoa muongozo kwa washiriki
 Dj Ras akirekebisha mitambo ili washiriki wa mdahalo waendelee na libeneke husika
 Viongozi wa Asasi ya Sonno wakiwa kwenye dawati la usajiri wa washiriki wa mdahalo huo

Mzee Said Ramadhan akichangia hoja katika mdahalo huo

APANDISHWA KIZIMBANI KWA KOSA LA KUMBAKA MWANAFUNZI WA KIDATO CHA TATU

Na Gideon Mwakanosya,Songea

MTU mmoja mkazi wa mtaa wa Ruvuma katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi mkoani humo kwa
tuhuma ya kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha tatu.

Ilidaiwa Mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka Wakili wa Serikali Shaban Mwegole mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Jenifer Changani
kuwa mnamo kati ya Januari na Mei mwaka jana, mshtakiwa Sababu Iddi(18) ambaye ni mkazi wa mtaa huo alitenda kosa hilo.

Mwendesha mashtaka huyo aliendelea kudai kuwa mwanafunzi huyo anasoma shule ya sekondari Ruvuma ambapo mshtakiwa ameonekana kutenda kosa hilo huku akijua kwamba ni kosa kisheria kufanya mapenzi na mwanafunzi jambo ambalo lilisababisha kukatisha masomo.

Kadhalika wakati kesi hiyo ikiendelea mahakamani hapo Hakimu mkazi wa Mahakama ya mkoa wa Ruvuma Shangani alisema mshtakiwa ana kesi ya kujibu kutokana na shtaka linalomkabili na kwamba anapaswa kuleta utetezi wake mahakamani.

Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 14 mwaka huu itakapoletwa mahakamani kwa ajili ya kuanza kusikiliza utetezi wa mshtakiwa na kwamba mshtakiwa amerudishwa mahabusu kutokana na kukosa
mdhamini.

MWISHO.

VILABU MANISPAA YA SONGEA KUANZA KUCHUKUA FOMU USHIRIKI LIGI YA SANGA ONE

 Mwenyekiti wa SUFA Golden Sanga, Maarufu kwa jina la Sanga One
Diwani Mstaafu na Mdau wa Michezo Golden Sanga(Sanga One) akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ligi ambayo inatarajia kuanza hivi karibuni mjini hapa

Na Stephano Mango,Songea

CHAMA cha mpira wa miguu katika Manispaa ya Songea(SUFA) kimezitaka vilabu kujitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kushiriki  mashindano ya Sanga One Cup ambayo yamepangwa kufanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Sokoine katika Manispaa hiyo.
 
Akizungumza mjini hapa jana, Katibu msaidizi wa SUFA, Godfrey Mvula alisema kuwa mashindano hayo yatahusisha vilabu vyote ndani ya Manispaa hiyo ambavyo vina usajili wa kudumu kutoka kwa msajili wa vyama vya michezo nchini na vile visivyokuwa na usajili huo.
 
Mvula alisema mashindano hayo yatadhaminiwa na mmoja wa wadau wa soka na pia Mwenyekiti wa SUFA katika Manispaa hiyo, Golden Sanga  maarufu kwa jina la Sanga One  yenye lengo la kusaka vipaji vipya na kuviibua ili kuwafanya wachezaji hao kuwa tegemeo na hazina kwa Manispaa mkoa na Taifa kwa ujumla.
 
Alisema mashindano hayo yatakuwa chachu na mbinu ambayo itasaidia SUFA  kuwapata wachezaji wenye vipaji na wanaojituma wawapo uwanjani badala ya kuwatafuta kwa kuwateua kupitia  kwenye mashindano ya ligi ya wilaya au mkoa na kuishia kutafuta maslahi yao binafsi badala ya mpira uliomweka hapo.
 
 Alieleza kuwa bingwa wa mashindano hayo ataondoka na kitita cha fedha taslimu Sh. 200,000/=,  wa pili atazawadiwa fedha Sh. 100,000/= na  mshindi wa tatu ataambulia fedha Sh.70,000/=, mchezaji bora atazawadiwa fedha taaslim Sh.20,000/= na timu itakayoonyesha nidhamu ya ndani na nje ya uwanja watapata fedha Sh.20,000/=.
 
Alisema gharama ya uchukuaji wa fomu imepangwa kulipia  Sh.10,000/= ambayo itapenda kushiriki mashindano hayo na zitarejeshwa fomu hizo Januari 26 mwaka huu saa 10:30 jioni kwenye ofisi za SUFA alidai mchezaji atakaye bainika amesajiliwa na timu zaidi ya moja jina lake litaondolewa kushiriki mashindano hayo.
 
MWISHO